Ziara ya Ruto mlimani ni mtihani kwa Rigathi, Kindiki
NAIBU Rais Kithure Kindiki na mtangulizi wake Rigathi Gachagua wanakabiliwa na mtihani mkubwa wa kisiasa huku Rais William Ruto akijiandaa kuzuru eneo la Mlima Kenya kuanzia Jumanne, Aprili 1.
Mkuu wa Huduma za Mawasiliano ya Rais, Munyori Buku, alisema kuwa Rais Ruto anatarajiwa kuanza ziara yake ya Mlima Kenya huko Laikipia Jumanne ijayo.
“Ataanza ziara ya maendeleo Jumanne, Aprili 1, huko Laikipia na kuzuru maeneo mbalimbali hadi Jumamosi, Aprili 5,” Bw Buku alisema.
Ziara hiyo, inayoonekana kama mkakati wa kuimarisha uungwaji mkono kuelekea uchaguzi wa 2027, inajiri katikati ya mvutano wa kisiasa unazidi kupanuka na mabadiliko ya uaminifu katika eneo hilo lenye kura nyingi.
Prof Kindiki ameongeza juhudi zake katika eneo hilo katika siku chache zilizopita, akizindua miradi ya maendeleo kama maandalizi ya ziara ya Rais huku Bw Gachagua akionekana kupata umaarufu baada ya kutimuliwa serikalini.
Ingawa amesisitiza kuwa ziara hiyo ni ya maendeleo pekee, wachambuzi wa siasa wanaichukulia pia kama njia ya kujaribu kurejesha umaarufu wa Kenya Kwanza katika eneo hilo.
“Wiki ijayo Rais atakuwa hapa Mlima Kenya. Na haji kufanya siasa. Anakuja kufungua masoko, kuhakikisha upanuzi wa mipango ya usambazaji wa umeme, kukagua barabara, miradi ya unyunyuzaji na miradi mingine inayoendelea katika eneo hili,” alisema Naibu Rais wakati akikagua miradi ya serikali inayoendelea katika Kaunti ya Murang’a mnamo Alhamisi.
Mtangulizi wake, Rigathi Gachagua, aliyeng’olewa mamlakani mnamo Oktoba mwaka jana, amekuwa akiendesha kampeni kali dhidi ya Dkt Ruto katika eneo hilo na kwa sasa anajipanga kuunda upinzani mpana zaidi wa kudhoofisha ushawishi wa Rais na Prof Kindiki.
Wachambuzi wa siasa, hata hivyo, wanasema mkakati wa Prof Kindiki wa maendeleo katika siasa za eneo hilo unaweza kumpa upendeleo mkubwa kwa wananchi na kupunguza ushawishi wa Bw Gachagua.
“Japo kuondolewa kwa Bw Gachagua kukitikisa miundo ya kisiasa ya Rais Ruto katika Mlima Kenya, bado Rais ana muda wa kurekebisha hali. Bw Gachagua ametumia habari za kupotosha kudhoofisha miundo ya kisiasa ya Rais Ruto katika Mlima Kenya,” alisema mchambuzi wa siasa, Dismas Mokua.
Aliongeza kuwa jukumu la Kindiki ni kuunda mkakati wa kukabiliana na mashambulizi makali ya kisiasa ya Gachagua dhidi ya Rais Ruto.
“Lengo kuu la Bw Gachagua ni kumzuia Rais Ruto kufaulu katika Mlima Kenya, kwa hivyo Kindiki anapaswa kuunda na kutekeleza mkakati ambao sio tu utapinga uongo wa Gachagua, bali pia kukuza na kuimarisha ushawishi wa kisiasa wa Rais Ruto,” alisema Bw Mokua.
Aliongeza kuwa Kindiki anapaswa kupata heshima kati ya wenzake kwa kujionyesha kama kiongozi wa mbele katika siasa za Mlima Kenya.Ziara hiyo inatarajiwa kuwa kipimo cha ushawishi wa Kindiki katika eneo hilo, ambapo Bw Gachagua na Rais wa zamani Uhuru Kenyatta wamejipanga kama viongozi wa kisiasa wa eneo hilo.
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanasema ziara ya Rais Ruto katika eneo Mlima Kenya inamuweka Gachagua kwenye hali tata.Wachambuzi wa siasa wanasema kwamba mapokezi ya Rais yataweka Gachagua katika hali ngumu.
“Hili ni jaribio gumu. Bw Gachagua ameshtumiwa sana kwa siasa za ubinafsi na kujaribu kuwaondoa watu wake serikalini,” anasema mchambuzi wa siasa, Bw Gasper Odhiambo.
Bw Odhiambo anahimiza tahadhari: “Gachagua lazima apunguze hisia za watu wake ikiwa anataka kudumisha mvuto wa kitaifa.”Anaonya kuwa ikiwa Rais atapokelewa kwa uhasama, inaweza kumdhoofisha Gachagua katika siasa za kitaifa, ambapo wakosoaji wanaweza kumshutumu kwa kugeuza Mlima Kenya kuwa ngome ya upinzani.
“Hata hivyo,” anaongeza Bw Odhiambo, “ikiwa Rais atazomwa, itathibitisha kuwa Gachagua bado ana ushawishi mkubwa katika eneo hilo.”Anaeleza kuwa Gachagua—ambaye amekuwa akishtumiwa kwa siasa za ukabila lazima ajibadilishe na kuwa kiongozi wa kitaifa.“Hili ni chaguo gumu kwa Bw Gachagua,” anasema Bw Odhiambo.
“Anapaswa kuamua kama ataruhusu Rais akaribishwe kwa uhasama ili kuthibitisha kuwa Wamunyoro bado ni moyo wa siasa za eneo hilo, au ahimize mapokezi mazuri ili kuonyesha taswira ya kitaifa.”