Raila ana kibarua kuokoa Ruto 2027
KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, anakabiliwa na mtihani mgumu wa kisiasa kuhusu iwapo ataamua kumuunga mkono Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 au la.
Wachambuzi wa siasa wanabashiri kuwa uamuzi wa Raila kushirikiana na serikali umetikisa imani ya sehemu ya wafuasi wake wa jadi, hasa kutoka maeneo ya Magharibi, Nyanza na Pwani.
Umaarufu wake, ambao kwa muda mrefu ulijengwa kwa dhana ya kupambana na mfumo dhalimu, sasa unapungua kadri anavyoonekana kuwa karibu na serikali.
Ingawa anasisitiza kuwa ushirikiano wake na serikali ni hadi 2027, kuna minong’ono kuwa huenda akamuunga Ruto 2027.“Raila alikuwa sura na sauti ya mapambano na matumaini ya wanyonge.
Lakini sasa, kwa kuungana na Ruto, amewachanganya wengi waliomsawiri kama mpiganiaji wa mageuzi,” mchambuzi wa siasa, Beatrice Kimani alisema.
Mbali na kushuka kwa umaarufu, Raila anakabiliwa na uasi wa kizazi kipya cha wapiga kura – maarufu kama Gen Z – ambacho hakina uaminifu wa kihistoria kwa vyama au viongozi wa kisiasa.
Kundi hili linaonekana kuwa na msimamo huru na halina mvuto kwa siasa za kikabila au upinzani wa jadi.
“Gen Z hawafuati viongozi kwa sababu ya historia au mapambano ya zamani. Wao wanapiga kura kulingana na masuala yanayowagusa moja kwa moja kama ajira, haki za kijamii, na uwajibikaji wa viongozi,” asema Kimani ambaye ni mtaalamu wa sera na sheria.
Matukio ya maandamano yaliyoongozwa na vijana Julai 2024 dhidi ya Mswada wa Fedha, ambapo Raila na viongozi wengine wa kisiasa walipuuzwa, yalidhihirisha wazi kwamba Gen Z wamekuwa nguvu isiyoweza kudhibitiwa na vyama vya kisiasa.
Wakati huo huo, upinzani nao umeanza kuungana bila Raila baadhi wakimvisha nembo ya msaliti, huku viongozi kama Kalonzo Musyoka, Martha Karua na viongozi wachanga kama Babu Owino na Edwin Sifuna wakionekana kujipanga kisiasa bila kutegemea ushawishi wake.
Muungano huu mpya unalenga kuchukua nafasi ya uongozi wa upinzani na kuwavuta vijana walioasi mifumo ya zamani ya kisiasa.“Tunaona kizazi kipya cha wanasiasa kikiibuka na kuleta mwelekeo tofauti.
Hii ni changamoto kubwa kwa Raila, hasa kwa kuwa anaonekana kuwa sehemu ya mfumo aliokuwa akipinga,” Profesa Macharia Munene wa Chuo Kikuu cha Amerika, aliambia jarida moja la siasa wiki hii.
Iwapo Raila ataamua kumuunga mkono Ruto 2027, haitakuwa kazi rahisi kama ilivyokuwa hapo awali alipokuwa akisema tosha na mambo yanafanyika. Si tu kwamba umaarufu wake umepungua, bali pia atahitaji kuwashawishi wapigakura wa kizazi kipya, kuunganisha wafuasi na jamii zilizo na shaka naye, na kuzuia upinzani unaojipanga nje ya kivuli chake.
“Kibarua kikubwa kwa Raila si tu kuokoa Ruto, bali pia kuokoa urithi wake wa kisiasa,” asema Dkt Kimani.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, Wakenya wanageukia kupiga kura kwa kuzingatia maslahi badala ya uaminifu wa kikabila. Anasema wapigakura sasa wanatafuta viongozi wanaoweza kujadiliana kwa ufanisi na wenzao kimawazo badala ya kufuata ‘mtu wetu.’
Anasema umaarufu wa Raila umepungua katika zilizokuwa ngome zake, hasa eneo la Magharibi mwa Kenya na Pwani.“Ushirikiano wa kisiasa kati ya Raila na Rais William Ruto umevuruga uaminifu wa Raila kikanda.
Raila amepoteza sehemu ya Magharibi kati ya maeneo mengine,” asema.Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasisitiza kuwa siasa za kikabila zimekita mizizi Kenya na zitaamua mshindi wa urais 2027 dhana ambayo Profesa Macharia Munene anapinga, akitoa mifano ya kihistoria kama ushindi wa Mwai Kibaki 2002 na kupingwa kwa chaguo la Uhuru Kenyatta mwaka 2022.
“Kupiga kura kwa misingi ya kikabila ni porojo tu. Watu hupiga kura kwa yule wanayemuona bora,” Prof Macharia alisema.