Pambo

Jipambe kaka uvutie vipusa

Na BENSON MATHEKA October 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA dunia ya sasa, mtazamo kwamba ni wanawake pekee wanaopaswa kuwa  nadhifu ni jambo umepitwa na wakati.

Wanaume nao wanahitajika kujitunza, kuonekana safi, kunukia vizuri na kuvaa kwa usafi na mpangilio. Hii si tu kwa sababu ya heshima binafsi, bali pia kwa sababu ya mvuto wao kwa wanawake. Mwanamume anayejijali huonekana kuwa na thamani, kujiheshimu na mwenye maono.

Kwa mujibu wa Dkt Ivy Njeri, mshauri wa mahusiano, wanawake huvutiwa na mwanaume anayejielewa, anayejitunza, na anayejua kujiwasilisha mbele ya watu.

“Mvuto wa nje ni mlango wa kwanza kabla ya mwanamke kuingia ndani ya tabia zako. Hii inamaanisha kwamba kabla hata hujazungumza, mwonekano wako tayari husema mengi kukuhusu,” asema Njeri.

Kuonekana nadhifu hakumaanishi kuvaa mavazi ya gharama pekee, bali kuwa msafi, kupiga pasi nguo zako, kunyoa nywele au ndevu kwa mpangilio na kuhakikisha unatoa harufu nzuri.

Betty Owia, mshauri wa mitindo na mahusiano anasema, harufu nzuri ni silaha ya kuvutia vimwana. “Mwanamume anayenukia vizuri hubaki kwenye kumbukumbu ya mwanamke kwa muda mrefu. Harufu yako inaweza kuwa kivutio kikubwa kuliko hata maneno yako,” asema Owia.

Kwa mwanamume, kuwa nadhifu huongeza kujiamini. Unapojihisi kuwa umependeza, hata mazungumzo yako huwa na uhakika zaidi. Hili linaweza kuwa kivutio kikubwa kwa mwanamke, kwani wanawake huvutiwa na mwanaume mwenye kujiamini lakini asiye na majivuno.

Kulingana na Dkt Ben Kiwia, mshauri wa saikolojia ya mahusiano anasema mvuto wa kimapenzi huanzia kwenye akili. “Mwanamke anapotazama mwanaume aliye nadhifu, tayari anahisi usalama na utulivu ambao wanawake hutafuta katika mahusiano,” asema Kiwia.

Zaidi ya mvuto wa kimapenzi, mwanaume nadhifu pia huonyesha kwamba anajali maisha yake, kazi yake, na hata mwenzi atakayekuwa naye. Hii ni alama ya ukomavu na uwajibikaji, sifa ambazo wanawake wengi huthamini sana.

Mara nyingi, wanaume huamini kwamba ni pesa au gari linalovutia mwanamke. Lakini utafiti wa kijamii unaonyesha kwamba wanawake wengi huzingatia usafi, nidhamu ya mwonekano, na mwelekeo wa maisha kabla ya mali. Kuonekana nadhifu ni kigezo cha awali ambacho huamua iwapo mwanamke atachukua hatua ya pili ya kukufahamu zaidi.

Mwanaume anayejali muonekano wake hujiweka katika nafasi nzuri ya kuvutia, kuheshimiwa, na hata kupata fursa zaidi katika kazi au mahusiano.

Dinah Kioko, mtaalamu wa masuala ya mahusiano anasema mwanaume anayejitunza humwambia mwanamke, ‘ninaweza kukutunza pia.’

Kwa hivyo, asema Dinah, weka bidii kwenye usafi wako si kwa ajili ya wanawake pekee, bali kwa heshima yako binafsi na mafanikio yako ya jumla,” asema.