JAMVI: Wimbi la ‘minjiminji’ layeyuka kama mvuke huku wakazi wakimkosoa Waiguru
Na WANDERI KAMAU
Kwa ufupi:
- Baadhi ya changamoto zinazomwandama Bi Waiguru zinatokana na tofauti zake na viongozi wengi wa eneo hilo ambao, awali, walikuwa washirika wake wakuu.
- Upungufu ya uongozi wa Bi Waiguru ni kutopatikana kwa urahisi, kutoshirikiana na viongozi wengine, kutenga baadhi ya maeneo katika masuala ya maendeleo, kuongeza ada za biashara na magari
- Waendeshaji magari Kerugoya walilalamikia “kupendelewa” kwa baadhi ya kampuni za matatu, kiasi cha mmoja wa wawakilishi wake kuteuliwa Waziri wa Fedha na Bi Waiguru
- Endapo kutakuwa na uchaguzi mpya, kutakuwa na ushindani mkali kati ya Bi Waiguru na Bi Karua, na huenda Bi Waiguru “akasombwa” na ghadhabu za wakazi dhidi ya uongozi wake
UTAWALA wa gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru umo kwenye darubini baada ya wakosoaji wake kudai kuwa anatenga maeneo ambayo hayakumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu uliopita..
Kwa muda wa chini ya miezi miwili, wakazi wa Kerugoya na Ngurubani wameandamana wakidai kupuuzwa na kutoshirikishwa katika maswala ya maendeleo katika kaunti hiyo.
Mbali na hayo, uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba kesi ya kupinga kuchaguliwa kwake iliyowasilishwa na Bi Martha Karua isikizwe tena, imetajwa na wadadisi kama kisiki kwamustakabali wake wa kisiasa.
Na ingawa Bi Waiguru amewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Mahakama ya Juu, wadadisi wanasema kibarua kigumu kwake, ni ikiwa patakuwepo na marudio ya uchaguzi wa ugavana.
Kulingana na Wahome Kiruma, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za ukanda wa Mlima Kenya, baadhi ya changamoto zinazomwandama Bi Waiguru zinatokana na tofauti zake na viongozi wengi wa eneo hilo ambao, awali, walikuwa washirika wake wakuu.
“Kibarua kinachomkabili gavana (Waiguru) ni kikubwa, ikiwa mahakama itaamua kuwe na uchaguzi mpya. Hii ni kwa sababu wakazi na viongozi wengi wamepoteza imani na uongozi wake, ikilinganishwa na matumaini waliyokuwa nayo kabla ya Agosti 2017,” asema Bw Kiruma.
Kwenye matokeo ya ugavana, Bi Waiguru alishinda kura 161, 343 huku mpinzani wake wa karibu Bi Karua, akizoa kura 122,091.
Hata hivyo, wachanganuzi wamekuwa wakitaja matokeo hayo kuwa kinyume na tafiti zilizotolewa na mashirika mbalimbali kuonyesha Bi Waiguru alikuwa kifua mbele kwa mbali.
Kwa mfano, siku kadhaa kabla ya uchaguzi huo, shirika la TIFA lilionyesha Bi Waiguru akiongoza kwa asilimia 55 ya kura dhidi ya Bi Karua, ambaye angepata asilimia 35 pekee.
Hata hivyo, hali ilikuwa kinyume, kwani Bi Karua alipata asilimia 42 ya kura kwenye uchaguzi huo, naye Bi Waiguru akazoa asilimia 54.
Si rahisi kumpata Waiguru
Kulingana na wakazi, baadhi ya mapungufu ya uongozi wa Bi Waiguru ni kutopatikana kwa urahisi, kutoshirikiana na viongozi wengine, kutenga baadhi ya maeneo katika masuala ya maendeleo, kuongeza ada za biashara na magari kati ya mengine.
Kwenye maandamano ya Ngurubani wiki iliyopita, waendeshaji wa magari aina ya Probox waliandamana wakilalamikia hatua ya kiongozi huyo kuongeza ada zao hadi Sh450, kinyume na ada za sasa ambapo huwa wanalipa wastani wa Sh200 kila siku.
Katika maandamano ya Kerugoya majuzi, baadhi ya waendeshaji magari walilalamikia “kupendelewa” kwa baadhi ya kampuni za matatu, kiasi cha mmoja wa wawakilishi wake kuteuliwa Waziri wa Fedha katika serikali yake.
Kwa hayo, wachanganuzi wanaeleza kuwa mojawapo ya sababu zinazowakasirisha uongozi wake ni kutokana na matumaini makubwa waliyokuwa nayo kwake, hasa baada ya kuraiwa kumpigia kura na Rais Uhuru Kenyatta.
“Wakazi wametamaushwa sana na uongozi wa Bi Waiguru, ikizingatiwa kwamba walipewa msukumo mkuu kumchagua na kampeni kali alizofanyiwa na Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto. Hivyo, ghadhabu yao huenda ikaashiria kutofurahishwa kwao na uongozi wa Serikali Kuu,” asema Bw Linford Mwangi, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.
Kutowajali wakazi
Aidha, anasema kwamba, katika hali ambapo kutakuwa na uchaguzi, huenda mojawapo ya sababu kuu zikawasukuma watu kutomuunga mkono ni dhana ya kutoshughulikia matakwa yao, licha ya kuungwa mkono na serikali ya kitaifa.
Tangu kuchaguliwa kuwa gavana, Bi Waiguru ametofautiana na viongozi wengi, akiwemo mwandani wake wa muda mrefu Bi Wangui Ngirichi, mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo.
Baadhi ya wabunge na madiwani pia wameeleza kutoshirikishwa vilivyo naye, kwenye uongozi wa kaunti hiyo.
Kwa wakati mmoja, mbunge wa Mwea, Kabinga Thayu, alimkosoa vikali Bi Waiguru hadharani kwa madai ya kulitenga eneo hilo, licha ya kuwa na idadi kubwa zaidi ya wapigakura.
“Ni masikitiko kwamba tumepewa waziri mmoja pekee, licha ya eneo hili kuwa na zaidi ya wapigakura 200,000. Hiki ni kinaya kikubwa, ikizingatiwa kwamba gavana mwenyewe anatoka katika eneo hili,” akalalama Bw Thayu.
Waiguru hatarini
Endapo kutakuwa na uchaguzi mpya, wachanganuzi wanatabiri ushindani mkali kati ya Bi Waiguru na Karua, huku wengine wakisema kwamba huenda Bi Waiguru “akasombwa” na ghadhabu za wakazi dhidi ya uongozi wake.
“Kuna uwezekano wa Bi Karua kupata uungwaji mkono zaidi ya ilivyokuwa Agosti 2017, kwani baadhi ya wakazi wanaonekana kujutia uamuzi wao,” asema wakili Mwangi Tharau, ambaye ni mkazi wa Mwea.
Licha ya malalamishi hayo, watetezi wa Bi Waiguru wanapuuzilia mbali mengi ya madai hayo, wakiyataja kama njama za mahasimu wake wa kisiasa.
“Bi Waiguru anapigwa vita kutokana na maono yake makubwa katika kustawisha eneo hilo. Haya ni mawimbi tunayoamini yatapita tu,” asema Naibu Gavana Peter Ndambiri.