MakalaSiasa

JAMVI: Uhuru apewa onyo kuhusu uasi wa kisiasa akizidi kukopakopa kiholela

March 4th, 2018 Kusoma ni dakika: 4

Rais Uhuru Kenyatta akihojiwa awali. Picha/ Maktaba

Na MWANGI MUIRURI

Kwa ufupi:

  • Uchumi wa Kenya unazua hatari ya ukaidi na Rais Uhuru anaonywa kuwa hali hiyo ya uasi huhitaji mbinu kali za kisisasa na kiuchumi kuizima
  • Raila Odinga ameonya kuwa serikali ya Jubilee imo mbioni kuwafukarisha Wakenya ikisaka pesa za mikopo ili wazifisadi
  • Hali ilivyo kwa sasa ni kuwa, mwananchi wa kawaida katika taifa hili ako na deni la Sh120, 000 na ni deni ambalo litadumu kwa miaka 30 ijayo
  • Kwa sasa kiwango cha mikopo ni 50:54 kumaanisha pato la Kenya kwa mwaka limelemewa kwa asilimia nne na deni
  • Hali ni kwamba, taifa linakopa likitarajia kuwa uchumi wake utaimarika. Desturi ni kwamba, uchumi wa Kenya hujikokota katika kupanuka

WACHANGANUZI wa masuala ya kisiasa wanaonya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta kuwa anacheza kamari hatari na uthabiti wa kiuchumi ambapo mikopo ambayo imetinga Sh4.6 trilioni inaweza kuzua ukaidi mkuu wa kisiasa.

Ina maana kuwa Kenya kwa sasa ni taifa la 14 barani Afrika kuwa na madeni makubwa na yanayoashiria hatari kwa uthabiti wa maisha ya wananchi wa kawaida.

Nao Wakenya wanapewa ushauri kuwa wakiangalia noti ya Sh50 nchini na waone imechafuka na kuzeeka, ina maana kuwa uchumi uko taabani. Hii ni kwa sababu noti hiyo ndiyo ya kiwango cha chini zaidi katika sarafu na ndiyo hutumika sana na Wakenya wa kipato cha chini.

Wanaambiwa kuwa ukiiona imechafuka na kuzeeka, ina maana kuwa inasambazwa katika uchumi kwa kiwango cha juu, kumaanisha Mkenya wa kawaida hana uwezo wa kujiwekea hazina au kubakia na noti hiyo kwa muda, hivyo basi kuonesha uchumi unawapeleka kasi.

Uchumi sampuli hiyo ndio huzua hatari ya ukaidi na Rais Uhuru anaonywa kuwa hali hiyo ya uasi ikisukumwa na uchumi mbaya, huhitaji mbinu kali za kisisasa na kiuchumi kuuzima, hali ambayo katika mpangilio wa siasa za upinzani, itakuwa ngumu kuafikia.

Tayari, Kinara wa Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga ameonya kuwa serikali ya Jubilee imo mbioni kuwafukarisha Wakenya ikisaka pesa za mikopo ili wazifisadi.

“Ukitaka kuwajumuisha Wananachi wote katika mrengo mmoja wa ukaidi kwa serikali yao, hata iwe iko mamlakani kwa hali mwafaka ya kidemokrasia, wafukarishe kwanza. Ukishafanya hivyo, njaa inayotokana na umasikini itawatia hisia kali za uasi na hata uwe wewe ni ‘mtu wao kikabila’, watakukaidi kwa dhati,” aambiwa na mhathiri wa somo la Kiuchumi, Festus Wangwe.

Rais Kenyatta anaonywa kuwa kwa sasa ako katika njia panda ya kuafikia umaarufu wa awamu zake mbili mamlakani na ambapo ameweka wazi kuwa analenga kuimarisha sekta ya viwanda, afya, uzalishaji chakula na kilimo.

Bw Wangwe anamuonya rais kuwa hali ya sasa ambapo serikali yake inakopa tu kukopa ili kufadhili miradi ya kuafikia malengo hayo sio suluhu kwa taifa ambalo limeorodheshwa kiuchumi kama “taifa limbukeni.”

Anasema kuwa sera ya kukopa ili kufadhili miradi isiyo na uwezo wa kuzoa mapato ni hatari na ambayo itaishia kufanya maisha ya Wakenya kuwa magumu kiasi kwamba ukaidi ndio utashamili mashinani.

 

Kila Mkenya anadaiwa Sh120,000

“Serikali ya maana kwa wananchi ni ile inayowapa imani kwa maisha yao ya sasa na ya mbele. Hali ilivyo kwa sasa ni kuwa, mwananchi wa kawaida katika taifa hili ako na deni la Sh120, 000 kwa sasa na ni deni ambalo litadumu kwa miaka 30 ijayo.

Ikiwa kwa miaka ijayo serikali itaongeza deni hilo na kipindi cha kulipia mikopo hiyo kirefuke zaidi, ina maana kuwa Wakenya wamekuwa watumwa wa kutafuta riziki walipie madeni wala sio wajijenge,” asema Wangwe.

Licha ya kuwa rais Kenyatta ametetea mikopo hiyo kwa msingi kuwa “Kenya iko na uwezo wa kulipa na ambapo hadi sasa hakujazuka hali ya kuonyesha hali ya hatari, bado anaonywa kuwa huo ni msimamo sawa na “utabiri wa hali ya anga.”

Anaambiwa kuwa uwezo wa kulipa madeni huenda sambamba na uwezo wa riziki ya faida.

“Ikiwa Wakenya wanazidi kuzama katika hali za majanga ambapo kwa sasa wanapambana na ukosefu wa mvua na ambao unazua kiangazi cha njaa kwa binadamu na mifugo; uko na uhakika gani kuwa hali hizo hazitakula hata hizo pesa umekopa ukipambana nazo na hatimaye urejee kukopa tena na ujipate bado umekwama?” auliza Wangwe.

Mshauri wa masuala ya Kifedha katika shirika la NewTimes, Wanjumbi Mwangi anasema kuwa taifa kukopa halina tofauti na mtu binafsi ambaye amekopa.

 

Ni vigumu kustawi

“Wakati wewe umekopa pesa na umezama katika hali ya kutafuta pesa za kulipa mkopo huo, kwa uhakika huwezi ukastawi.

Serikali haina uwezo wa kushiriki biashara ya faida kwa kuwa kazi yake kuu ni kutoa huduma na kuratibu rasilimali za nchi ili ziwe katika uwekezaji na ndipo faida ipatikane kutoka kwa biashara za wananchi na hatimaye serikali iwatoze ushuru,” asema.

Kinyume na hali hiyo, Bw Mwangi anasema, Kenya inakopa ili kufadhili miradi ambayo muda wake wa kuafikia matokeo ni mrefu na hapo katikati bado kuna changamoto zinazochipuka za kuhatarisha uthabiti wa uchumi.

Anasema kuwa kwa sasa kiwango cha mikopo ni 50:54 kumaanisha pato la Kenya kwa mwaka limelemewa kwa asilimia nne na deni.

“Hilo lina maana kuwa serikali imewasukuma Wakenya hadi kiwango cha kula akiba yao na katika maisha yao wameshinikizwa kukopa asilimia nne juu ya kiwango chao cha pato la kila mwaka na ambapo wamehukumiwa kulipa deni hilo wapende wasipende,” asema Bw Mwangi.

Kiwango cha mkopo ambacho kimependekezewa na Benki ya Ulimwengu (IMF) kuwa salama kwa taifa kama Kenya ni asilimia 12.7 ya pato lake la kitaifa, kumaanisha Kenya imevuka mstari hatari kwa asilimia zaidi ya 50 juu ya kiwango hicho salama.

 

Hakuna uhakika 

Tayari, Bw Benjamin ambaye ni msimamizi wa kitengo cha utafiti wa sera za kiuchumi katika Shirika la hazina ya Kifedha Duniani (IMF) ameonya kuwa hatari kuu ya hali ya mikopo ya Kenya ni kuwa hakuna uhakika kuwa pato la kitaifa likiondolewa gharama za kila siku litakuwa na uthabiti wa kulipia mikopo hiyo.

“Hali ni kwamba, taifa linakopa likitarajia kuwa uchumi wake utaimarika. Desturi ni kwamba, uchumi wa Kenya hujikokota katika kupanuka ambapo mwaka wa 2007 ulikuwa katika kiwango cha asilimia 7.0 lakini baada ya changamoto kuukumba, ukaporomoka na miaka 11 baadaye uko katika kiwango cha asilimia 5.2,” asema.

Katika hali hiyo, Carton anaonya kuwa athari kama kiangazi na ukosefu wa ajira, hali ambayo hudunisha Rais Kenyatta alirithi urais mwaka wa 2013 kutoka kwa Mzee Mweai Kibaki kiwango hicho cha deni kikiwa asilimia 38.20 dhidi ya pato la kitaifa, kumaanisha alipata akiba ya asilimia 11.80 ya pato.

Lakini mwaka wa 2014 kiwango hicho kilipanda hadi asilimia 52 huku kwa sasa likiwa limepanda hadi asilimia 54 na kisha kutazamiwa kuongezeka hadi asilimia 59 mwishoni mwa 2019.