• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Mhadhiri mwenye miaka 25 anavyotetea haki za walemavu

Mhadhiri mwenye miaka 25 anavyotetea haki za walemavu

Na DIANA MUTHEU

AKIWA na miaka 25, John Lokuta Ewoi ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa (TUM).

Licha ya ulemavu wake ambapo alizaliwa na mikono mifupi zaidi iliyo na vidole chache, Bw Lokuta amejitahidi kimasomo na kikazi ili aweze kupatana na viwango vya maisha ya kisasa katika jamii.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, Lokuta anasema kuwa mara yake ya kwanza kuingia darasani kufunza, wanafunzi walidhani alikuwa mwanafunzi mwenzao.

“Niliingia darasani na kusimama karibu na ukuta upande wa dirisha. Wanafunzi wote walipoingia darasani, nilisimama mbele na kujitambulisha kama mwalimu wao. Wengi walishangaa, lakini kadri tulipoendelea kukutana na kufunzana, waliweza kuniheshimu kama mhadhiri wao,” akasema huku akiongeza kuwa kiranja wa darasa alimsaidia kumtayarishia kompyuta yake, haswa kuitoa mfukoni na kuiweka ipate moto wa stima, na pia kuandika baadhi ya mambo muhimu ubaoni.

“Kwa mara ya kwanza mtu anaweza kunidharau kwa kuwa nina ulemavu. Lakini nikijitambulisha kwao na kusema nafanya kazi gani, huwa wanamakinika kuniskiliza,” akasema Lokuta.

Hata hivyo, Lokuta alisema kuwa safari yake katika maisha haikuwa rahisi, ikizingatiwa kuwa alizaliwa katika jamii ambayo waliamini kuwa, mama akijifungua mtoto mwenye ulemavu, ni dhahiri kuwa familia yake ilikuwa imelaaniwa.

Kijana huyu ni mzaliwa wa eneo la Baragoi, kaunti ya Samburu na ni mtoto wa nne miongoni mwa watoto nane. Yeye pekee ndiye alizaliwa na ulemavu.

“Nikiwa katika shule ya msingi, nilijihisi kuwa mtu tofauti sana, na wakati mwingi niliamua kujitenga na watoto wengine, sikucheza nao na hata sikuwa na marafiki,” alisema Lokuta.

Lokuta alihudhuria shule ya msingi ya Baragoi na mwaka wa 2009 alifanya mtihani wa kitaifa wa shule ya msingi (KCPE) na akafuzu kwa alama 351.

Licha ya ulemavu wake, alijiunga na shule ya malazi ya Maralal ambapo alisoma pamoja na wanafunzi wengine ambao hawakuwa na ulemavu wowote.

Shule hiyo ilikuwa umbali wa kilomita 105 kutoka nyumbani kwao.

“Maisha katika shule ya upili haikuwa rahisi vile. Nilipokuwa katika shule ya msingi, wazazi wangu walinifulia sare zangu, wakanipigia viatu vyangu rangi na mambo mengine ya msingi niliyohitajika kufanya. Katika shule hiyo ya bweni, wakati mwingine nililazimika kuvalia sare chafu kwa kuwa hakuna yeyote aliyenisaidia upande wa kudumisha usafi,” akasema huku akigusia baadhi ya mambo aliyoweza kujifanyia mwenyewe ni kuandika na kula.

Hata hivyo, anasema maisha yake yalibadilika alipopata marafiki.

“Walinisaidia sana. Walinifulia na kuyafanya maisha yangu rahisi pale shuleni. Mwaka wa 2013 nilifanya mtihani wa kitaifa wa shule za upili (KCSE) na nilifuzu na alama ya B+,” akasema.

Mwaka wa 2014, alijiunga na chuo kikuu cha TUM ambapo alifanya kozi kuhusu maswala ya biashara (BA), na mwaka wa 2018 alipata digrii ya kiwango cha juu zaidi (first class honours).

Chuo hicho kiliweza kugharamikia masomo yake ya shahada, ambayo anaendeleza kwa sasa na pia kumpa kazi ya uhadhiri wa masomo ya biashara.

Wakati huu ambapo shule zilikuwa zimefungwa kwa sababu ya janga la corona, amekuwa akiendeleza masomo yake mtandaoni, na pia kuwafunza wanafunzi wake kwa mtindo huo huo wa kidijitali.

“Nilipojiunga na chuo kikuu, nilijumuika na watu wengi na nikaweza kutambua kuwa pia kulikuwa na watu wengine wenye matatizo mengi kuniliko. Mazingira ya pale yalinibadili kabisa na wanafunzi wenzangu walinikubali jinsi nilivyo, na hapo nilijikubali kabisa na kujipenda zaidi,” akasema Lokuta.

Zaidi alisema kuwa aliweza kuwa jasiri sana, akajitosa katika siasa za chuo na kuchaguliwa kama Kiongozi aliyetetea maslahi ya wanafunzi wenye ulemavu.

Pia, aliweza kushiriki katika shughuli zingine za ziada chuoni na pia michezo, haswa kandanda.

“Napenda mchezo wa kandanda na kwa kawaida nambari yangu ni 10. Watu hudhani nitaumia nikiwa uwanjani lakini kipenga kinapopulizwa na nipate mpira, nitawapiga wachezaji wenzangu chenga na hata kufunga mabao kwa kutumia ujuzi wangu ambao nimekuwa nao tangu utotoni. Nikianguka, huwa naamka bila matatizo yeyote,” akasema Lokuta huku akiongeza kuwa aliweza kuunganisha vijana katika kijiji chao na wakaunda timu moja kwa jina Saint Martin FC ambayo anasema imeweza kushiriki katika mashindano kadhaa na kushinda.

Lokuta anasema kuwa unyanyapaa ndio jambo ambalo huwadhalilisha watu wenye ulemavu.

“Kuna wakati nilienda katika ofisi ya Kiongozi mmoja wa kaunti. Nikiwa mlangoni nikisubiri, nilimwona mzee mmoja amesimama. Nilipomkaribia kumuuliza kama anajua ofisi ya Kiongozi huyo, hata kabla ya kumuuliza alinijibu ‘sina kitu bro’. Nilishangaa sana kwa kuwa alidhani nilitaka kumwomba pesa,” akasema.

Bw Lokuta anasema kuwa familia yake imekuwa ikimsaidia sana na pia kanisa la Kikatoliki la parokia ya Baragoi limempa matumaini katika maisha.

“Licha ya changamoto mingi, namshukuru Mungu kwa kunipa familia inayonijali na kanisa ambalo lilisimama na mimi kwa kila jambo. Kwanza, kanisa hilo lilinisaidia kulipa sehemu ya karo ya shule ya upili na pia likanipa kazi ya ualimu katika moja ya shule ya misheni ili nipate fedha za kujikimu nikijiunga na chuo kikuu,” akasema.

Kwa upande mwingine, Lokuta anasema kuwa ana mpenzi na ana matumaini kuwa mambo yakiwa mazuri anaweza kufunga ndoa naye.

“Mara nyingi maswala ya uchumba huwa na changamoto zake, lakini tunajaribu vivo hivyo,” akasema.

Pia, alisema kuwa ana maono ya kujitosa katika siasa na hata kugombea nafasi kadhaa za uongozi baadaye.

Kijana huyu anasema kuwa walemavu bado hawajaweza kujumuishwa katika sekta zote nchini, ipasavyo.

Amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za walemavu na alipokuwa anafanya mafunzo yake katika baraza kuu la watu wenye ulemavu nchini (NCPWD) baada ya kuhitimu, aliweza kuandika makala mengi akiwasilisha kilio cha walemavu.

Anasema kuwa miradi mingi huwa inatekelezwa bila kuzingatia haki za walemavu.

“Shule nyingi za ghorofa hazina eneo la watu walemavu kutembelea haswa wale ambao hutumia viti vya magurudumu. Pia, vyoo vingi vya umma havijajengwa kumfaidi mlemavu, barabara zetu pia na magari ya umma hayakumzingatia mlemavu,” akasema Lokuta huku akiongeza kuwa miradi kama vile Kazi Mtaani vimetengewa vijana wenye uwezo pekee.

Ombi lake kwa watu watu wenye ulemavu ni wajihami na masomo na ujuzi katika sekta mbalimbali.

“Walemavu wote wajikakamue, ili kunapotokea nafasi zozote za ajira, waweze kutengewa nafasi hizo. Si kwa kuwa wanahurumiwa, lakini kwa kuwa wana uwezo wa kufanya kazi hizo,” akasema.

You can share this post!

Wakufunzi wapya wa Kabras RFC kutua nchini Jumamosi

Vihiga United waingiwa na hofu wanapojiandaa kwa mchujo