Jamvi La SiasaMakala

Junet: Baba alikuwa akinipigia simu thenashara

Na SAMMY WAWERU October 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa wachache Bunge la Kitaifa, Junet Mohamed ameelezea jinsi alivyokuwa na uhusiano wa karibu na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga anayezikwa leo, Jumapili, Oktoba 19, 2025 nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya.

Kulingana na Bw Junet ambaye pia ni mbunge wa Suna East, wawili hao walikuwa marafiki wa dhati kiasi kwamba Raila alikuwa akimpigia simu mapema asubuhi.

“Alikuwa mhandisi wa kazi na kisiasa, na angenipigia simu thenashara (saa kumi na mbili asubuhi). Angenipigia saa nne asubuhi, ilikuwa salamu tu,” Junet aliambia waombolezaji, katika hafla ya maziko iliyoongozwa na Rais William Ruto.

Akimuomboleza Odinga, Mbunge huyo wa ODM, alisema kuwa hakudhania alikuwa yatima pekee kisiasa aliyehuzunika kuachwa na Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/makala/jamvi-la-siasa/siasa-za-ubabe-odm/

Bw Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu chini ya utawala wa Rais Mwai Kibaki, hayati kwa sasa, kati ya 2008 na 2013.

Sawa na viongozi wengine wanachama wa ODM, Junet alisimulia jinsi Odinga alimlea kisiasa.

“Nilidhania ni mimi pekee nimesalia yatima kisiasa kama inavyotajwa mitandaoni, ila naona tuko wengi.”

Waziri wa Fedha, John Mbadi akimuomboleza Bw Odinga, alikumbuka jinsi kiongozi huyo wa ODM alivyompalilia kuingia ulingo wa siasa tangia akiwa chuo kikuu.

Bw Mbadi, ambaye ni kati ya mawaziri waliojiunga na Baraza la Mawaziri wa Serikali ya Ruto 2024 – baada ya Odinga na Rais kutangaza kuzika tofauti zao kisiasa, alisema, “Baba (akimaanisha Odinga) alikuwa akinitembelea chuoni kwenye chumba nilichokuwa nikilala, tangia 1992.”

Bw Raila Odinga atapewa heshima za kijeshi ambapo mizinga itafyatuliwa.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, pia amehudhuria maziko hayo. Itakumbukwa kuwa kati ya 2017 na 2022, Bw Kenyatta na Odinga walifanya salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki, ambapo Rais huyo wa Nne wa Jamhuri ya Kenya alimuunga mkono Raila kuwania urais 2022.