Makala

Presha inapanda makanisa zaidi yakiendelea kuponda serikali ya Ruto

Na CHARLES WASONGA December 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAKANISA yameendelea kuiponda serikali kwa kushindwa kutatua changamoto zinazowasibu Wakenya yakisema inaendelea kutoa kauli za uongo na kutekeleza sera zinazowaumiza raia.

Kwenye taarifa iliyotoa Jumanne, Desemba 3, 2024, Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) lilifananisha hali mbaya ya kiuchumi inayoshuhudiwa nchini na “mgonjwa ambaye yuko katika hali mahututi”.

Katika taarifa hiyo iliyotiwa saini na mwenyekiti wa baraza hilo Kasisi Dkt Elias Otieno Agola na Katibu Mkuu Padri Chris Kinyanjui, baraza hilo la makanisa lilisema changamoto zinazoikabili Kenya zinatokana na mwenendo wa umma.

Kulingana nao, wananchi  husikiza na kuamini kauli za kupotosha zinazotolewa na wanasiasa wanaolenga kusalia katika au kupata mamlaka.

“Hali inashuhudiwa nchini ni zao na mazoea yetu kama Wakenya kusikiza na kuamini kauli zinazotolewa na watu wanaotaka kuingia au kusalia katika siasa na uongozi. Kauli hizo mara nyingi huwa ni za uongo,” taarifa hiyo ikasema.

“Tunawaomba, ndugu na dada, kwamba muwe mkitafuta ukweli. Msiamini tu kile kinachosemwa, lakini chukua hatua na uthibitishe ikiwe yale yanayosemwa ni kweli,” taarifa hiyo ikaongeza.

NCCK pia iliitaka serikali kuu isitishe utelezaji wa Bima mpya ya Afya ya Jamii (SHIF) inayosimamiwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) hadi changamoto inayoikumba itatuliwe.

“Haina haja kwa serikali kuendelea kutekeleza bima ya SHIF ilhali inakumbwa na changomoto nyingi kiasi kwamba baadhi ya wagonjwa wanalazimika kulipa pesa taslimu wakati mitambo inakwama,” baraza likaeleza.

NCCK imeirushia serikali ya Rais Ruto kombora kali siku mbili baada ya kiongozi wa taifa kuhimiza kuwa kusiwe ni mivutano ya kila mara kati ya Kanisa na Serikali.

Akiongea Jumapili, wakati wa ibada maalum iliyoshirikisha viongozi wa makanisa mbalimbali katika eneo la Kimana, eneobunge la Kajiado Kusini, Dkt Ruto alisema kuwa Kenya haitastawi katika mazingira ya mivutano, haswa yanayolenga kuwagawanya wananchi.

“Hakuna mashindano kati ya kanisa na serikali. Ningependa kusisitiza hapa kwamba hakuna haja ya kuwepo kwa mvutano kati ya Kanisa na Serikali kwa sababu sote tunawahudumia raia,” Dkt Ruto akasema.

“Sharti tuungane tufanye kazi pamoja. Kanisa na Serikali sharti zifanye kazi pamoja. Viongozi kutoka jamii zote sharti wafanye kazi pamoja na viongozi kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa sharti pia wafanye kazi kwa manufaa ya taifa. Hatutaki chuki na mashindano yasiyo na maana wala manufaa kwa watu wetu,” Rais Ruto akaongeza.

Katika siku za hivi karibuni viongozi wa makanisa mbalimbali wameikosoa serikali ya Rais Ruto kwa utawala mbaya unaoendekeza ufisadi na vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu kama vile utekaji nyara wa watu wanaosawiriwa kuwa wakosoaji wa serikali.

Viongozi wa Kanisa Katoliki, Kanisa la Kianglikana (ACK), Makanisa ya Kipentekosti na Kievanjelisti pia wameikosoa serikali ya Rais Ruto kwa kuendeleza sera zinazokandamiza raia kutokana na ushuru mwingi.

Rais Ruto na wandani wake pia wamekosolewa kutokana na mtindo wao wa kutoa mamilioni ya fedha kama ‘sadaka’ kanisani, viongozi wa kidini wakishuku kuwa hizo zinapatikana kwa njia ya ufisadi.

Majuma mawili yaliyopita, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nairobi Philip Anyolo aliamuru kurejeshwa kwa Sh2.2 milioni ambazo Rais Ruto alitoa katika Kanisa Katoliki la Soweto Nairobi.