KAULI YA MATUNDURA: Ni muhimu kuitafitia kazi yoyote ya kiubunifu kabla ya kuiandika
Na BITUGI MATUNDURA
Katika makala yangu ‘Uandishi wa kubuni hauhitaji nguvu za uchawi’ (Taifa Leo Juni 23, 2016) niliangazia jinsi mtu yeyote anayejitosa katika ulingo wa kutunga anavyoweza kupata visa vya kuandikia.
Katika makala ya leo, ninaelekeza kurunzi yangu kwenye suala la kufanya utafiti kabla ya kuandika tungo za kubuni. Utafiti huu unaweza kufaidi utunzi wa takriban tanzu zote – hadithi fupi, riwaya, novella, fasihi ya watoto, ushairi na tamthilia.
Hata hivyo, ni muhimu kutaja katika hatua hii kwamba baadhi ya tanzu huhitaji utafiti zaidi kuliko nyingine.
Ikiwa kwa mfano unatunga riwaya ambayo mandhari yake (mahali na wakati) ni mwongo mmoja au karne moja iliyopita, ni muhimu kufanya uandishi wake uwe wa kuaminika na hata kuelimisha.
Watu husoma fasihi mara nyingi kwa minajili ya kujiburudisha na kujifahamisha au kujifunza masuala kadha wa kadha kuhusu maisha.
Watu wengi hudhani kuwa, ili kupata taarifa za kuandikia ni lazima mwandishi asake chemchemi ya tajriba ya maisha yake tu. Hili si kweli. Wanariwaya kama Stef Penney ( Uingereza), ambaye riwaya yake –The Tenderness of Wolves (2006), inasimulia matukio ya Kanada ya miaka ya 1860, ingawa mwandishi mwenyewe hajawahi kwenda nchini Kanada.
Alifanya utafiti wake wote kwenye maktaba jijini London kusaka matukio ya kusimulia katika riwaya hii. Wala Sid Smith (Uingereza) hajawahi kwenda Uchina, ambapo matukio katika riwaya yake ya kwanza, Something Like a House (2001) yanatokea.
Mbali na kwamba fasihi ni sanaa ya ubunifu inayotumia lugha kuwa malighafi yake, ni lazima mambo anayoyazungumzia mwandishi yaakisi uhalisia wa namna fulani.
Kwa mfano, baada ya kusoma novela yangu – Adhabu ya Joka (Longhorn, 2013) mwanangu alinikosoa kwamba joka la mganga lililoibwa na mhusika mkuu – Ziro lilikuwa limefungiwa kwenye sanduku.
Mwivi alidhani kuwa sanduku hilo lililokuwa limefichwa kwenye mvungu wa kitanda cha mganga huyo maarufu lilikuwa na pesa. Joka hilo lilikuwa likipumua vipi? Akaniuliza mwanangu.
Swali hilo lilinishangaza sana kwa sababu katika utunzi wangu, nilikosa kuzingatia uhalisia wa mambo kwamba kila kiumbe aliye hai lazima apumue.
Kwa hivyo, ikiwa mwandishi anaandika hadithi ambayo inahusu mazungumzo baina ya mgonjwa ambaye amekwenda kwa daktari.
Mgonjwa akimweleza tabibu kwamba miguu yake imefura, hatutarajii daktari amuulize mgonjwa huyo: Je, ulienda lini haja kubwa chooni mara ya mwisho?
Ninachoshadidia hapa ni kuwa, mwandishi anayeandikia masuala ya taaluma ya utabibu sharti asome na kutafiti kwa marefu na mapana masuala yanoyohusu tiba.
Hali hii itamwezesha kutunga mambo yanayoafiki uhalisia wa mambo katika taaluma hiyo kwa njia moja au nyingine.
Swali la kwenda msalani analouliza tabibu halihusiani kwa vyovyote na kufura kwa miguu ya mgonjwa tunayemtaja kwenye makala haya.
Mwandishi yeyote anayeandikia mazingira asiyoyafahamu hawezi kuandika kazi ya fasihi inayosadikisha.
Katika kuandika tamthilia ya Kinjeketile inayosawiri mapambano baina ya Watanganyika waliokandamizwa na Wajerumani, Ebrahim Hussein bila shaka alilazimika kusoma kwa kina vita vya Maji Maji (1905 – 1909) ambavyo kwavyo kiunzi cha tamthilia yake kimekitwa.
Hussein anafahamu kwamba kuna muumano na mulandano mkubwa baina ya tamthilia yake (labda kutokana na utafiti alioufanya kabla ya kutunga mchezo huo).
Anatahadharisha wasomaji kwa kusema kuwa historia isitumiwe kuwa kigezo cha kupimia ufanisi wa Sanaa yake – kwani sanaa na historia ni mambo mawili tofauti.
Hata hivyo, sikosei kudai kwamba mpaka baina ya kazi hii ya kisanaa na historia ni mwembamba mno.