Makala

Maeneo haya yatapata mvua ndani ya siku tano zijazo

Na  BENSON MATHEKA May 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUTAKUWA  na mvua kiasi katika maeneo mbalimbali ya nchi  hadi Jumanne ijayo.

Kwa mujibu wa Idara ya Utabiri wa Hewa Kenya mvua inatarajiwa katika maeneo ya Bonde la Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa, maeneo ya chini ya Kusini Mashariki, sehemu za Magharibi mwa Kenya na Ukanda wa Pwani.

Katika utabiri wa hali ya hewa hadi Jumanne Mei 6,  Idara ilieleza kuwa mvua  inatarajiwa asubuhi katika kaunti za Nyanda za Juu Mashariki ambazo ni: Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka-Nithi na Nairobi.

Aidha, kaunti zilizo katika Bonde la Ziwa Victoria na Bonde la Ufa kama Kakamega, Vihiga, Bungoma, Siaya, Busia, Baringo, Nakuru, Trans Nzoia na Uasin Gishu pia zinatarajiwa kupata mvua.

Maeneo mengine yanayotarajiwa kuwa na hali ya hewa sawa ni sehemu za W Pokot Magharibi, Kisii, Nyamira, Kericho, Bomet, Kisumu, Homa Bay, Migori na Narok. Kulingana na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Dkt David Gikungu, maeneo haya yatakuwa na vipindi vya jua asubuhi vikifuatiwa na mvua na ngurumo za radi mchana na usiku.

Kwa upande wa Pwani, kaunti za Mombasa, Kilifi, Lamu, Kwale, pamoja na sehemu za Kaunti ya Tana River, zinatarajiwa kupata mvua kubwa mwishoni mwa juma.

Dkt Gikungu alifafanua kuwa mwezi wa Mei unatarajiwa kuwa kilele cha msimu wa mvua ndefu nchini, na akaonya kuwa huenda kukawa na kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na maji chafu.

Pia aliwaonya wakazi wa Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa wajitayarishe kwa hali ya baridi kali nyakati za usiku, ambapo halijoto inaweza kushuka hadi nyuzi joto 10 kwa kipimo cha selsiasi. Maeneo haya ni pamoja na Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka-Nithi na Nairobi.

Kwa upande mwingine, kaunti za Pwani, Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi pamoja na maeneo ya hapa na pale katika Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, zinatarajiwa kupata joto kali sana mchana, ambapo halijoto itapanda hadi angalau nyuzi joto 30 kwa siku tano zijazo.