Makala

Kashfa za ufisadi hupangwa na wataalamu, ripoti ya EACC yafichua

Na BENSON MATHEKA January 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KASHFA kubwa za ufisadi nchini zinapangwa na kutekelezwa na wataalamu wa sekta mbali mbali, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imefichua.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Dkt David Oginde, alisikitika kuwa wataalamu wamekuwa wakichangia pakubwa katika kufanikisha ufisadi jambo ambalo alisema ni hatari kwa nchi.

“Tumetambua kuwa kashfa nyingi kubwa nchini ni zinazopangwa na kutekelezwa na wataalamu – wasanifu wa majengo, wahandisi, wanasheria, wahasibu, maafisa wa ununuzi, wasimamizi wa wafanyakazi, madaktari miongoni mwa wengine.

Tunataka kuwahimiza waache kutumia utaalamu wao kuwezesha wizi wa fedha za umma. Zaidi ya hayo, mashirika ya kitaaluma yanapaswa kuchukua hatua madhubuti za kutekeleza kanuni zao za maadili ili kukuza maadili mema miongoni mwa wanachama wao,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa EACC aliwahimiza viongozi wa kidini kukemea ufisadi katika mahubiri yao na kutekeleza jukumu lao kama walinzi wa maadili katika jamii.

“Kataeni kunyamazishwa kwa kupokea mapato ya rushwa kama michango ya taasisi za kidini,” alihimiza.Alikosoa viongozi wa kupuuza maadili na kutumia lugha chafu na matusi kwenye mitandao ya kijamii akisema wanatoa mfano mbaya kwa vijana na vizazi vijavyo.

Dkt Oginde alisisitiza kuwa vita dhidi ya ufisadi vinahitaji kujitolea na mchango wa wadau wote vikiwemo vyombo vya habari, serikali na mashirika mengine yasiyo ya serikali, akisema kila mmoja ana jukumu muhimu la kutekeleza iwapo vita vatafanikiwa.

Huku akipongeza vyombo vya habari kwa kufichua kashfa za ufisadi, Dkt Oginde alihimiza bunge kuweka sheria ya kusaidia kuondoa changamoto zinazokumba tume hiyo.

“Bunge linahitaji kuimarisha mifumo iliyopo ya kisheria kushughulikia changamoto zinazozuia hatua madhubuti za kupambana na ufisadi. Katika hili tunaomba Bunge kupitisha Mswada wa Kupambana na Ufisadi (Marekebisho) wa 2025 uliochapishwa na Mwanasheria Mkuu ili kushughulikia mapungufu katika sheria zilizopo,” alisema Dkt Oginde.

Aliutaka umma kutojihusisha na ufisadi na badala yake raia wakatae kutoa hongo.Alilalamika kuwa ufisadi umekuwa ukirithishwa katika familia huku watu wakificha mali wanayopata kupitia njia haramu kwa watu wa karibu wa familia zao.

“Tunatoa wito kwa watu wa familia kukataa kushirikishwa katika mikataba ya ufisadi. Badala yake wazazi wanapaswa kuchukua majukumu yao kujenga maadili katika jamii,” alisema.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Abdi A. Mohamud, alisema kuwa tume iliwasilisha faili 126 za uchunguzi kuhusu kesi za ufisadi, uhalifu wa kiuchumi na utovu wa maadili kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupendekeza kufunguliwa mashtaka kwa watuhumiwa.

“Kwa jumla, tume kwa sasa inafuatilia zaidi ya kesi 400 za kutwaliwa kwa mali iliyopatikana kwa ufisadi ya thamani ya Sh49.5 bilioni,” alisema Bw Abdi.

Dkt Oginde na Bw Abdi walikuwa wakizungumza wakati wa kuzindua ripoti ya hali ya ufisadi nchini Kenya ya mwaka wa 2023-2024 katika makao makuu ya tume jijini Nairobi.