Karata noma ya siasa iliyofanya Kindiki kumpiga kumbo Gachagua
HATA kabla hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua kukamilika katika Seneti mnamo Alhamisi usiku, wandani wa Rais William Ruto katika Ikulu walikuwa tayari wamewasilisha majina sita ya watu waliowaziwa kuchukua nafasi hiyo kwa mashirika mbalimbali vya Serikali yanayohusika na kutoa vibali kwa wanaoteuliwa na kuajiriwa katika ngazi za juu za utumishi wa umma.
Kando na Waziri wa Masuala ya Ndani Kithure Kindiki, ambaye hatimaye aliteuliwa Ijumaa asubuhi na kuidhinishwa haraka na Bunge la Kitaifa kama Naibu Rais Mteule, Taifa Jumapili imebaini kuwa majina mengine yaliyowasilishwa ni ya Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa, na Magavana wa Kaunti Cecily Mbarire (Embu), Ann Waiguru (Kiirinyaga) na Irungu Kangata (Murang’a).
Majibu kutoka kwa mashirika hayo yalitakiwa kufanywa haraka.
Hiyo inaeleza kasi ambayo Dkt Ruto aliweza kuwasilisha jina la Prof Kindiki katika Bunge la Kitaifa Ijumaa asubuhi, saa chache baada ya Bw Gachagua kutimuliwa usiku wa manane, akiambatisha na vibali hitajika kutoka kwa Mamlaka ya Ushuru ya Kenya, Idara ya Uchunguzi wa Jinai,Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu, Afisi ya Taifa ya Usajili na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Barua hiyo kwa Bunge pia iliambatishwa na nakala zilizoidhinishwa za picha ya pasipoti ya Prof Kindiki, kitambulisho cha taifa, cheti cha kuzaliwa, vyeti vya shahada pamoja na wasifu kazi wake.
Kulingana na vyanzo vingi, mashirika yote yaliyohusika na kutoa vibali yalifahamishwa mwendo wa saa nne na nusu Alhamisi usiku, maseneta walipokuwa wakipiga kura kumuondoa mamlakani Bw Gachagua ambaye alikosa kuhudhuria akisema aliugua ghafla.
Mashirika hayo yaliagizwa kutuma wafanyakazi katika ofisi zao kwa ajili ya ukaguzi wa haraka.
Katika hali ya kawaida, ni wanaoteuliwa au wanaoomba kazi ambao huwasiliana moja kwa moja na mashirika hayo ili kupata kibali, ambacho kinaweza kuchukua siku au hata wiki.
Taifa Jumapili imeelezwa kuwa wanne kati ya sita waliidhinishwa na mengi ya mashirika hayo, huku wawili kati yao wakinyimwa vibali kutokana na uchunguzi unaoendelea.
Hata hivyo, inaonekana pia kuwa kutuma majina sita ilikuwa ni sehemu tu ya kamari ya siasa ya kufumba macho, kwa kuwa Rais Ruto tayari alikuwa ameamua Prof Kindiki ndiye chaguo lake la Naibu Rais.
Mchakato huu ulianza baada ya Dkt Ruto na washirika wake kufanya uamuzi wa mwisho wa kumuondoa Bw Gachagua.
Wiki ya pili ya Septemba, idadi kubwa ya viongozi waliochaguliwa kutoka eneo pana la Mlima Kenya walitia saini ‘Azimio la Nyahururu’ la kumuidhinisha Prof Kindiki kama kinara wao wa kisiasa badala ya Bw Gachagua, ambaye alishikilia jukumu hilo kwa kuwa naibu rais.
Hiyo ilikuwa ishara tosha ya aliyependelewa na Rais Ruto, lakini muda mfupi baadaye, majina mengine yalianza kutajwa. Bi Waiguru na Dkt Kang’ata, haswa, pamoja na Bw Ichungwah, walianza kuangaziwa kama waliofikiriwa kuteuliwa Naibu Rais.
Inaonekana kwamba walifahamishwa kimyakimya na wandani wa Ikulu kwamba walikuwa wakizingatiwa, na wakahimizwa kujipigia debe kupitia shughuli mbalimbali.
Hashtagi ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii zikishinikiza Bi Waiguru kwa wadhifa huo.
Picha ya Dkt Kang’ata akiwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambaye amekuwa broka mkuu wa kisiasa tangu aanzishe ukuruba wa kisiasa na Rais Ruto, ilisambazwa na washirika wake.
Pia katika kamari pana ya siasa, kulikuwa na hatua za wazi za kutaja majina ya washirika wa Raila kwa wadhifa huo, huku Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga akiibuka maarufu.
Hatimaye ni Prof Kindiki ambaye aliteuliwa baada ya kamari iliyonuiwa kufaulu kwa mpango wa kumtimua Bw Gachagua.
Kasi ambayo Bw Gachagua aliondolewa na Prof Kindiki kuteuliwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa inaonyesha mipango iliyosukwa kwa umakini.
Changamoto zote zilizotarajiwa na dharura zinazofaa ziliondolewa katika mkakati huo.
Pia, ilikuwa wazi kwamba Dkt Ruto asingechukua hatua kama hizo bila kuwa na imani mpango ungeungwa mkono na idadi inayohitajika wa wabunge na maseneta