Makala

Maswali Rwanda ikimrejesha mshukiwa wa ugaidi ashtakiwe India

Na MOSES K GAHIGI November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Rwanda imemsafirisha hadi India mwanaume ambaye anashukiwa kuwa na uhusiano na vuguvugu la kigaidi.

Mwanaume huyo anashukiwa kutekeleza uhalifu India na kutorokea mafichoni.

Mshukiwa huyo anayetambuliwa kwa jina Salman Khan, alikamatwa Septemba 9 nchini Rwanda baada ya Shirika la Kimataifa la Polisi wa Kukabili Uhalifu (Interpol) kuelekeza mshukiwa atafutwe na kukamatwa mnamo Agosti 2.

Baada ya kutiwa mbaroni, Salman alianikwa mbele ya wanahabari mjini Kigali akiwa amevaa kanzu na kofia ya kiislamu.

Anahusishwa na kundi la ugaidi la Lashkar-i-Taiba ambalo huwapa itikadi kali waumini wachanga wa Kiislamu dhidi ya nchi ya India.

Salman alikamatwa na Idara ya Ujasusi ya Rwanda kisha makachero hao wakatoa taarifa kwa India kupitia Interpol.

Lakini mchakato huu wa kumrejesha Salman ashtakiwe India, uligonga mwamba kwa sababu India na Rwanda hawana makubaliano ya sheria ya kurejesha wahalifu washtakiwe katika mataifa wanamoaminiwa kufanyia uhalifu.

Mkuu wa Mashtaka wa nchi ya Rwanda, Siboyintore Jean Bosco aliambia vyombo vya habari kuwa licha ya kutokuwepo kwa makubaliano haya, walitumia sehemu ya sheria ya nchi kuhusu urejeshaji wahalifu katika mataifa walikofanyia makosa.

“Sheria yetu ina sehemu ya kuwezesha urejeshaji wa wahalifu kwa mataifa ambayo Rwanda haina makubaliano nayo, almuradi wao pia wafanye hivyo kwa mshukiwa tunayemtaka akipatikana nchini mwao. Inaitwa makubaliano ya kurudishiana mkono,” Bw Siboyintore akasema.

“Rwanda si sehemu salama kwa wahalifu ambao wanatekeleza uhalifu katika maeneo mengine. Hakuna nafasi ya kuruhusu uhalifu kabisa. Nchi nyingine zimetufanyia kile ambacho tumefanyia India – tumenufaika na ushirikiano wa kimataifa kuhusiana na masuala ya uhalifu.

Maswali

Lakini kukamatwa na kurejeshwa India kwa Salman kumeibua maswali kuhusu mchakato mzima.

Wakili anayefanya kazi mjini Kigali Louis Gitinywa alisema nchi zinafaa kuwa na makubaliano ya kurejesha wahalifu hata bila ya kuwa na maelekezo ya kukamatwa kwao kutoka kwa Interpol.

Bw Gitinywa alieleza hii inaendana na sheria ya kimataifa.

“Raia huyu wa India angeshtakiwa nchini Rwanda ili jaji atathmini madai dhidi yake kabla ya kurejeshwa,” alisema. “Hatujui hata ni vipi mtu huyu alikuja nchini. Pengine alikuja kama mhamiaji ama mtalii. Alikuwa nchini kisheria? Iwapo alikuwa mtu anayetafuta makao, kuna vipengee vya kisheria vinavyompa ulinzi, la sivyo amekuwa nchini Rwanda kinyume cha sheria.”

Wakili huyu anadai kuwa serikali ya Rwanda iliingia katika mtego wa ‘kuvurugwa na nchi zenye nguvu ili zipate zinachotaka.’

“Kwa kawaida kuna manufaa ya nipe nikupe ya kisiasa na kiuchumi. Huwa tukio la kibiashara, na Rwanda inafaa iwe na maslahi hapo,” wakili aliongeza.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan