Makundi ya Whatsapp yanavyoimarisha usalama
MAKUNDI ya WhatsApp sasa yanatumika kuimarisha usalama katika Kaunti ya Kiambu, watu wakipiga ripoti kuhusu visa vya uvamizi vinavyosaidia kuwaokoa watu kutoka visa vya uhalifu.
Familia ya Harrisson Muhu mnamo Novemba 29, 2024 ilinusurika kuvamiwa na majambazi baada ya jirani yake kuandika tukio kwenye ukumbi wa WhatsApp ambao unawashirikisha hata maafisa wa usalama.
Bw Muhu na familia yake kutoka kijiji cha Echuka Limuru, walikuwa wakila chajio, kitoweo cha nyama na viazi vitamu huku wakipiga gumzo.
Hata hivyo, furaha hiyo ilidumu kwa muda mfupi waliposkia vishindo kwenye lango lao kuu.
Tafrani zilizuka, watoto wake wakipiga nduru kufahamisha jirani lakini wahalifu hao hawakuonekana kutetereka huku wakiendelea kuvunja lango.
Kwa bahati mzuri majirani waliskia kilio chao na mmoja wao akaandika kwenye ukumbi wa WhatsApp na kuarifu Afisa Msimamizi wa Kituo cha Tigoni Christine Mudanya.
Baada ya muda mfupi Bi Mudanya na kikosi chake waliwasili na wezi hao wakatoroka.
Bw Muhu alisema alipunguziwa wasiwasi Bw Mudanya alipompigia simu kuuliza iwapo kulikuwa na watu kwenye lango lake.
“Nilikuwa kituoni na mara moja nikachukua maafisa wengine kisha tukaingia kwenye gari langu kwa sababu lile la kituo lilikuwa likipiga doria,” akasema.
Japo wahalifu hao walitoroka baada ya kuandamwa, Bw Muhu anasema huenda hali ingekuwa vinginevyo iwapo kuvamiwa kwake hakungeripotiwa katika kundi la WhatsApp.
Makundi ya WhatsApp yanayoshirikisha maafisa wa usalama yameundwa na Kaunti ya Kiambu na yanasaidia kukabiliana na utovu wa usalama.
Kundi la Limuru Highlands lina wanachama 377 huku lile la Tigoni Security Alerts likiwa na wanachama 466.
Wenyeji, maafisa wa usalama, machifu, wazee, manaibu chifu wapo kwenye makundi hayo.
Huwa OCS anatoa nambari ya afisa wa polisi kwenye zamu ili kukiwa na tukio lolote, anapigiwa simu ndipo awajibike na wenzake kidharura.
Kutokana na hili uhalifu umepungua na ukitokea, polisi huwa wanawajibika haraka.
Kamanda wa Polisi wa Kiambu Doris Kemey amesifu ushirikiano huo wa wanajamii na polisi akisema umesaidia kuwarahishisia kazi katika kukabili utovu wowote wa usalama.
Bi Kemey amesema kuwa ushirikiano huo pia umesaidia kuondoa dhana hasi kuwa polisi ni maadui wa raia na badala yake sasa uhusiano huo unaonyesha jinsi ambavyo jamii itakuwa salama polisi na raia wakishirikiana.
“Polisi wakifanya kazi kivyao hawatawezana na wahalifu lakini umma ukiwasaidia, basi wahalifu wenyewe watanyakwa na vitendo vyao kulemazwa,” akasema Bi Kemey.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Muungano wa Wakazi wa Tigoni Elias Ndungú Kariuki alisema kuwa jamii imesaidia katika kuhakikisha usalama wao wakitumia mitandao kuripoti visa vya uhalifu.
Bw Kariuki anasema kuwa sasa wakazi wanaweza kuendelea na shughuli zao kama kawaida hata nyakati za usiku iwapo wamekumbana na wahalifu polisi hupata habari haraka na kutibua majaribio ya wizi au uvamizi.
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga wote wameeleza umuhimu wa jamii kutumia mtandao hasa kumbi za WhatsApp kushirikiana na polisi kupambana na wahalifu.