Makala

MWITHIGA WA NGUGI: Wakenya hawajavuna matunda ya ugatuzi miaka sita baadaye

September 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWITHIGA WA NGUGI

NI miaka tisa sasa tangu Wakenya wakumbatie mfumo wa utawala wa ugatuzi baada ya kupitisha Katiba Mpya Mwaka 2010.

Matarajio yao yalikuwa mengi na hasa wakielewa fika kwamba raslimali na uchumi wa nchi ungeweza hatimaye kuwafikia hadi mashinani. Alichotaka kuona Wanjiku ni maendeleo ya kumtoa kwenye pango la umasikini na mazingira ‘takatifu’ ya ufisadi.

Lakini baada ya miaka sita, tunachoona kila siku ni umero wa viongozi wanaotaka kuendelea kunyonya raslimali na uchumi wa Kenya. Wananchi wengi wanalia kwa sababu ya ukosefu ya huduma wanazohitaji. Je, wananchi watapigania haki zao hadi lini?

Kila, Mkenya anataka kuona na kuyahisi maendeleo kutokana na jasho, na hususan kutoka kwa ushuru wa ‘Wanjiku’ mlipa ushuru. Hebu niseme hivi, kila Mkenya lazima akumbuke kuwa viongozi wetu wanafaa kukumbushwa kila wakati kwamba, wao ni watumishi wanaofaa kuwasikiliza waajiri wao ambao ni wananchi.

Kwenye katiba yetu, nina kila sababu ya kusema kwamba, mwenye mamlaka na nguvu ni mwananchi na hakuna yeyote yule anafaa kukiuka haki hii.

Kwa miaka sita, tumeona miradi katika kaunti mbalimbali ikianzishwa na kutekelezwa, lakini kwa bahati mbaya, ufisadi mwingi umedhalilisha mipango hii yote huku fedha nyingi za miradi ikiishia kwenye mifuko ya wachache.

Kwetu sisi, wengi tuliamini kwamba ugatuzi ungewafaidi walalahoi kule mashinani, wengi waliamini kwamba wawakilishi wadi wangeweza kuwa siyo tu watetezi katika kaunti, lakini wokozi wao katika kuhakikisha kwamba usawa wa ugavi wa raslimali na maendeleo unawafikia wote hadi vitongojini, lakini wapi?

Siasa za urithi

Kinachonishangaza wa leo, ni kuona viongozi wa taifa wakizipiga siasa za urithi wa urais wa 2022, badala ya kwanza kutimiza miadi yao ya kampeni waliotoa mnamo 2017.

Kuanzia asubuhi hadi usiku, ninachosikia ni siasa za kuwania viti vya kila aina 2022. Ukweli ni kwamba, Kenya ina shida nyingi. Wengi wanalala njaa, watoto wengi hawaendi shule kwa sababu ya ukosefu wa karo na kwa hivyo, kumsikia mwanasiasa yeyote mwenye umero wa kiti cha urais kamwe hafai kusikilizwa.

Kila taifa linalotaka kuwa na maendeleo, bila shaka lazima liweze kupiga kumbo siasa za pesa nane. Ukweli wa mambo ni kuwa, historia hujirudia, na wakati umefika kwa wananchi kufanya maamuzi yao ya kibinafsi pasina shinikizo la wenye nguvu, mamlaka na pesa za kuwarubuni kiakili, kwani huu ndio mwanzo wa kuijenga nchi pasipo kupumbazwa na wanasiasa matapeli.