Akili MaliMakala

Mchipuko wa mashamba mapya ya kahawa

Na SAMMY WAWERU May 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LICHA ya kiwango cha uzalishaji kahawa nchini kusalia kilivyo kwa muda mrefu, maeneo mapya yamejiunga na mtandao wa ukuzaji.

Kulingana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Nchini (CRI), ni mwaka wa 1987 pekee Kenya ilivuna zaidi ya tani metri (MT) 120,000, mwaka huo mazao yakigonga 127,000MT.

Kimazao, kwa miaka mingi uzalishaji umekuwa kati ya 38, 000MT hadi 52,000MT kwa mwaka.

Hata hivyo, baadhi ya maeneo nchini yameanza kukumbatia kilimo cha kahawa suala ambalo huenda likarejeshea Kenya hadhi ya kiungo hicho cha unywaji kinachofahamika kama ‘dhahabu nyeusi’.

Kahawa iliyovunwa ikigrediwa. Picha|Sammy Waweru

Maeneo hayo ni pamoja na Kaskazini na Kusini mwa Bonde la Ufa, Magharibi mwa Kenya na Pwani.

Mashamba mengi ni yanayolimwa majanichai, miwa na yale ya kijani – yaani green zones kwa lugha ya Kiingereza.

“Kwa upande wa upanuzi wa mashamba, tunaona maeneo mapya yakijiunga na mtandao wa uzalishaji kahawa licha ya baadhi ya maeneo hasa mijini ardhi zikigeuzwa kuwa miradi ya maendeleo,” anasema Dkt Elijah Gichuru, Mkurugenzi Mkuu CRI.

CRI, kwa Kiingereza ni Coffee Research Institute, ni taasisi ya kiserikali ambayo ni mojawapo ya matawi ya Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), inayojukumika kutafiti masuala ya kahawa na kuboresha uzalishaji wa zao hilo.

CRI ina makao yake makuu eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Dkt Elijah Gichuru, Mkurugenzi Mkuu CRI. Picha|Sammy Waweru

Kwa mujibu wa maelezo ya Dkt Gichuru, sehemu kama Narok (mpaka wa Narok na Bomet), Trans Mara, Kisii, Kaskazini mwa Bonde la Ufa, ukanda wa Ziwa – Nyanza, Mlima Elgon, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Baringo, na Laikipia, ni faafu katika ukuzaji kahawa.

Aidha, wakulima wameanza kukumbatia zao hilo.

“Cha kuridhisha zaidi ni kwamba baadhi ya sehemu hizo ni maeneo kame na nusu-kame (ASAL). Uwepo wa teknolojia za kisasa kama vile matumizi ya mifereji kunyunyizia mimea na mashamba maji, utasaidia kuboresha kilimo cha kahawa,” anaelezea Dkt Gichuru.

Maeneo yanayoshuhudia kiangazi na ukame, wakulima hawakumbatii mfumo wa mifereji pekee, ila pia wanatumia bunifu na teknolojia za kisasa kuboresha mazao.

Kahawa iliyopakiwa kabla ya kukaangwa. Picha|Sammy Waweru

Data za New KPCU – chama cha muungano wa ushirika wa kusaga kahawa na kuitafutia soko, zinaonyesha Kericho inachangia asilimia 10 ya kahawa inayozalishwa nchini kwa mwaka.

New KPCU, ni taasisi ya kiserikali ambayo hutafutia wakulima soko la kahawa ndani na nje ya nchi.

“Tukiangalia Nandi, imeandikisha ukuaji wa karibu asilimia 500, Kericho aslimia 265, na Baringo karibu 100. Ukuaji huo ni ishara ya sekta ya kahawa kuboreka, hata ingawa baadhi ya maeneo tunaona wakulima wakigeuza mashamba yao kuwa majengo ya kukodi,” anasema Muhia Murigi, Naibu Mkurugenzi New KPCU, anayehusika na masuala ya utoaji huduma za kitaalamu kwa wakulima.

Mkahawa shambani. Picha|Sammy Waweru

Kenya huuza ng’ambo asilimia 95 ya kahawa inayozalishwa, hii ikiashiria asilimia tano pekee ndiyo hutumika nchini.

Hata hivyo, Murigi anasema asilimia tano hiyo ni ongezeko kutoka asilimia tatu miaka michache iliyopita – hilo likitokana na mikakati iliyowekwa na Serikali kwa ushirikiano na wadauhusika katika sekta kuhamasisha unywaji wa kahawa ndani kwa ndani.

Isitoshe, Mswada wa Kahawa 2023 na Sheria za Kahawa, uliopitishwa mwishoni mwa 2024, umeainisha mikakati kuhamasisha unywaji wa kahawa nchini.

Kulingana na Mamlaka ya Chakula na Kilimo (AFA), eneo la kilimo cha kahawa linakadiriwa kuwa hekta (Ha) 114,000, ongezeko kutoka 109,000Ha miaka michache iliyopita.

Maharagwe ya kahawa yaliyochomwa tayari kusagwa. Picha|Sammy Waweru