Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Utulivu wa nafsi ni matunda ya daraja za imani na kumtambua Mola

August 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla. Swala na salamu anastahiki Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam maswahaba wake watukufu na watangu wema hadi Siku ya Kiyaamah.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Yeye ndiye Aliyeshusha utulivu katika nyoyo za waumini ili waongezeke imani juu ya imani yao.”Al-Fath: 4.

Anasema mmoja wa daktari mashuhuri Marekani, “Nilipokuwa kijana niliweka ratiba ya vitu vizuri vinavyokubalika katika maisha, nikaandika hali nimejawa na matamanio ya kidunia, navyo ni: afya, mapenzi, ujuzi (kipaji), nguvu, utajiri, umashuhuri. Nikampelekea mzee mwenye hekima.

“Akaniambia huyo mzee, ratiba nzuri imepangika vilivyo lakini inaonesha umesahau kipengele muhimu akapiga mstari katika ratiba yote na kuandika maneno mawili ‘Utulivu (wa) Nafsi’.

Akasema hii ni zawadi ambayo Anamhifadhia Allaah Aliyemchagua (katika waja wake) Anawapa wengi akili na afya, mali, ama utulivu wa nafsi , Anatoa kwa kukadiria.

“Akasema: haya nisemayo si mawazo yangu ila nimenakili kutoka kwa wenye hekima wanasema: (Ewe mola acha neema ya dunia chini ya miguu ya wajinga, na unipe moyo usiotetereka (usiotatizika).

“Niliona tabu wakati huo kukubali hayo, lakini sasa baada ya nusu karne nimekiri katika majaribio niliyopitia na mazingatio niliyopata, nimejua utulivu wa nafsi ndio lengo la mwongozo wa maisha yenye kupigiwa mfano, na mimi nimejua sasa jumla ya mambo mengine sio lazima yampatie mtu utulivu, nimeona utulivu huu unachanua bila usaidizi wa mali, wala afya. Katika nguvu za utulivu inabadilisha banda kuwa kasri, ama kunyimwa utulivu inabadilisha kasri la mfalme kuwa kiota.”

Haya ni maneno ya mtu anayeishi Marekani nchi ya starehe na utajiri, nchi ya uhuru kufanya utakacho. Anayasema haya baada kupitia maisha, hakupata katika maisha neema bora na ghali kama utulivu wa nafsi.

Hakuna utulivu bila imani

Utulivu wa nafsi ndio chimbuko la furaha (sa’ada), vipi itafikiwa ikiwa haitokani na akili wala elimu, afya, nguvu, mali, utajiri, umashuhuri, wala neema nyingine ya kimaisha.

Jibu lenye matumaini ni Kumuamini Allaah na siku ya mwisho.

Yametufundisha maisha kwamba watu wengi wenye wasiwasi, kukosa msimamo, hisia za upungufu na kupotea ni walionyimwa neema ya imani na yakini.

Utulivu huu ni matunda ya daraja za Imani na Tawhiyd.

Anashusha Allaah (Subhaanah wa Ta’ala) katika mioyo ya waumini waliopo duniani wawe na msimamo watakapopata matatizo watu, waridhike watakapokasirika watu, wawe na yakini watakapotilia shaka watu, wasubiri watakapotetereka watu, wawe wapole watakapokuwa wajinga.

Utulivu huu ndio uliojaa moyo wa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) siku aliyohama. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“…basi Allaah Alimnusuru walipomtoa wale waliokufuru, alipokuwa (mmoja tu na mwenziwe) wa pili wake, (peke yao) walipokuwa wote wawili katika pango, (Mtume) alipomwambia sahibu yake, usihuzunike kwa yakini Allaah Yu pamoja nasi.” At-Tawbah: 40

Sababu za utulivu kwa muumini

1. Muumin Kuutikia Wito Kimaumbile

Mwanzo wa sababu ya utulivu kwa Muumin ni kwamba ameongozwa katika umbile Alilomuumba nalo Allaah, linaloshikamana na kuwepo kwake na kumuwezesha kuishi kwa amani na upendo sio ugomvi na vita.

Anasema Ibnul Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake Madaarij As-Saalikiyn:

“Katika moyo kuna mtawanyiko (sha’itha) huwezi kukusanya ila kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na kuna ubaya hauondoki ila kujibembeleza kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na kuna huzuni haiondoki ila kufurahika kwa kumjua (Allaah), kuwa mkweli katika matendo.

Na kuna wasiwasi hautotulia ila kwa kukutana Naye na Kuwa kimbilio lako.

Na kuna moto wa majuto hauzimiki ila kwa kuridhia Amri Yake, makatazo, na Qadhwaa Yake, na kuikumbatia subra juu ya hilo mpaka utakapokutana Naye.

Kwa ajili ya kupata utulivu huu ikawa kazi ya Mitume kuamrisha ‘Ibaada ya Allaah na kujiepusha na twaaquut.

2. Muumin Kuongoka Kutokana Na Siri Ya Kuwepo Duniani

Ndani ya kila mwanaadamu kuna sauti iliyojificha inamuita, na maswali yanayompitia kutaka jawabu litakalomuondoshea hofu na kumtuliza nafsi, ni nini ulimwengu? Nani mwanaadamu, amekuja kutoka wapi? Nani kamtengeneza? Nani anamsimamia mambo yake? Nini lengo lake? Vipi ameanza na ataishia vipi? Ni nini maisha na mauti? Ni nini kinamsubiri baada ya maisha haya? Je, inapatikana kitu baada ya maisha haya? Na ni nini uhusiano wake na kudumu (al-khuluud)?

Qur’an imeeleza kwamba hii dini ni ya kimaumbile, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):