Jamvi La Siasa

Siogopi kuvuliwa ukatibu wa ODM, sasa asema Sifuna

Na JUSTUS OCHIENG January 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIBU Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amesema haogopi kuvuliwa wadhifa huo huku akipuulizia mbali uwezekano wa chama hicho kinachoongozwa Raila Odinga kuungana na kile cha UDA cha Rais William Ruto kabla ya uchaguzi wa 2027.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Sifuna alieleza kuwa ODM itaungana tu na vyama vilivyo na malengo sawa na yake na ambavyo itikadi zao zinafanana na zinazoegemea kumlinda raia.

“Asili ya siasa zetu wakati mwingine inahitaji tuingie katika mipango ya kimkakati na vyama vya siasa vilivyo na nia sawa na yetu. Neno muhimu hapa ni kuwa na nia sawa. Vyama vya kisiasa ambavyo itikadi zao zinafanana na sera za ODM vinajulikana. Hivyo vinafaa kuwa tunavyotafuta kushirikiana nazo, wala si vile vinavyokandamiza raia,” Bw Sifuna alisema.

Msemaji huyo wa ODM pia alizungumzia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwa nini wanachama wa chama chake waliojiunga na baraza la mawaziri la rais Ruto wamejitenga na msimamo wa chama.

Wao ni waliokuwa naibu viongozi wa chama cha ODM Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM John Mbadi na aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi pamoja na aliyekuwa mwanachama wa bodi ya uchaguzi Bi Beatrice Askul.

“Wale kutoka chama chetu waliojiunga na serikali wako huru kuzungumza kuhusu jinsi watakavyopiga kura zao kibinafsi mnamo 2027 lakini hawazungumzi kwa niaba ya chama. Baba (Bw Odinga) amesema wazi, lazima tuandae chama kwa uchaguzi wa 2027, msimamo ambao umeidhinishwa na Kamati Kuu ya chama chetu,” akasema Bw Sifuna.

Bw Sifuna, ambaye pia ni seneta wa Nairobi alisema haogopi vitisho vya kufurushwa ofisini kutoka kwa baadhi ya wanachama kutokana na msimamo wake mkali wa kupinga Serikali Jumuishi.

“Ninashikilia wadhifa wa Katibu Mkuu kwa hisani ya wanachama, na sitaushikilia milele. Wanasema usipotetea maadili yako unapojaribiwa, utakuwa ukijifurahisha tu na si maadili. Imekuwa heshima ya maisha yangu kuhudumu kama katibu mkuu wa ODM. Mwaka jana nilikua katibu mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya chama. Mnamo Februari ninaanza mwaka wangu wa 8. Kila siku katika miaka saba iliyopita nimekuwa nikisikia vitisho sawia kutoka kwa watu hao na bado niko hapa,” alisema.

Alisisitiza kuwa wito wake kwa wanachama wa ODM kuacha kuunga chochote wanachosema au kufanywa na washindani wao ulitoka kwa uongozi wa chama baada ya kikao cha Kamati Kuu na haukuwa msimamo wake binafsi.

“Kama Katibu Mkuu pia nina wajibu wa kuzingatia maazimio yanayotolewa na asasi za chama na ndiyo maana nilizungumza kuhusu hilo huko Siaya. Kazi ya kulinda ODM ni yangu kama Katibu Mkuu. Ninaamini kwa dhati kwamba idadi kubwa ya wanachama wa ODM na Wakenya kwa jumla wanataka mambo haya yasemwe. Ni kazi yangu na nitaendelea kuifanya,” alisema.

Akiwa Siaya wiki jana wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu Kenya (KNCHR) Rosylene Odede, Bw Sifuna alikosoa wanachama wa ODM wanaounga serikali licha ya maovu inayohusishwa nayo.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA