Ruto ammiminia sifa Trump kwa ushindi licha ya uwezekano wa minofu kuondolewa
RAIS William Ruto amejiweka kwenye orodha ya marais na viongozi wa mataifa mbalimbali ya ulimwengu waliotuma risala za pongezi kwa Donald Trump kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumanne, Novemba 5, 2024.
Sababu ni kwamba Kenya imekuwa mshirika wa Amerika tangu ilipopata uhuru miaka 60 iliyopita.
Kwa misingi ya ushirikiano huo, Amerika imekuwa ikitoa aina mbalimbali za usaidizi kwa Kenya katika sekta kadhaa, kama vile za usalama, uchumi, biashara, elimu, afya na hata mipango ya kukuza utawala bora na kuendeleza vita dhidi ya ufisadi.
Kwa hivyo, bila shaka, Rais Ruto anayo matarajio kwamba ushirikiano huo utaendelezwa na, labda kuimarishwa zaidi, chini ya utawala mpya wa Trump.
Hii ndio maana katika ujumbe wake wa pongezi kwa kiongozi huyo, Dkt Ruto alisema hivi: “Kenya inatarajia kuendeleza ushirikiano wake na Amerika katika nyanja muhimu kama vile, biashara, uwekezaji, tekonolojia na ubunifu, amani na usalama na maelendeleo endelevu.”
“Hii ni kwa sababu Kenya inathamini uhusiano kati yake na Amerika ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 60 na uliojengwa katika misingi ya mifumo sawa ya kidemokrasia, maendeleo na heshima,” Rais akaongeza huku akitaja ushindi wa Trump kama “kielelezo kwamba Waamerika wamerejesha imani yao kwa uongozi wake wa ujasiri na wenye maono.”
Lakini wadadisi wanaonya kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba, chini ya utawala wa Trump, Rais Ruto na serikali yake itapoteza baadhi ya “minofu” ambayo Amerika iliahidi Kenya mwezi Mei mwaka huu.
Ahadi hizo zilitolewa wakati wa ziara rasmi ya Dkt Ruto nchini humo ambapo mikataba ya thamani ya mabilioni ya fedha ilitiwa saini.
Kwa mfano, Kenya aliahidiwa usaidizi wa thamani ya Sh52 bilioni katika nyanja za uendelezaji wa misingi ya demokrasia, Haki za Kibinadamu, Uongozi na Afya.
Aidha, Amerika iliahidi kuipiga jeki Kenya katika mipango ya kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, na ile ya kustawisha biashara na uwekezaji, uchumi wa kidijitali, vita dhidi ya ugaidi miongoni mwa mingine.
Lakini Dkt Osiemo Opiyo anasema kuwa chini ya Trump Kenya itapoteza ufadhili katika nyanja za kuendelezaji wa misingi ya demokrasia, haki za kibinadamu na vita dhidi ya ufisadi.
“Hii ni kwa sababu ilivyodhihirika katika utawala wake uliopita, sera za Trump kuhusu Afrika ilijikita katika masuala yanayofaidi Amerika moja kwa moja badala ya masuala ya uongozi,” anasema mhadhiri huo wa Chuo cha Harvard Business School.
“Hii ndio maana kwa mfano, kauli mbiu ya Trump katika uchaguzi wa mwaka huu ni ‘Make America Great Again’ (Ifanya Amerika inawiri tena)”, anaeleza.
Kenya, pia itapoteza ufadhili katika mipango ya kupambana na madhara ya kabadiliko ya tabia ambao utawala wa sasa wa Joe Biden aliazimia kutoa.
Hata hivyo, Dkt Opiyo anaongeza, kuna uwezekano mkubwa Trump ataendelea kuunga mkono mkataba wa kibiashara kati ya Amerika na Kenya kwa “sababu itawasaidia Waamerika.”
Naye aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni Macharia Kamau alisema kuwa Amerika itaendeleza usaidizi wake kwa Kenya katika nyanja ya usalama, “hata kama Trump ataibuka mshindi”.
“Vita dhidi ya ugaidi katika ukanda huu wa Afrika ni muhimu zaidi kwa Amerika. Kwa hivyo, usaidizi katika nyanja hii utaendelezwa hata endapo chama cha Democratic kitaondolewa mamlakani,” akasema juzi kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen.