Makala

Maandamano: Raila akashifu polisi kwa mauaji ya Gen Z

Na SAMMY WAWERU June 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga ameelezea kusikitishwa kwake na visa vya mauaji ya vijana yanayotajwa kutekelezwa na maafisa wa polisi wakati wakikabiliana na waandamanaji mnamo Jumanne, Juni 25, 2024.  

Maandamano yalishuhudiwa maeneo tofauti nchini kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024, na idadi ya watu isiyojulikana wanahofiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Baadhi walikumbana na mauti wakati wakijaribu kuingia Bunge la Kitaifa, eneo ambalo Jumanne lilikuwa chini ya ulinzi mkali Mswada tata wa Fedha ukijadiliwa na kufanyiwa marekebisho.

Bw Raila, kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari alisema ni jambo la kusikitisha kuona serikali inatumia asasi zake za kiusalama “kuangamiza watoto ambao waliandamana kwa amani kutekeleza haki yao Kikatiba”.

Kulingana na Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye miaka ya awali amekuwa akiongoza nchi kushiriki maandamano kushinikiza serikali kuangazia gharama ya juu ya maisha, Wakenya walitarajia serikali ya Kenya Kwanza ingewapa sikio vijana wanaoandamana.

“Ninasikitishwa na ukatili wa polisi kwa vijana waliokuwa wakiandamana kwa amani na kwa mujibu wa sheria… Ninasikitishwa na mauaji, kutiwa nguvuni, kuzuiliwa na msako unaoendeshwa na polisi kwa wavulana na wasichana wetu ambao tu wanataka kusikizwa kuhusu ushuru dhalimu, unaowanyang’anya maisha yao ya leo na ya siku za usoni,” akasema Bw Raila.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM alisema malalamiko ya vijana yangesuluhishwa kwa njia ya amani, ila yaliyoonekana Jumanne hayajawahi kushuhudiwa tangu Kenya ipate uhuru wa kujitawala.

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, ikiwemo Chama cha Wanasheria Nchini (LSK), yamekashifu vikali jinsi polisi wanakabiliana na waandamanaji.

Mswada wa Fedha 2024 ambao Jumanne mchana ulipitishwa na wabunge, sasa ukisubiri kutiwa saini na Rais Ruto kuwa sheria, unahofiwa huenda ukasababisha maisha kuwa magumu kutokana na ushuru wa ziada (VAT) unaopendekezwa kwa baadhi ya bidhaa na huduma.

“Maoni ya vijana yanayotofautiana na serikali, badala yake yamepokelewa na chama tawala kwa dhuluma na mauaji,” Bw Raila akasikitika kwenye taarifa yake.

Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kutetea demokrasia ya nchi, anasema jinsi serikali inakabiliana na maandamano ni dalili ya Katiba na sheria kuwekwa kando.

“Kenya haitamudu kuua watoto wake kwa sababu wanaomba chakula, kazi na skizo”.

Jumatatu, Juni 24, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alikuwa ameonya waandamanaji dhidi ya kuvamia majengo ya kiserikali yanayolindwa.

Prof Kindiki, hata hivyo, alisema kila Mkenya ana haki kuandaaa maandamano ya amani kwa kuzingatia sheria.

Rais Ruto awali alikuwa ameahidi kwamba atafanya mazungumzo na vijana, huku akielezea kuridhishwa kwake na jinsi wamejitokeza kulalamikia masuala yanayowahusu – wasiyofurahia.