MUAFAKA: Orodha ya Uhuru na Raila yapingwa vikali
Na WAANDISHI WETU
UAMUZI wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga kuteua jopokazi la watu 14 kuwashauri kuhusu jinsi ya kuleta umoja wa kitaifa, umekosolewa kwa “kukosa uwakilishi unaostahili.
Viongozi mbalimbali jana walisema jopo lililotangazwa Jumapili halina wawakilishi wa vijana, dini tofauti na pande nyingine muhimu za kisiasa.
Kwa hivyo, wanaamini kuwa hilo ni kundi la kutaka kutekeleza maslahi ya wawili hao pekee, wala si ya taifa zima kama ilivyotarajiwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu wa Kenya (CIPK) tawi la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, Sheikh Abubakar Bini, alisema ingawa awali Rais Kenyatta na Bw Odinga walionyesha nia njema kwa kushirikiana, hatua ya kuacha makundi mengine nje kwenye jopokazi hilo haifai.
“Jinsi ilivyo kwa sasa, kikundi hicho hakina sura ya Kenya katika uwakilishi wa kidini kwani Wakristo pekee ndio wanaowakilishwa. Je, hii itaunganisha Wakenya au kuwagawanya?” akasaili kwenye kikao cha wanahabari mjini Eldoret.
Wazee wa jamii za Bonde la Ufa pia walipinga jopo hilo na kusema halitasiaidia taifa. Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bw Gilbert Kabage, walishangaa kwa nini Naibu Rais William Ruto anatengwa katika mashauriano hayo.
“Hatufurahishwi na jinsi Bw Ruto anavyotengwa katika hatua hizi. Sisi tunamfuata Bw Ruto na tumeghadhabishwa na mambo hayo,” akasema akiwa Nakuru.
Wakizungumza bungeni, Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw Cleophas Malala, na Mbunge wa Butere, Bw Tindi Mwale, ambao ni wanachama wa ANC, walisema vijana walitengwa.
“Inavunja moyo kwamba viongozi hao wawili wa heshima hawakuona sababu ya kujumuisha vijana katika kikundi cha kuleta umoja. Ingawa ninaunga mkono walivyojitolea kuleta upatanisho, ninatoa wito kwao wazingatie kujumuisha vijana,” akasema Bw Malala.
Hata hivyo, chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Odinga kilitetea hatua hiyo na kusema wale waliochaguliwa ni mchanganyiko wa wazee wa kijamii, wasomi, viongozi wa dini na wataalamu wenye misimamo thabiti.
“Kikundi hicho ni kizuri. Hakina watu wenye maazimio ya kibinafsi, kwa hivyo hakitasababisha migawanyiko na kitajitolea kuimarisha uwiano kikiungwa mkono,” akasema Mbunge huyo wa Suba Kusini.
Malalamishi pia yalienea kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutoka kwa vijana ambao walishangaa kama kazi yao katika masuala ya uongozi huishia katika kampeni za uchaguzi na upigaji kura.
Miongoni mwa waliochaguliwa ni Seneta wa Busia, Bw Amos Wako, mwenzake wa Garissa, Bw Yusuf Haji na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Samburu, Bi Maison Leshomo.
Wengine ni Dkt Adams Oloo, Bi Agnes Kavindu, Bi Florence Omose, Prof Saeed Mwanguni, Mzee James Matundura, Meja Mstaafu John Seii, Bw Morompi ole Ronkai na Bi Rose Museu. Viongozi wa kidini waliochaguliwa ni Askofu Lawi Imathiu, Peter Njenga na Zacheus Okoth.