Jamvi La Siasa

Ruto: Nimepoteza nguzo na mlezi wangu kisiasa

Na SAMMY WAWERU October 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amemuomboleza aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga akisema kifo chake ni “pigo kwake.”

Akiongea Jumapili, Oktoba 19, 2025 kwenye mazishi ya Bw Odinga yaliyofanyika nyumbani kwake Jooust, Bondo, Kaunti ya Siaya, kiongozi wa nchi katika rambirambi zake alikiri kuondokewa na rafiki wa karibu.

Dkt Ruto aliambia waombolezaji kwamba Raila Odinga alikuwa mlezi wake kisiasa. “Mashabiki’ wengi kwenye vyombo vya habari wanasema kifo cha Raila Odinga ni pigo kuu kwangu, ndio, ninawajibu ‘Ni pigo kuu kwangu,’” akasema Rais.

Ruto, kupitia kauli hiyo inaashiria kwamba alikuwa akilenga wapinzani wake kisiasa kuhusu uwezekano wake kutwaa wadhifa wake kwenye uchaguzi mkuu 2027.

Naibu rais aliyebanduliwa mwaka uliopita, 2024, Rigathi Gachagua, pamoja na wapinzani wenza wamekuwa wakimpiga kisiasa Rais Ruto wakiapa kuhakikisha atahudumu muhula mmoja pekee.

Akizungumza kwenye hafla ya maziko ya Bw Odinga, Rais alisema endapo chama cha ODM – kilichoongozwa na Odinga, hakitakuwa kwenye serikali baada ya 2027 basi huenda kikaunda serikali.

Rais Ruto aliapa kuhakikisha kwamba chama hicho ambacho kimekuwa kikimuunga mkono tangu 2024, baada yeye na Bw Odinga kuanza kushirikiana, hakuna atakayekisambaratisha.

“Urafiki wangu na Baba (Raila Odinga) ulianza 1997 nilipochaguliwa mbunge kwa mara ya kwanza,” Ruto akasema, akisimulia historia yao kuunda urafiki.nKiongozi wa taifa alimsifia Odinga akimtaja kama mlezi wake kisiasa na pia baba.

Aidha, iwapo angekosa kuwahi urais 2022 bado ushindi ungesalia kwake kwa sababu wawili hao wamekuwa marafiki kwa muda. Wakati wa kampeni, hata hivyo, wanasiasa hao wakimenyana hawakuwa ‘wakionana’.

Rais Ruto, aliambia waombolezaji kwamba miezi michache baada ya kutwaa serikali kutoka kwa mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, alimfikia Odinga na kumrai washirikiane. Alidokeza kuwa chambo chake kilimnasa na wakaishia kufufua urafiki wao wa tangu jadi.

Akitetea maamuzi kumpa Bw Odinga mazishi ya kitaifa, alisema “Hata ingawa hajawahi kuwa rais wa Kenya, amekuwa rais wa wananchi.” Bw Odinga anatarajiwa kupata heshima za kijeshi – mizinga kufyatuliwa.