JAMVI: Mkataba wa Raila na Uhuru wazalisha mayatima wa kisiasa
Na WYCLIFFE MUIA
HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa NASA Raila Odinga kutangaza ushirikiano mpya inatishia mustakabali wa wanasiasa wengi walionuia kufaidi na mzozo wa mara kwa mara kati ya viongozi hao wawili.
Wachanganuzi wanakubaliana kuwa, mkutano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ulipangua pakubwa mipangalio ya sasa ya kisiasa na italazimu baadhi ya viongozi katika pande zote kujitathmini upya la sivyo, watakufa kisiasa.
Kwa mujibu wa wataalamu wa kisiasa, waathiriwa wa kwanza kabisa wa umoja wa vinara hao ni Naibu Rais William Ruto na vinara wenza wa upinzani Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).
Juhudi za Bw Musyoka kutaka rais kumpa sikio zinaonekana kugonga mwamba huku matumaini yake ya kupata uungwaji mkono wa Bw Odinga kuwania urais 2022 yakisalia kitendawili.
Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Odinga tayari kimethibitisha ushirikiano wake na serikali ya Jubilee na kumtaka kiongozi wao (Bw Odinga) asiyumbishwe na walio na azma ya kuwania urais 2022.
Wakili Kamotho Waiganjo anasema, kuna kila sababu ya Bw Musyoka na Bw Mudavadi kuwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu ni bayana macho yote yako 2022 na mkutano wa rais na Bw Odinga unazika Mkataba wao wa kisiasa wa 2017 ambapo chama cha ODM kilikubali kutoteua mgombeaji wa urais 2022 na badala yake, kuunga mmoja wa wagombeaji wa vyama tanzu.
“Iwapo mkutano wa rais na Bw Odinga ni mwanzo wa serikali nyingine ya muungano, bila shaka vigogo kadhaa wa kisiasa wanaathiriwa. Kuna uwezekano wa kuchipuka kwa miungano mingine ya kisiasa inayohusisha wanasiasa ambao hawadhirishwi na umoja wa vinara hao wawili,”anasema Bw Waiganjo.
Bw Waiganjo anahisi kuwa, japo Bw Ruto ana uungwaji mkono wa 2022 wa chama cha Jubilee, anapaswa kufuatilia kwa makini uhusiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.
Kulingana na mhadhiri wa masuala ya kisiasa Herman Manyora, shida kubwa ya kisiasa inayorudisha taifa hili nyuma, ni usaliti wa kisiasa na rais pamoja na Bw Odinga wanaweza kuleta suluhu.
Historia ya usaliti
“Shida kuu hapa ni usaliti wa kihistoria. Shida hii ilianza pale Mzee Jomo Kenyatta alipomruka Jaramogi Odinga, mtindo huu ukaendelea baada ya Mwai Kibaki kusaliti maafikiano yake na Raila.
Kisha Uhuru akaonekana kukandamiza demokrasia ambayo ingemwezesha Raila kutimiza ndoto yake ya kuwa rais. Mkutano wao uliashiria mwisho wa usaliti huo,”anasema Bw Manyora.
Kulingana na Bw Manyora, ili kutatua shida hii, sharti wanasiasa kadhaa watolewe kafara pamoja na ndoto zao za kisiasa.
Bw Manyora anahisi kuwa umoja huu utampa rais mandhari mazuri ya kutekeleza ahadi zake za maendeleo pamoja na kuunda wosia wake wa kisiasa naye Bw Odinga huenda akagawiwa mamlaka.
“Inawezekana kuwa si kweli lakini nahisi kuwa kuna mpango wa kuhakikisha Raila ameonja urais. Huu mjadala unasikia kuhusu mabadiliko ya katiba ni kuhakikisha Bw Ruto hajaachwa nje,”anasema Bw Manyora.
Katika miaka mitano iliyopita, Bw Ruto amekuwa akiunda himaya yake ya kisiasa, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kumrithi Rais Kenyatta mnamo 2022.
‘Mke mwenza’
“Lazima Bw Ruto atambue sasa ndoa yao na rais imepata mke mwenza hali ambayo huenda ikabadilisha kabisa mipango ya urithi wa urais,”anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Edward Kisiang’ani.
Prof Kisiang’ani anahisi kuwa, Bw Ruto ni yatima mkubwa wa Jubilee na mustakabali wake wa kisiasa utategemea jinsi atakavyohusiana na Bw Odinga.
Kwa upande wa NASA, MaBw Musyoka, Mudavadi na Seneta Wetangula huenda wakalazimika kusahau ndoto zao za kuwa rais, iwapo Bw Odinga atasisitiza kuwania urais tena 2022.
“Tayari umesikia baadhi ya viongozi wa Jubilee wenye misimamo mikali kama (Adan) Duale na Seneta (Kipchumba) Murkomen, wakimsifu Bw Odinga na kumtaja kama kiongozi mwenye uzalendo mkubwa. Wanafahamu vyema kuwa yeye ndiye atakayeunda siasa za 2022,” anaongeza Prof Kisiang’ani.
Kando na Duale na Murkomen, Prof Kisiang’ani anahisi kuwa Seneta wa Tharaka Nithi Kindiki Kithure vilevile ni yatima wa umoja huu ikizingatiwa kuwa alikuwa ametangaza wazi kuwa anataka kuwa mgombea mwenza wa urais wa Bw Ruto ifikiapo 2022.
Onyo
Tayari Prof Kindiki ameonya kuhusu uhusiano wa Bw Odinga na Jubilee akisema Waziri huyo Mkuu wa zamani ni ‘mtaalamu’ wa kisiasa na huenda akavuruga kabisa mpangilio wa 2022 wa chama hicho.
Iwapo Bw Musyoka na wenzake katika NASA watajumuishwa katika mkataba wa rais na Bw Odinga, viongozi walioazimia kuwania urais 2022 wataathiriwa sana kisiasa.
Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho na mwenzake wa Machakos Dkt Alfred Mutua watalazimika kutathmini upya mipango yao ya kisiasa ya 2022 kwa sababu hawatawania ugavana kwa awamu ya tatu.
Wengine ambao hatima yao haijulikani iwapo Bw Odinga atajiunga na serikali ni Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i na mwenyekiti wa chama cha Jubilee Raphael Tuju.
Dkt Matiang’i amekuwa akitoa maagizo yaliyoonekana kuwahangaisha viongozi na wafuasi wa upinzani huku Bw Tuju akitunukiwa nyadhifa zilizolenga kujumuisha jamii ya Luo.
Kando na wanasiasa, wanablogi, mabwenyenye wanaofadhili wanasiasa na vyombo vya habari vitakuwa na wakati mgumu baada ya joto la kisiasa kutulia kufuatia umoja wa rais na Bw Odinga.