OBARA: Hali halisi ya kaulimbiu 'Vindu Vichenjanga' katika siasa za Kenya
Na VALENTINE OBARA
KAULIMBIU ya ‘Vindu Vichenjanga’ au ‘Mambo Yabadilika’ ilipovumishwa na Muungano wa NASA wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka uliopita, matarajio ya wengi yalikuwa kwamba mabadiliko yangetokea tu ikiwa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, angefanikiwa kuwa rais.
Hata hivyo, uhalisia wa kaulimbiu hii umeanza kudhihirika mwezi mmoja baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kutangaza kwamba wameamua kushirikiana ili kuendeleza taifa mbele.
Wakati wa uchaguzi wa 2017, inaaminika viongozi wa kisiasa katika eneo la magharibi walipata umaarufu kwa kuonyesha uaminifu wao kwa Bw Odinga. Kwa upande mwingine, gumzo mitaani ni kuwa wale wa eneo la kati walipata umaarufu maeneo yao kwa kumshambulia kwa maneno kigogo huyo wa kisiasa hadharani.
Sasa mambo yamebadilika, kwani Bw Odinga anarushiwa cheche za maneno makali na viongozi kadhaa wa magharibi wakiongozwa na kinara mwenzake wa NASA, Bw Moses Wetang’ula ambaye ni Kiongozi wa Chama cha Ford Kenya.
Kinyume na hayo, wanasiasa wa eneo la kati wanazidi kumiminika afisini mwake kuonyesha wamejitolea kushirikiana naye sawa na jinsi Rais Kenyatta alivyofanya.
Kufikia sasa, Bw Odinga amekutana na Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria, na aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo.
Mkutano wake na Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, uligonga mwamba wiki iliyopita kwani iliripotiwa alikuwa ziarani Tanzania siku ambapo gavana huyo alipanga kwenda kumwalika kwa kongamano la magavana litakalofanyika baadaye mwezi huu.