Jamvi La Siasa

Wiki ya kufa au kupona kwa ‘makanga’ Riggy G kimbunga kikali kikimsubiri Seneti

Na WAANDISHI WETU October 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anategemea Mahakama imwokoe maseneta wanapoanza kuchambua hoja ya kumwondoa afisini Jumatano.

Bw Gachagua ambaye amekuwa akisimama kidete wakati huu ambapo dhoruba ya kisiasa inamkabili, Jumapili alielezea matumaini kuwa “matakwa ya wananchi hayawezi kubatilishwa na mawakilishi wachache.”

Akiongea hadharani kwa kwanza Jumapili tangu wabunge walipopitisha hoja ya kumbandua afisini, mbunge huyo wa zamani wa Mathira alielezea imani kuwa Mahakama itashughulikia suala hilo la kutimuliwa kwake litakapofika huko.

Naibu Rais alilitaka bunge kuheshimu chaguo la wananchi akisema alichaguliwa kwa tiketi moja na Rais William Ruto na hivyo hakufai kwamba yeye ndiye analengwa kuondolewa afisini.

Akipongeza Idara ya Mahakama kwa kuzingatia haki wakati wa kufanya maamuzi yake, Bw Gachagua alisema kuwa mahakama itaheshimu matakwa ya wananchi akiongeza kuwa “nchi nzuri huendeshwa kwa misingi ya heshima kwa utawala wa kisheria.”

“Naheshimu uhuru wa Idara ya Mahakama. Nina uhakikika kuwa mahakama zitadumisha uhuru wake, kulinda katiba na matakwa ya wananchi,” akasema Bw Gachagua.

“Mahakama zetu hufanya kazi vizuri. Majaji hulinda Katiba, utawala wa sheria na daima huhakikisha matakwa ya wananchi yanaheshimiwa. Nina uhakikisha kuwa utawala wa sheria utazingatiwa na matakwa ya wananchi kudumishwa,” akaongeza.

Bw Gachagua alikuwa akiongea katika Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kianglikana (ACK) Dayosisi ya Embu, wakati wa maadhimisho ya miaka 34 tangu kuanzishwa kwa dayosisi hiyo.

Huku akiwasifu wabunge 44 waliopiga kura ya kupinga hoja hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, Naibu Rais aliwahimiza viongozi kusikiza matakwa ya raia.

Aliwasihi Wakenya wamwombee na taifa wakati ambapo joto la kisiasa limepanda baada ya wabunge kupitisha hoja ya kumtimua wiki jana.

Vile vile, aliwataka Wakenya kusalia watulivu pasina kujadili matokeo ya uamuzi wa Seneti kuhusu hoja hiyo.

Bw Gachagua ambaye alikuwa ameandamana na mkewe Dorcas Rigathi, hata hivyo alisema yu tayari kwa uamuzi wowote kutoka kwa Seneti.

Aidha, aliandamana na viongozi kadhaa akiwemo Mbunge wa eneo hilo (eneo bunge la Manyatta) Gitonga Mukunji, Mbunge Mwakilishi wa Embu Pamela Njoki Njeru, almaarufu Doubl N, Onesmus Ngogoyo (Kajiado Kaskazini), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), George Koimburi (Juja), seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Laikipia Cate Waruguru na madiwani.

Mnamo Jumatano Bunge la Kitaifa, likiongozwa na Bw Mutuse (Mbunge wa Kibwezi Magharibi) litawasilisha kesi yake mbele ya seneti mwendo wa saa sita adhuhuri.

Bunge hilo litawasilisha ushahidi wake na mashahidi hadi saa kumi na nusu joni. Kisha mawakili wa Bw Gachagua watawahoji mashahidi hao kwa saa mbili hadi saa kumi na mbili na nusu jioni.

Baadaye, Maseneta watapewa muda wa saa moja kuwauliza maswali na kusaka ufafanuzi kabla ya shughuli za siku hiyo ya kwanza kutamatishwa.

Bw Mutuse na Bunge la Kitaifa watawatumia Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Katibu katika Baraza la Mawaziri Mercy Wanjau na aliyekuwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KEMSA Andrew Mulwa kama mashahidi wao.

Bw Gachagua atawakilishwa na jopo la mawakili wakiongozwa na Wakili Mkuu Paul Muite.

Wengine ni pamoja na; Victor Swanya, George Wandati, Faith Waigwa, Elisha Ongoya, Ndegwa Njiru, George Sakimpa, Murigi Kamande, Amos Kisilu, Tom Macharia na Julia Omwamba.

Kwa upande mwingine Bunge la Kitaifa pia limekodi huduma za jopo la mawakili likiongozwa na Wakili Mkuu Paul Nyamodi.

Bw Nyamodi atasaidiana na akina Eric Gumbo, Kipkogei Moses Kipkemboi, Muthomi Thiankolu, Peter Wanyama, Melly Kennedy Kipkoech, Joan Jeruto, Muriuki Eric Mwirigi, Mwereru Boniface Mawira na Ondago Kevine Otieno.

Bw Gachagua anakabiliwa na mashtaka 11 ikiwemo kukaidi uamuzi uliopitishwa katika baraza la mawaziri la kuwafurusha watu waliojenga makazi ndani ya eneo la mita 30 kutoka kingo za mito katika kaunti ya Nairobi.

Kwa kufanya hivyo, Naibu Rais alikiuka kanuni ya uwajibikaji wa pamoja wa wanachama wa Baraza la Mawaziri.

Pia anakabiliwa na tuhuma ya kuingilia mipango ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi ya kuwahamisha wafanyabiashara kutoka Soko la Wakulima hadi Soko jipya lililoko katika Barabara ya Kangundo, eneo bunge la Embakasi Mashariki.

Mnamo Alhamisi asubuhi itakuwa zamu wa Naibu Rais kujitetea dhidi ya mashtaka yote yaliyoelekezwa dhidi yake na Bunge la Kitaifa

Katika wasilisho litakaloanza saa tatu asubuhi, Bw Gachagua atawasilisha ushahidi, hatikiapo na mashahidi hadi saa saba mchana.

Inasemekana kuwa Naibu Rais atawasilisha mashahidi kadhaa lakini mawakili wake wamedinda kuwatambua kwa majina wala kufichua idadi yao.

Saa moja itatengwa ya kuhojiwa kwa mashahidi wa Bw Gachagua, shughuli itakayoendelea hadi saa tisa na nusu alasiri.

Baada ya hapo maseneta watapewa muda wa saa moja kuuliza maswali na fafanuzi.

Saa mbili zitatengewa taarifa za mwisho kutoka pande mbili husika kabla ya mjadala kamili kuanza kuanza saa kumi na mbili na nusu jioni.

Mjadala huo unaotarajiwa kushuhudia cheche na malumbano makali utaendelea hadi saa mbili na nusu usiku kisha kutoa nafasio kwa kipindi cha upigaji kura.

Bw Gachagua atakuwa ameondolewa afisini rasmi ikiwa angalau maseneta 45 kati ya 57 watapiga kura kuidhinisha mojawapo kati ya mashtaka 11 dhidi yake.

Ripoti ya COLLINS OMULO, GEORGE MUNENE NA DAVID MUCHUI

Tafsiri: CHARLES WASONGA