Akili MaliMakala

Kijana anavyotumia ubunifu wake wa kipekee kujikimu

Na LABAAN SHABAAN November 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DENNIS Bwire, 27, si mjasiriamali wa kawaida ambaye utamkuta katika kituo cha kibiashara akinadi vitu vya kawaida.

Upekee wake katika ubunifu wa kuunda bidhaa ni siri yake ya kuvutia wateja na kupata mkate wa kila siku.

Wengi wa wanaostaajabia sanaa yake huishia kununua bidhaa kutoka katika karakana yake iliyoko Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Vitu hivyo ni kama vile kifaa cha soketi ya umeme kilichoundwa kwa mbao na radio za kujitengenezea kutumia malighafi za kuokota mitaani.

Umaalum wa kazi yake ni kuunda meza ambayo pia ni radio, sawa na taa zenye spika na radio.

Vifaa hivi vyote huwa na funguo; kwa hivyo ili mtumiaji afurahie, lazima awe na ufunguo.

Tulipokutana naye katika maonyesho ya kibiashara jijini Nairobi, Bwire alikuwa amezingirwa na watu wengi waliokuwa na maswali mengi kuhusu sanaa yake.

“Kazi yangu huwa inashangaza wengi kwa sababu mara nyingi, watu hawatengenezi vitu kama hivi,” alitanguliza huku akikalia meza aliyokuwa akinadi. “Hii ni meza, radio na spika na ni ya bei nafuu.”

Meza yenye spika na radio inayouzwa kwa angalau Sh15,000. Meza hii ilivutia wateja wakati wa maonyesho ya kibiashara katika uwanja wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi mnamo Jumapili Novemba 10, 2024 Picha|Labaan Shabaan

Kwa wiki, Bwire huuza angalau meza moja inayogharimu takriban Sh15,000. Vile vile, Bwire huuza taa inayopiga muziki kwa Sh3000.

“Hizi taa pia zinapendwa sana kwa sababu pia zinafanya kazi ya radio. Umeme ukipotea, zinaweza kuweka moto hadi siku nne,” alieleza huku akifichua kuwa anauza zaidi ya taa tatu kwa juma.

Ni taa za kuchaji ambazo zimevutia biashara ndogo ndogo eneo la Ruiru na wateja wanaoagiza kutumia mitandao ya kijamii.

Bwire anaendelea kuziboresha kwa kuweka paneli za sola ili zihifadhi nguvu kutumia miale ya jua.

Mbunifu huyu ambaye aliacha masomo akiwa shule ya msingi kwa sababu ya ukosefu wa karo, huokota vifaa kutoka kwa mafundi wa vifaa vya kielektroniki, karakana za seremala na kwenye jaa la takataka, hatumii gharama kubwa kutengeneza bidhaa zake.

Vifaa vya soketi ya umeme vinavyotengenezwa kutumia mbao na vitu vilivyotupwa vikiwa katika maonyesho ya kibiashara kwenye uwanja wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi mnamo Jumapili Novemba 10, 2024 Picha|Labaan Shabaan

“Wakati ninapokosa bidhaa hizi kutoka sehemu zangu za kawaida, mimi hulazimika kununua kutoka madukani,” aliungama huku akizipigia debe.

“Kiungo ambacho nimegundua kinawavutia wateja wengi ni kuwa wananunua kitu kimoja kinachofanya kazi zaidi ya moja. Pia, wanapoona wana uwezo wa kufunga taa, soketi na meza kwa kufuli ili kuzuia usumbufu hasaa kutoka kwa watoto, wanavipenda sana.”

Bwire anaambia Akilimali kuwa bidhaa inayonunuliwa sana ni kifaa cha soketi ya umeme ambayo imetengenezwa kwa mbao.

Anaeleza kuwa karakana yake ya Debiwa Technical Works hutumia mbao maalum na kuzipaka mafuta na rangi ili zisipitishe umeme na kusababisha hatari.

“Soketi hizi ni za kudumu nami huziuza kwa kati ya Sh500 na Sh1,500. Wateja wangu wengi huwa makanisa, saluni, kinyozi na biashara nyingine,” alieleza akiongeza kuwa soketi za bei ya juu huwa na funguo.

Bwire anasema kuwa alipata ujuzi huu kwa sababu ya hamu ya kujua jinsi vifaa vya kielektroniki na magari vinafanya kazi.

“Nilikuwa ninaharibu radio, runinga, taa, gari na vitu vingine vya marehemu baba yangu nikitaka kujua jinsi vinafanya kazi,” alikumbuka msingi wa ujuzi wake unaompatia riziki sasa.

Taa inayohifadhi nguvu na pia hutumiwa kama radio ikiwa katika maonyesho ya kibiashara katika uwanja wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Kenyatta (KICC) mnamo Jumapili Novemba 10, 2024. Picha|Labaan Shabaan