Jamvi La Siasa

Yafichuka Ruto alikataa juhudi za viongozi wa kidini kumpatanisha na Gachagua

Na KAMORE MAINA, BENSON MATHEKA October 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

JUHUDI za viongozi wa kidini kupatanisha Rais William Ruto na Naibu Wake Rigathi Gachagua ziligonga mwamba mapema wiki hii.

Mnamo Jumatatu, Oktoba 7, mwendo wa saa nne na dakika arobaini na tano asubuhi, Bw Gachagua alipokea simu muhimu.

Wakati huo, Bw Gachagua alikuwa katika mkutano na watu wa karibu wa familia yake na mawakili wakitayarisha hotuba yake kwa Bunge la Kitaifa wakati wa hoja ya kuondolewa mamlakani siku iliyofuata.

Ni aina ya simu ambayo mtu anayekabiliwa na vita vikali jinsi alivyokuwa, ingezua hisia tofauti- aidha alikuwa akipata msaada au shida zake zilikuwa zikizidi kuwa mbaya zaidi.

Kwenye simu alikuwa Rais William Ruto. Bw Gachagua na bosi wake walikuwa hawajazungumza kwa muda mrefu tangu mara ya mwisho walipokutana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) mnamo Julai.

Bw Gachagua alikuwa na matumaini na alitarajia rais alimpigia simu kumhakikishia kila kitu kitakuwa sawa au kumpa fursa ya kusuluhisha tofauti zao.

Hata hivyo, haikuhusu moja ya mambo hayo mawili.

Badala yake, ilichukua chini ya dakika moja kwa rais kupitisha ujumbe wake kwa naibu wake. Baada ya simu hiyo, ilikuwa wazi kwa Bw Gachagua kwamba alikuwa peke yake.

Wanaofahamu matukio hayo waliambia Taifa Leo kwamba kabla ya simu hiyo, Bw Gachagua alikuwa ametuma wajumbe kwa rais katika jaribio la mwisho la kujiokoa. Juhudi hizo zilifeli jambo ambalo linaashiria ujumbe mbaya katika simu hiyo ya Jumatatu.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed hakujibu maswali ya Taifa Leo kuhusu simu hiyo ya rais, juhudi za upatanishi na kimya chake kuhusu masaibu yanayomkabili naibu wake.

Iliibuka kwamba Jumapili, siku ambayo naibu rais aliomba msamaha hadharani kutoka kwa bosi wake na wabunge katika ibada ya kanisa, Rais Ruto alikuwa amekutana na kundi la viongozi wa kidini waliokuwa katika juhudi za kuwapatanisha wawili hao.

Askofu wa Kanisa Katoliki Anthony Muheria, Askofu Mkuu wa kanisa la ACK James Ole Sapit, kiongozi wa SDA Samson Nyaberi na viongozi wa makanisa ya kiinjilisti walikuwa miongoni mwa walioongoza juhudi za kupatanisha Gachagua na bosi wake.

Viongozi hao wa kidini walitaka kujua sababu ya mzozo kati ya viongozi hao wawili na wanavyoweza kuzika tofauti zao.

Kulingana na vyanzo vilivyofuatilia mazungumzo, rais alisema naibu wake amejitenga na wabunge wengi kwa ukali wake. Rais Ruto pia alimshutumu naibu wake kwa kupiga vita sera za serikali na kutotangaza miradi inayotekeleza katika eneo la Mlima Kenya. Lakini mbaya zaidi, rais anaripotiwa kugusia mpango wa naibu wake ambao ulikuwa chanzo cha tofauti zao zisizoweza kusuluhishwa.

“Ninaweza kuthibitisha kwamba baadhi ya maaskofu na hata mimi mwenyewe tulifanya majaribio ya kuwapatanisha wawili hao. Ninafahamu maaskofu walikutana na rais katika Ikulu,” gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga aliambia Taifa Leo.

Baada ya mkutano wa Jumapili, Bw Mutahi aliongeza, rais aliahidi kukutana tena na viongozi wa kidini siku iliyofuata ambao hata hivyo haukufanyika.

Bw Kahiga alisema mnamo Jumatatu, mkesha wa hoja ya kumtimua katika Bunge la Kitaifa, yeye binafsi aliwaita baadhi ya wabunge wa Mlima Kenya ambao walikuwa miongoni mwa 291 waliokuwa wametia sahihi hoja hiyo akitarajia kuwashawishi kumuunga mkono naibu rais.

“Walinifanya kusubiri katika hoteli moja jijini Nairobi na hawakufika,” gavana huyo alisema.

Alhamisi, wakili Danston Omari, akizungumza kwa niaba ya Bw Nyaberi, ambaye pia amewasilisha kesi mahakamani kupinga ushirikishaji wa umma kuhusu kutimuliwa kwa Bw Gachagua, alithibitisha majaribio ya kuwapatanisha viongozi hao wawili.

“Kumekuwa na juhudi za pamoja za viongozi tofauti wa kanisa kupatanisha rais na Bw Gachagua lakini juhudi hizi hazikufaulu,” Bw Omari aliambia Taifa Leo.

Bw Omari alisema sababu iliyowafanya viongozi wa SDA kwenda kortini ni kwamba waliona hilo kama chaguo pekee lililosalia kuokoa nchi baada ya mipango inayoongozwa na kanisa kufeli.

Taifa Leo iliwasiliana na maaskofu Sapit na Muheria lakini viongozi hao wawili wa kanisa walikuwa bado hawajajibu simu na arafa.

Pia imebainika kuwa hoja ya kumtimua naibu rais ikitarajiwa kuanza wiki ijayo katika Bunge la Seneti, juhudi bado zinaendelea kuwapatanisha viongozi hao wawili kabla ya kura ya mwisho.

Lakini juhudi hizo mpya hazionekani kufaulu.

Wandani wa rais waliambia Taifa Leo kwamba wabunge wamemwambia kiongozi wa nchi hawatakubali makubaliano ambayo yatakwamisha mchakato wa kumuondoa madarakani Bw Gachagua.