Makala

MAADILI: Babu Owino na Jaguar waomba msamaha kwa kulimana bungeni

November 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino na mwenzake wa Starehe Charles Njagua (Jaguar) Alhamisi waliomba msamaha hadharani mbele ya wenzao bungeni kwa kupigana ndani ya majengo ya bunge mapema mwaka 2018.

Katika kikao kilichoongozwa na Naibu Spika Moses Cheboi wawili hao walishurutishwa kuomba msamaha kutokana na kitendo hicho ambacho kilisemekana kushusha heshima na hadhi ya asasi hiyo.

Hii ni kwa mujibu wa pendekezo kwenye ripoti ya Kamati ya Mamlaka na Hadhi iliyochunguza tukio hilo na kuwasilisha ripoti yake bunge mnamo Jumanne.

Kamati hiyo inayoongozwa na Spika Justin Muturi pia ilibaini kuwa vitendo vya wabunge hao vijana vilikwenda kinyume na hadhi ya bunge na wanaweza kuadhibiwa kwa mujibu wa Sehemu ya 41 ya Sheria ya Uongozi na Maadili na Sehemu ya 17 (3) ya Sheria ya Mamlaka na Hadhi ya Bunge.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka na Hadhi ya Bunge, 2017 Mheshimiwa Paul Ongili Owino na Mheshimiw Charles Kanyi Njagua wanaamuriwa kuomba msamaha kwa bunge na wabunge kwa kushiriki vitendo ambavyo vilishusha hadhi na heshima ya bunge la kitaifa na wanachama wake,” ikasema ripoti hiyo iliyowasilishwa bunge na Mbunge wa Limuru Peter Mwathi.

Akichangia mjadala kuhusu ripoti hiyo kiongozi wa wengi Aden Duale alisema wawili ha walivunja sheria ya mamlaka na hadhi ya bunge kwa kupigana ndani ya majengo ya bunge. “Hatutaruhusi viongozi vijana kulikoseshea heshima bunge hili,” akasema.

“Mkiendelea kudhihirisha tabia mbaya, tutawafurusha kutoka vyama vyetu. Najua mna wafuasi wengi- Njagua ni mwanamuziki mashuhuri lakini Babu Owino anafaa kufahamu kuwa aliacha siasa za chuo kikuu na sasa yeye ni Mbunge,” akasema Bw Duale.

Akichangia mjadala huo, kiongozi wa wachache John Mbadi aliuliza ni kwa nini mwenzake Millie Odhiambo (Suba Kaskazini) alidhulumiwa mnamo bunge 2015 lakini suala hilo halikuwasilishwa mbele ya Kamati ya Mamlaka na Hadhi ya Bunge.

Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini alisema Bi Odhiambo alicharazwa na kuvuliwa nguo na wabunge wa Jubilee fujo zilipozuka bunge wakati wa kujadiliwa kwa Mswada tata wa Marekebisho ya Sheria za Usalama, lakini kisa hicho hakijawahi kuchunguzwa.

“Bunge hilo linapasa kuonekana kama ambayo haipendelei yeyote linaposhughulikia kesi za utovu wa nidhamu, heshima na hadhi miongoni mwa wabunge. Kesi ya dadangu Millie haikushughulikiwa na bunge hili ilhali alishambuliwa n ahata kudhulumiwa kimapenzi na mmoja wetu hapa. Huku tukiwasuta Owino na Njagua, sharti bunge hili pia lishughulikie kesi zingine za dhuluma. Au ni kwa sababu Millie ni mwanamke?” akauliza Bw Mbadi.

Naibu Spika Bw Cheboi alimwonya Mbadi dhidi ya kuelekeza mjadala katika mkondo wa kutetea Bi Odhiambo bali ajikite katika ripoti kuhusu Mbw Owino na Njagua.

Katika mchango wake, Bi Odhiambo aliunga mkono mapendekezo ya ripoti hiyo lakini alilikumbusha bunge kuwa waliodhulumu pia wanafaa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Mbunge aliyedai kumshambulia Bi Odhiambo ni Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria fujo zilipotanda bungeni huku wabunge wa uliokuwa mrengo wa Cord wakipinga mswada huo.

Huku akiwaomba wabunge wenzake msamaha Bw Owino alikana madai kuwa alimzaba kofi Bw Njagua.

Akasema: “Mheshimiwa Spika, sio kweli kwamba nilimzaba kofi Mhe Njagua. Kilichofnyika ni kuwa shavu lake liligusana na mkono wangu”

Hata hivyo, Bw Cheboi alimtaka kuomba msamaha kwa njia ya “heshima” pasina kuingiza mzaha katika suala hilo lenye uzito. Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki hatimaye alisalimu.

Naye Bw Njagua akasema: “Waheshima wenzangu nawaomba msamaha kwa yale yalitendeka siku hiyo. Babu na rafiki yangu na tutaendelea kuheshimiana huku tukishirikiana kuboresha maisha ya wakazi wa Nairobi.”