Ujanja wa Ruto kurithi ngome za Raila
RAIS William Ruto ameanza kampeni ya kunyakua maeneo ya Magharibi na Nyanza huku akiwania kuchaguliwa kwa muhula wa pili 2027.Katika mkakati wake mpya, anawalenga wakazi wa maeneo hayo wanaojumuisha Waluo, Waluhya, Abagusii na Wakuria.
Amepunguza ziara zake eneo la Mlima Kenya, nguzo kuu ya kuchaguliwa kwake 2022 na kuongeza safari zake katika maeneo ya magharibi mwa nchi na haonyeshi dalili ya kuzipunguza.
Ukuruba washangaza wengi
Rais Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wanaendelea kushangaza wengi kufuatia ukuruba wao licha ya kuwa mahasimu wakali wa kisiasa kabla na baada ya uchaguzi wa 2022.
Bw Odinga alipowakabidhi baadhi ya washirika wake wa karibu ‘wataalamu kusaidia kuendesha’ serikali ya Kenya Kwanza, wengi walishuku nia yake.
Hata hivyo, wadadisi na wanasiasa waliozungumza na Taifa Jumapili wanaamini kuwa wawili hao waliafikia makubaliano ambayo yatafaidi kila mmoja.
Hii ni pamoja na Dkt Ruto kuhakikisha kuwa mpinzani wake wa zamani anachaguliwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, ambayo muhula wake utaendelea hadi baada ya 2027, huku Bw Odinga akiacha kukosoa serikali na kuwakabidhi wafuasi wake kwa Dkt Ruto ili kumsaidia kushinda muhula wa pili.
Washirika wa Raila kuunga Ruto hadharani
Kwa kuruhusu washirika wake kumuunga mkono Dkt Ruto hadharani, kuwateua watu zaidi kutoka upinzani serikalini na kufanya ziara nyingi katika ngome za Bw Odinga na kufufua na kuagiza miradi mikubwa katika eneo la Magharibi, Rais Ruto haachi chochote kuvutia eneo hilo kabla ya uchaguzi wa 2027.
Baadhi wanaamini anajihatarisha kwa kuangazia zaidi upande huo wa nchi baada ya kupoteza eneo la Mlima Kenya. Alikita kambi katika eneo hilo siku za mwisho za Disemba, ambapo pia alifika Kisii kukaribisha mwaka mpya na kushinda huko siku iliyofuata.
Ijumaa wiki jana, Rais alifanya ziara ya ghafla katika Kaunti ya Homa Bay, na kuwashangaza wengi, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani ambaye alikiri kwamba hakufahamu kuwa Rais alikuwa katika Kaunti ya Nyanza Kusini.
Hata hivyo, ziara ya ghafla ya Ijumaa haikuwa ya kwanza kwa Rais Ruto katika eneo hilo, ambako alikaribishwa na Gavana Gladys Wanga.
Ziara za mara kwa mara Nyanza
Alikuwa huko Februari mwaka jana na tena alipozuru kaunti nne za Nyanza miezi kadhaa baadaye. Wadadisi wa masuala ya kisiasa Mbw Dkt Obora Okoth, Mark Bichachi na Bw Daniel Orogo wanasema hatua hiyo ya Rais inatokana na kupoteza Mlima na inambidi atafute njia ya kufidia kura hizo ili kuweka hai azma ya kuchaguliwa tena.
“Rais anajua wazi: ukitaka kusawazisha kura za Mlima, geukia Magharibi mwa Kenya. Akiweza kupata Nyanza, Magharibi na Gusii, atakuwa amefanikisha mengi katika azma yake ya kuchaguliwa tena,” asema Bw Bichachi. Aidha, anashikilia kuwa Rais atafaulu tu iwapo Bw Odinga atashinda kiti cha AUC.
Kwa mujibu wa Bw Orogo, Ruto alikosea katika hesabu zake kwa kumteua Prof Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.
“Prof si mbishi kama mtangulizi wake na kwa hivyo hataweza kurudisha kura ya Mlimani,” akasema Bw Orogo.