• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
ONYANGO: Isiwe mabasi ya NYS ni ya kunufaisha watu fulani

ONYANGO: Isiwe mabasi ya NYS ni ya kunufaisha watu fulani

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) kujitosa katika sekta ya usafiri wa umma jijini Nairobi imezua mjadala mkali nchini.

Baadhi ya Wakenya wamesifu hatua hiyo wakisema kuwa mabasi ya NYS yatasaidia wakazi wa Nairobi kwa kutoa huduma za usafiri kwa bei nafuu.

Wanaounga mkono wanasema mabasi hayo yanayotoza nauli ya Sh50 katika barabara zote saba yanapohudumu, yatawarahisishia usafiri wakazi wa Nairobi na kudumisha uungwana katika sekta ya usafiri wa umma ambayo imegubikwa na ujeuri jijini.

Chama cha wahudumu wa matatu jijini Nairobi nacho kimepinga vikali mabasi hayo yanayotoza nauli nafuu kutokana na kigezo kwamba yatawaharibia biashara.

Chama hicho kinadai kuwa kitapata hasara endapo matatu za kibinafsi zitapunguza nauli ya Sh50 sawa na mabasi hayo ya NYS.

Tayari shirika la NYS limeleta mabasi 24 yanayohudumu katika barabara mbalimbali jiji Nairobi. Mabasi mengine 50 zaidi yanatarajiwa kuletwa kufikia mwishoni mwa mwezi huu.

Serikali pia imeanzisha mikakati ya kutenga sehemu itakayotumiwa na mabasi hayo ya NYS katika Barabara ya Thika ili kuyawezesha kwenda kwa mwendokasi bila kukwama kwenye msongamano wa magari, tatizo ambalo limekuwa donda ndugu jijini Nairobi.

 

Mabasi ya mwendo wa kasi
Serikali inalenga kuiga mfumo wa mabasi ya mwendo kasi sawa na wa Dar-es-Saalam, Tanzania ambapo mabasi maalumu yametengewa barabara ya kusafirisha abiria bila kukwama kwenye msongamano wa magari.

Serikali ya Tanzania inakadiria kuwa jumla ya mabasi 140 ya mwendokasi yanabeba jumla ya abiria 160,000 kwa siku.

Japo mpango huo wa kuleta mabasi ya NYS ni hatua inayofaa kupongezwa, umegubikwa na maswali tele.

Kulingana na takwimu, jiji la Nairobi huwa na watu zaidi ya milioni 5 mchana na wanaosalia usiku ni takribani milioni 3. Hiyo inamaanisha kuwa zaidi ya watu milioni 2 wanasafiri kila siku kwenda na kutoka jijini Nairobi.

Mamilioni ya wakazi wa Nairobi pia husafiri kuelekea katika maeneo yao ya kufanyia kazi kila siku.

Mabasi 74 ya NYS yana uwezo wa kubeba chini ya abiria 100,000 kwa siku. Mbona magari yanayobeba idadi ndogo ya abiria yatengewe barabara maalumu?

Barabara ya Thika tayari inakabiliwa na tatizo sugu la msongamano wa magari, kutenga sehemu ya barabara hiyo kutumiwa na mabasi ya NYS kutafanya hata hali kuwa mbovu zaidi.

Shirika la NYS pia limesongwa na sakata si haba kuhusiana na ufisadi. Je, serikali imeweka mikakati ipi kuhakikisha kwamba mapato yanayotokana na mabasi ya NYS hayaishii katika mifuko ya watu binafsi serikalini? Je, mabasi ya NYS ni kitega uchumi cha watu binafsi serikalini?

You can share this post!

TAHARIRI: Maagizo ya korti hayafai kupuuzwa

Sofapaka yamtimua Waliaula baada ya Ssimbwa kujiuzulu

adminleo