Makala

Msifanye chochote kuhusu dili ya Adani, kamati ya bunge yaonya Mbadi, KAA


KAMATI ya Bunge imeamuru ukaguzi wa kitaalamu ufanywe kuhusu mkataba kati ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya na kampuni ya India ya Adani Holdings kuhusu pendekezo la uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Haya yanajiri huku Waziri wa Fedha John Mbadi akitoa masharti mangumu ya kifedha kwa kampuni hiyo ya India kuhusiana na msamaha wa ushuru.

Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Uwekezaji wa Umma kwa Masuala ya Biashara na Kawi inayoongozwa na Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing inataka Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufichua jinsi Adani ilikabidhiwa kandarasi hiyo

Katika kikao na wasimamizi wakuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA), wakiongozwa na kaimu Mkurugenzi Mtendaji Henry Ogoye, Bw Pkosing alionya kuwa hakuna shughuli yoyote inayofaa kufanyika hadi ripoti ya ukaguzi iwasilishwe mbele ya kamati hiyo.

 “Ni ushauri wa kamati kwamba usifanye lolote na Adani hadi kamati hii iripoti suala hili Bungeni,” Bw Pkosing alisema.

“Utawajibika kibinafsi. Ni Bunge la Kitaifa lenye mamlaka ya kufanya mambo haya. Tutafanya kazi yetu kama kamati, “aliongeza.

Bw Pkosing anataka ripoti ya ukaguzi  iwasilishwe mbele ya kamati hiyo kufikia mwisho wa Oktoba.

Katika ukaguzi huo, kamati inamtaka mkaguzi kubaini jinsi gharama ya Sh230 bilioni za kuboresha uwanja huo ilivyoafikiwa.

Kamati hiyo pia ilimtaka mkaguzi huyo kuchunguza na kuthibitisha gharama ya ujenzi wa jengo jipya la abiria na njia ya pili ya ndege.

Zaidi ya hayo, wabunge hao pia wanataka ukaguzi wa kisayansi ili kubaini kama PIP ilikuwa mpango bora zaidi wa mradi huo na kama kuna njia mbadala ya kuokoa pesa za walipa kodi.

Kamati hiyo pia iliagiza  ukaguzi wa kisayansi unapaswa pia kueleza kwa uwazi jinsi meneja mpya wa uwanja wa ndege atafanya kazi na shirika la ndege la kitaifa na hatima ya wafanyikazi wa sasa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya.

Huku kamati hiyo ikitaka ukaguzi  ufanyike, Bw Mbadi aliambia kamati kuhusu deni la umma na ubinafsishaji kwamba maombi yoyote ya Adani kutotozwa ushuru yatakaguliwa na lazima yaafikiane na sheria za nchi.

Akiwa mbele ya kamati kuhusu mpango huo, Bw Mbadi alisema kutotozwa ushuru kwa miaka 30 ilivyoomba  kampuni hiyo ya India kutafanyiwa uchambuzi wa gharama na manufaa watakayopata Wakenya kabla ya kukubaliwa.

Bw Mbadi pia aliambia kamati inayoongozwa na Abdi Shurie kwamba kabla ya mkataba huo kutiwa saini,  hatari  ya kukodisha uwanja kwa kipindi chote cha miaka 30 itapitiwa upya.

Zaidi ya hayo, Bw Mbadi alisema asilimia ya mapato ambayo Adani inastahili kukusanya kutoka uwanja wa ndege ndani ya kipindi cha miaka 30 pia imepitiwa upya kutoka asilimia 18 iliyopendekezwa  hadi asilimia 16.

“Hadi sasa tumeshajadiliana na kupunguza asilimia hiyo kutoka asilimia 18 hadi 16. Asilimia 16 tuliyojadiliana ilitokana na viwango vya Benki Kuu ya Kenya,” Bw Mbadi alisema.

Waziri huyo aliwaambia wabunge kwamba mlango bado haujafungwa kwa kampuni yoyote ambayo bado inataka kushiriki uboreshaji wa JKIA kwa vile serikali bado haijatia saini mkataba na Adani.

“Sheria inasema kwamba ikiwa tutapata ofa bora zaidi, tunaweza kuacha Adani, jambo la pekee tunalohitaji kufanya ni kampuni hiyo mpya ifidie Adani kwa gharama yoyote ya kifedha iliyotumika kufikia hatua hii ya mchakato,” Bw Mbadi alisema.

Bw Mbadi aliwaambia wakosoaji ambao wamekuwa wakisema kuwa kuna makampuni mengine yaliyo na mikataba bora zaidi kujitokeza na kuwasilisha pendekezo lao kwa KAA ili likaguliwe.

“Nasikia watu wakisema kuna makampuni mengine mengi ambayo yanaweza kufanya kazi bora zaidi, yako wapi? Ikiwa tunaipenda sana nchi hii, huu ndio wakati mwafaka zaidi kujitokeza wakati suala la Adani liko mahakamani,” Bw Mbadi alisema.

Aliwaambia wabunge hao kuwa serikali ilitumia Pendekezo la Kibinafsi (PIP) kwa sababu nchi iko mahali pabaya kifedha na haiwezi kufadhili mradi huo.