Makala

Mafunzo ya wanahabari kuhusu utunzaji mazingira na kuangazia athari za mabadiliko ya tabianchi

Na PAULINE ONGAJI March 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UFUO wa Bahari Hindi kwenye eneo la Afrika Mashariki ni mojawapo ya sehemu maridadi na zilizo na rasilimali nyingi duniani.

Eneo hili linalojumuisha mataifa kama vile Kenya, Tanzania, Msumbiji, Somalia na visiwa vya Ushelisheli na Mauritius, aidha, huhimili mamilioni ya watu.

Kwa mfano uchumi samawati (blue economy) wa eneo hili hutoa rasilimali za samaki kwa mamilioni ya watu, huku takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO) zikionyesha kwamba mwaka wa 2020 zaidi ya tani milioni mbili za samaki zilipatikana hapa.

Nchini Kenya, takwimu zinaonyesha kwamba uzalishaji wa samaki hufikia takriban tani 130,000 kila mwaka na kuhimili maisha ya watu takriban 800,000, ilhali sekta ya baharini nchini Tanzania inachangia asilimia 6 ya jumla ya kipato cha GDP ya taifa hilo, huku zaidi ya asilimia 30 ya watu wakijihusisha na uvuvi wa samaki.

Kando na hayo, mazingira ya baharini yanayojumuisha matumbawe, mikoko na mimea ya baharini ni viumbehai vilivyo katika hatari ya kutoweka na ambavyo ni muhimu sana.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), matumbawe nchini Kenya, Tanzania, na Msumbiji huhimili zaidi ya spishi 1,200 na aina nyingi za wanyama wanaopatikana baharini.

“Mikoko ambayo imechukua takriban hekta 12,000 katika eneo la Afrika Mashariki, hulinda mifumo ya pwani kutokana na mmomonyoko na pia husaidia kufyonza gesi ya dioksidi ya kaboni kutoka hewani,” aeleza Mahfoudh Haji, mwenyekiti wa muungano wa vyama vinavyoangazia mabadiliko ya tabianchi katika kisiwa cha Zanzibar (ZACCA).

Kando na hayo, Bi Sarah Pima, Mkurugenzi wa HUDEFO, shirika la kimazingira nchini Tanzania, anasema kwamba sekta ya utalii katika eneo la Afrika Mashariki hutegemea mifumo hii ya ikolojia.

Bi Sarah Pima, Mkurugenzi wa HUDEFO, shirika la kimazingira nchini Tanzania, akitoa mafunzo ya uchumi samawati na uchumi endelevu kwa wanahabari kutoka eneo la Afrika Mashariki. PICHA|PAULINE ONGAJI

Takwimu za baraza la usafiri na utalii duniani (WTTC) za mwaka wa 2019 zilionyesha kwamba utalii ulichangia asilimia 8.5 ya jumla ya pato la eneo hili (GDP).

Lakini licha ya rasilimali hizi, maeneo haya yamo hatarini.

“Kwa mfano, mabadiliko ya tabianchi tayari yanasababisha uharibifu mkuu ikiwa ni pamoja na ongezeko la vina vya usawa wa bahari, kuongezeka kwa viwango vya asidi baharini na uchubukaji wa matumbawe,” asema Ghaamid Abdulbasat, msimamizi wa mawasiliano kuhusu masuala ya baharini, IUCN Eastern and Southern Africa: The great blue wall initiative.

Aidha, kulingana na wataalamu uchafuzi wa mazingira hasa yanayotokana na matumizi ya plastiki au uharibifu wa mazingira, vile vile uharibifu wa rasilimali za baharini kama vile uvuaji samaki kupindukia unaendelea kuathiri ubora wa maisha ya viumbe baharini.

“Mojawapo ya sababu ambazo zimechangia pakubwa uharibifu huu ni ukosefu wa uelewa miongoni mwa wakazi na wenyeji wa maeneo haya. Sio wengi wanaoelewa umuhimu wa kuhifadhi mazingira na jinsi matendo ya binadamu yanavyoendelea kusabababisha uharibifu huu,” aeleza Bi Pima.

Na ndiposa wataalamu wanasisitiza umuhimu wa wanahabari kama vyombo vya kupitisha habari, na hivyo, umuhimu wa kuwapa mafunzo maalum kuhusu masuala haya.

Kulingana na ripoti ya Jopo la mataifa tofauti kuhusu mabadiliko ya tabianchi (IPCC), vyombo vya habari vina jukumu kuu kuhamasisha umma kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi.

Julien Chambolle, Katibu wa Africa 21, shirika linalohusika na masuala ya maendeleo endelevu, diplomasia na masuala ya Afrika, anasema kwamba mafunzo haya yanawapa wanahabari uwezo wa kuandika na kuchapisha habari kuhusu masuala haya hasa ikizingatiwa kuwa wana uwezo wa kushinikiza maamuzi ya sera, kushawishi maamuzi ya umma na kuwapa wanajamii uwezo wa kubadilisha mienendo yao.

“Ndiposa ni muhimu kuwapa wanahabari hasa wa Afrika uwezo na nguvu za kuweza kutoa taarifa bora kuhusiana na masuala muhimu kama vile uchafuzi wa mazingira na umuhimu wa kulinda bioanuwai ya viumbe, ikiwa ni pamoja na wanyama wanaoishi majini ambao maisha yao yametishiwa.”

Bw Henrique Pacini kutoka shirika la UNCTAD akitoa mafunzo kuhusu masuala ya plastiki katika eneo la Afrika Mashariki kwa wanahabari kutoka nchi za Afrika Mashariki zilizo na ufuo kwenye Bahari ya Hindi. PICHA|PAULINE ONGAJI

Mbinu hii imeonekana kuzaa matunda katika maeneo mengine ulimwenguni.

Utafiti uliochapsiwa kwenye jarida la Journal of Environmental Studies and Sciences linaonyesha jinsi kutoa mafunzo ya mabadiliko ya tabinachi na uchumi samawati kumeimarisha ufahamu wa umma kuhusiana na masuala haya.

“Lakini mafunzo haya ni ghali mno hasa ikizingatiwa kuwa mashirika mengi ya habari sio tu Barani Afrika, bali duniani, yanaendelea kukumbwa na ugumu wa kiuchumi,” aeleza Bi Consuello Natale, Mkuu wa uongozi katika Ubalozi wa Uswizi katika kisiwa cha Zanzibar.

Ndiposa Bi Natale anasisitiza umuhimu wa wafadhili kuingilia kati na kufadhili miradi ya kutoa mafunzo kwa wanahabari.

Aidha, kulingana na Bw Arthur Tuda, Mkurugenzi mtendaji wa muungano wa wanasayansi wa baharini katika kanda ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi (WIOMSA), wafadhili pia wanapaswa kuwekeza katika miradi ya kuwawezesha wanahabari kuwa wataalamu katika sehemu mbalimbali za utangazaji.

“Kutokana na upungufu wa rasilimali, sio rahisi kwa wanahabari kumakinika katika sehemu fulani ya uanahabari na wao wenyewe kuwa wataalamu na sauti ya kuaminika, kwani kufanya hivyo kunahitaji fedha,” aongeza Bw Tuda.

Kulinagan na Kapteni Hamad, Katibu Mkuu katika Wizara ya Uchumi Samawati na masuala ya uvuvi katika kisiwa cha Zanzibar, wanahabari wa Afrika Mashariki wakipewa ufahamu ufaao kuhusu bahari, uchumi samawati na mabadiliko ya tabianchi, wanaweza kuwasiliana na jamii kuhusu mbinu za uhifadhi wa rasilimali zinazopatikana katika eneo hili.