Makala

Kwa nini familia zinafaa kuunda maazimio ya mwaka mpya pamoja

Na WINNIE ONYANDO December 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA nyingi huanza mwaka mpya kwa kufanya maazimio ya kibinafsi ikijumuisha elimu, kazi, biashara au afya.

Hata hivyo, maazimio yenye mafanikio huanzia pale familia inapokaa pamoja na kupanga mwelekeo wa pamoja.

Kwa mujibu wa mshauri wa masuala ya kisaikolojia, Loice Noo, mipango ya pamoja huwa ramani inayoongoza jinsi familia inavyohusiana kijamii, kimwili, kiroho, kiuchumi na kihisia.

“Familia inapopanga pamoja, huunda mwelekeo wa pamoja. Malengo ya mtu binafsi huanza kuendana na dira ya familia nzima,” anaeleza.

Anasema familia zinazofanya mikutano ya mara kwa mara na kusikiliza kila mmoja wakiwemo mtoto hujenga mshikamano wa kihisia na uwajibikaji.

Kwa watoto, kushirikishwa kunawafanya wajihisi kuthaminiwa na kuheshimiwa.

“Mtoto anaposhirikishwa maamuzi yanayomuhusu, basi hii huwafanya wajiamini,” anasema Bi Noo.

Hata hivyo, anabainisha kuwa mawasiliano duni bado ni chanzo kikuu cha migogoro ya kifamilia inayowasilishwa kwenye tiba ya kisaikolojia.

Wazazi mara nyingi huchukulia upinzani wa watoto kama ukaidi, ilhali watoto huhisi wamelazimishwa kuishi maamuzi ambayo hawakushirikishwa kuyafanya.

Ili maazimio ya familia yawe na mafanikio, Bi Noo anashauri familia kukagua mwaka uliopita pamoja, kusherehekea mafanikio, hata yale madogo kabla ya kujadili matarajio ya mwaka unaofuata.

Malengo yawe halisi, huku yale makubwa yakigawanywa katika vitengo vidogo vidogo vinavyoweza kutekelezwa.

Katika enzi ya kidijitali, mikutano ya familia ni rahisi zaidi kupanga.

Hata hivyo, Bi Noo anasisitiza kuwa mazungumzo yenye maana yanahitaji uongozi wa makusudi kutoka kwa wazazi au walezi.

“Maamuzi makubwa kama kuhama makazi, kubadilisha shule au mabadiliko ya muundo wa familia hayapaswi kuja kama mshangao,” anaonya, akisema kutoshirikisha watoto huwafanya wajitenge kihisia au kuasi kimyakimya.

Kwa mujibu wake, familia za kisasa pia zinakabiliwa na mabadiliko ya thamani, malezi, kazi na masuala mengine ambayo yanahitaji mjadala wa wazi hasa kwa watoto waliopevuka kiakili.

Kwa familia zinazokumbwa na changamoto, dira ya pamoja inapaswa kutambua udhaifu uliopo na kubainisha jinsi kila mmoja atachangia mafanikio yake.

“Kutafuta ushauri wa wataalamu kama wanasaikolojia, washauri wa kifedha au viongozi wa kidini husaidia maazimio ya familia kuwa shirikishi na endelevu,” anasema.

Pale mikutano ya ana kwa ana inaposhindikana, familia zinahimizwa kutumia majukwaa ya kidijitali kujifunza pamoja kabla ya kufanya maamuzi makubwa ili maazimio yawe ya busara, jumuishi na yenye kudumu.