MAPISHI: Meat pie
Na MARGARET MAINA
JINSI ya kupika meat pie
Muda wa kuandaa: Dakika 40
Muda wa kupika: Dakika 40
Walaji: 3
Vinavyohitajika
– Vikombe 2 unga wa ngano
– ½ kikombe mafuta ya samli au Ghee kwa Kiingereza
– Baking powder kijiko 1
– ½ kikombe pamoja na vijiko 3 vya chakula buttermilk (maji au maziwa)
– ¼ kijiko cha chumvi
– Yai 1
– nusu kilo nyama ya kusaga
– Karoti 2
– Pilipili mboga nusu; iwe ya kijani, manjano au nyekundu
– Kitunguu maji 1
– Vijiko 2 vya kitunguu saumu
– Kijiko 1 cha tangawizi
– ½ kikombe majani ya giligilani
– Vijiko 2 vya chakula mafuta ya kupikia
– Chumvi
Maelekezo
Kwenye bakuli kubwa, changanya unga wa ngano, chumvi, baking powder na samli. Changanya vizuri kwa mkono mpaka uwe kama chenga.
Ongeza nusu kikombe cha buttermilk (maji au maziwa) uanze kukanda. Endelea kuongeza kijiko kimoja kimoja cha buttermilk (maji au maziwa) mpaka unga ushikane vizuri. Kanda hadi ulainike kabisa.
Funika bakuli na kitambaa safi cha jikoni, acha unga utulie kwa dakika kama 10-20 hivi.
Wakati unga unatulia, anza kutengeneza vipande vya nyama vya kujaza sambusa. Katakata kitunguu, karoti na pilipili mboga vipande vya mraba vidogovidogo sana. Twanga kitunguu saumu na tangawizi; katakata majani ya giligilani vipande vidogovidogo sana. Weka kando.
Kwenye kikaangio na katika moto wa wastani, weka nyama, tangawizi na kitunguu saumu. Ongeza chumvi na pilipili kwenye nyama. Kama nyama ni kavu ongeza vijiko viwili vya mafuta, ila kama ina mafuta usiweka mafuta. Pika mpaka nyama iive vizuri, huku ukigeuzageuza kwa robo saa.
Ongeza kitunguu maji na karoti. Pika kwa dakika tatu zingine, huku ukigeuzageuza kisha ongeza pilipili mboga na changanya na majani ya giligilani kabla ya kuepua.
Washa ovena joto la nyuzi 170 digrii za Celsius, au andaa jiko la mkaa kwa ajili ya kuoka. Wakati jiko linapata moto, kanda unga tena, ugawanye kweye madonge madogomadogo ya mduara 20. Weka madonge ya unga kwenye sehemu iliyonyunyiziwa unga, acha yapumzike kwa dakika chache.
Sukuma kila donge utengeneze umbo la mduara kama la chapati; litakuwa dogo kulinganisha na chapati na lisiwe nyembamba sana.
Weka kijiko kimoja na nusu hadi vijiko viwili vya nyama katikati ya mduara uliosukuma. Usijaze sana kwa sababu ukijaza sana itakuwa ni vigumu kufunga. Hakikisha unaacha nafasi ya kufungia.
Inua upande mmoja huku ukihakikisha nyama inabakia katikati. Funika ncha zikutane upande wa pili.
Tumia uma kufunga ncha za meat pie kisha funga vizuri.
Rudia mpaka umalize zote. Panga meat pie kwenye chombo cha kuokea kilichopakwa mafuta au karatasi za kuokea. Piga yai, paka yai lililopigwa juu ya meat pie kwa kutumia brush au kijiko.
Oka kwenye ovena iliyopata moto kwa dakika 20 hadi 25, au mpaka zipate rangi ya kahawia kumaanisha zimeiva vizuri.
Pakua na ufurahie.