Tahariri

Vyema EAC na SADC kutafuta amani nchini DR Congo

Na MHARIRI February 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NI jambo la kutia moyo kwamba, hatimaye kuna mwanga kwenye mazungumzo ya kutafuta amani nchini DR Congo.

Kwa muda sasa, mamia ya watu wamepoteza maisha yao huku maelfu wakifurushwa makwao na wengine wakitafuta hifadhi katika mataifa jirani.

Yote haya ni kutokana na mtafaruku wa muda mrefu uliohusisha viongozi wa kisiasa wa DR Congo kwa upande mmoja, na pia waasi, hasa wale wa M23 na mataifa jirani kwa upande mwingine.

Na sasa, baada ya miaka mingi ya makundi tofauti ya wahisani kujaribu kutafuta mwafaka wa amani, hatimaye makundi hayo yote yameungana kwa lengo moja-kutafuta amani katika nchi hiyo ya pili kwa ukubwa na tajiri zaidi kwa rasilmali Afrika.

Katika wiki iliyopita, marais wa Afrika Mashariki chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na wenzao wa jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamekuwa mbioni wakiandaa msururu wa vikao vya kutafuta amani nchini DR Congo.

Na kwa mara ya kwanza, viongozi wa EAC na SADC wamekubaliana kuwa na vikao vya pamoja kinyume na awali ambapo mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika jijini Nairobi chini ya Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta na yale ya Luanda, chini ya Rais wa Angola Joao Lourenco. Mazungumzo hayo sasa yatajulikana kama vikao vya Nairobi/Luanda.

Kama wataalamu walivyowahi kutaja hapo mbeleni, mzozo unaokumba DRC kwa sasa unachochewa na utajiri mkubwa wa raslimali zake ambazo zinamezewa mate na mataifa ya kigeni tangu miaka ya 1960.

Kama tulivyowahi kutaja kwenye safu hizi, mzozo wa DR Congo unaweza kutatuliwa kikamilifu na raia wake. Waje kwenye meza ya mazungumzo wakifahamu kwamba, kuna majirani na wahusika wengine kutoka nchi za mbali ambao wangependa mzozo wa sasa kuendelea kwa muda mrefu ili waendelee kuvuna malighafi nyingi zilizomo nchini humo.

Raia wa DR Congo kwa sasa wametapakaa kote duniani ambapo wengi wanaishi maisha ya uchochole kambini. Wengine wanakita kambi Ufaransa na kwingineko, wakitafuta riziki.

Huu ndio wakati wa kutafakari kuhusu mustakabali wa nchi yao na kuchukua hatua ambazo zitaleta ufanisi kwa taifa hilo ambalo limejaliwa kwa njia nyingi.

Na kwa marais wanaoongoza mchakato mzima wa kutafuta amani, kumbukeni kwamba, ni kwa manufaa yenu kama viongozi wa nchi jirani DR Congo kupata utulivu na amani ya kudumu.

Bila shaka wanafahamu mzigo wanaoubeba nchi inapoporomoka. Tunaamini huo ni mkondo ambao wangependa kuepuka kwa vyovyote vile.