Mnaota, Raila na ODM ni chanda na pete, wachambuzi wasema
KUOTA au kufikiria kuwa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga anaweza kustaafu siasa za Kenya hata akipata uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) ni sawa na kufuru ya kisiasa kwa wafuasi wake wa dhati, wachambuzi wa siasa wanasema.
Hii ni licha ya waziri mkuu huyo wa zamani kuashiria kuwa atabanduka siasa za humu nchini kuzingatia wadhifa wa bara.
“Kuanzia sasa sitajihusisha zaidi na siasa za Kenya kwani nitalenga zaidi kampeni katika mataifa yote barani Afrika.
Hii ni awamu ya mpito kutoka kuzamia siasa za Kenya na kuingia katika siasa za bara la Afrika,” Bw Odinga aliwaambia wanahabari katika afisi ya Bw Musalia Mudavadi mwezi jana.
Kauli yake ilijiri wiki chache baada ya wanasiasa wa ODM wakiongozwa na mwenyekiti Gladys Wanga na kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohammed kusema kwamba Raila angali kiongozi wa muungano wa Azimio na kulaumu vinara wenza akiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa kupanga kumng’oa uongozini.
Na wiki hii, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alikanusha ripoti kwamba Bw Odinga anapanga kustaafu kama kiongozi wa chama hicho wadhifa ambao amekuwa akishikilia kwa miaka 17.
Kulingana na Bw Sifuna, Bw Odinga hajawahi kutangazia nchi kwamba atang’atuka kutoka uongozi wa ODM anapowania wadhifa wa bara.
“Mara kadhaa, Mheshimiwa Raila Odinga amekuwa akiarifu nchi kwamba atagombea wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika katika uchaguzi utakaofanyika Februari 2025. Kufikia sasa, Bw Odinga au ODM hawajatangaza kuondoka au kustaafu kutoka uongozi wa chama,” Bw Sifuna alisema.
Wachambuzi wanasemaje?
Mchambuzi wa siasa Sally Gichuru anasema ni mwiko na kukufuru kwa wafuasi na wanasiasa wa ODM kuwazia na kuamini kuwa Bw Odinga atastaafu sio tu siasa za humu nchini bali pia kuachilia chama hicho.
“Wanasiasa wengi wa ODM wanatumia jina la Bw Odinga kujijenga kisiasa na kwa hivyo kufikiria kuwa ataondoka uongozini ni sawa na kukufuru. Wanajua kwamba wasipotumia jina lake, hawawezi kupata nyadhifa wanazoshikilia au hata kushinda viti vya kisiasa,” asema Bi Gichuru.
Viongozi wengi kutoka ngome za Raila hasa maeneo ya Nyanza, Magharibi, Nairobi na sehemu za Pwani huwa wanatumia jina la kiongozi huyo wa ODM kushinda uchaguzi na baadhi ya wanafunzi wake wa kisiasa.
“Raila ni mlezi wa wanasiasa wengi katika ODM na hawawezi kufikiria kuondoka kwake chamani na katika siasa za Kenya. Ndio sababu hali ni tete katika chama hicho wanasiasa wakisubiri uchaguzi wa AUC. Iwapo atashinda, lazima hali itabadilika kwa njia moja au nyingine na wanaotumia umaarufu wake katika siasa za humu nchini huenda wataachwa mataani,” aeleza Bi Gichuru.
Wasiotaka kusikia au kuota Raila akistaafu siasa katika ODM, ni wale ambao wanamtegemea kisiasa na wanajua akiondoka, nyota zao zitafifia, asema mdadisi wa siasa Gerald Omondi.
Anatoa mfano wa jinsi uchaguzi wa chama mashinani na mchujo wa wagombeaji katika uchaguzi mkuu unavyozua joto wanasiasa wakiwania tiketi.
“Ni wale walio na ukuruba wa karibu na Bw Odinga wanaopata viti na tiketi za kuwania nyadhifa. Katika ngome za Odinga, tiketi ya ODM huwa ni sawa na ushindi wa moja kwa moja uchaguzini. Mtu anayefaidika na umaarufu wa Odinga hawezi kufikiria mwanasaisa huyo mkongwe atastaafu siasa,” Bw asema Omondi.