Makala

Rais Ruto akosa nyota kortini maamuzi kadhaa yakizimwa na majaji

Na SAM KIPLAGAT, BENSON MATHEKA July 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

SERIKALI ya Rais William Ruto imepata msururu wa mapigo mahakamani huku majaji wakisitisha amri, mipango ya Utawala wa Kenya Kwanza au kufutilia mbali baadhi ya teuzi serikalini.

Kuanzia kuzima uteuzi wa Mawaziri wasaidizi (CAS) hadi kufuta mpango wake mpya wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC), hadi kuondolewa kwa watu walioteuliwa kushikilia afisi mbalimbali, kesi dhidi ya serikali zimekuwa nyingi.

Orodha ya wanaowasilisha kesi hizo inaonyesha wanatoka matabaka tofauti yakiwemo mashirika ya kijamii kama vile Katiba Institute, Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC), Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) na watu binafsi akiwemo daktari wa upasuaji anayeishi Nakuru Dkt Magare Gikenyi, Seneta wa Busia Okiya Omtatah na wakili Saitabao ole Kanchory.

Kesi ya hivi punde zaidi dhidi ya serikali iliwasilishwa na Katiba Institute kupinga marufuku ya kuandamana katikati ya jiji la Nairobi iliyotangazwa na kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.

Katika uamuzi huo, Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye alisema hakuna afisa wa polisi anayefaa kutekeleza agizo lililotolewa na Bw Kanja mnamo Julai 17 hadi kesi itaposikizwa na kuamuliwa.

Bw Kanja alikuwa amepiga marufuku maandamano yote katikati mwa jiji la Nairobi na viunga vyake ili kuhakikisha usalama wa umma.

Bosi huyo wa polisi alisema wahalifu walijipenyeza katika vikundi vya waandamanaji, na kusababisha hali ya kutatanisha ya tabia ya fujo na uharibifu.

Huko Malindi, Jaji wa Mahakama Kuu Mugure Thande alitoa amri ya muda, kuzuia mashirika ya usalama kutumia maji ya kuwasha na vitoa machozi dhidi ya waandamanaji.

Ingawa polisi kwa kiasi kikubwa wamepuuza maagizo ya mahakama, jaji pia alizima matumizi ya risasi halisi, risasi za mpira au silaha nyingine za kivita au aina yoyote ya vurugu dhidi ya waandamanaji.

Jijini Nairobi, Jaji Francis Gikonyo alifutilia mbali uteuzi wa mwenyekiti wa Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) Anthony Mwaura, kutokana na kwamba alipewa kazi hiyo huku akiwa na kesi ya ufisadi mahakamani.

Jaji Gikonyo ambaye aliahirisha utekelezaji wa uamuzi huo kwa siku 45 ili kumruhusu Bw Mwaura kukata rufaa, alisema uteuzi wa Bw Mwaura na Rais Ruto mnamo Novemba 18, 2022 haukuwa halali.

“Uteuzi huu una dosari za kiutaratibu na ni kinyume cha sheria kwa vile vipengele muhimu kuhusu kikatiba na kisheria ya uadilifu hazikuzingatiwa katika mchakato wa uteuzi,” Jaji alisema.

Rais Ruto alipotaja jopo kazi la rais kushughulikia wafanyakazi wa sekta ya afya, vikundi kadhaa vya watetezi vilienda kortini vikisema alikiuka katiba.

Makundi hayo yakiwemo Tribeless Youth, Siasa Place, Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) na Africa Centre for Open Governance (Africog) yanahoji kuwa jopokazi hilo linatwaa mamlaka ya Baraza la Ushauri la Wafanyakazi wa Afya Kenya, ambalo lilianzishwa chini ya Sheria ya Afya.

Kesi hiyo itasikizwa wiki ijayo.

Katika notisi ya gazeti la serikali mnamo Julai 5, Dkt Ruto aliteua jopo kazi kufanya ukaguzi wa kina wa deni la taifa na kuwasilisha ripoti yake katika muda wa miezi mitatu.

Lakini Jaji Lawrence Mugambi alizima jopo kazi hilo, kusubiri kusikizwa kwa kesi hiyo iliyowasilishwa na Dkt Gikenyi na Bw Eliud Matindi.

Rais wa LSK Faith Odhiambo, ambaye alikuwa ametajwa kama mwanachama wa jopokazi hilo, alikataa uteuzi huo akisema timu iliyochaguliwa itatwaa jukumu la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu.

Kesi hiyo pia itatajwa Julai 23.

Kuna kesi kadhaa katika Mahakama Kuu kupinga Sheria ya Nyumba Nafuu.

Ijapokuwa majaji watatu walikataa kusitisha utozwaji wa ushuru huo, mahakama ilikubali kwamba masuala yaliyoibuliwa katika kesi hizo ni mazito.

Dkt Gikenyi, mmoja wa walalamishi anaitaka mahakama iamue hakukuwa na ushiriki wa kutosha wa umma, kabla ya sheria hiyo kupitishwa.

Mwaka jana, Mahakama Kuu ilisitisha Notisi ya Gazeti la Kenya ya Novemba 6, iliyoongeza ada za stakabadhi muhimu kama vile vitambulisho, pasipoti na beji za wafanyikazi wa serikali, ikisubiri kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa kwa Dkt Gikenyi.

Pengine pigo kubwa kwa serikali kortini kufikia sasa ni mpango wa UHC, ambao ulipata pigo baada ya majaji watatu wa Mahakama Kuu kufutilia mbali sheria zilizotungwa kuchukua nafasi ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF).

Majaji Alfred Mabeya, Robert Limo na Fred Mugambi walitangaza Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) 2023, Sheria ya Afya ya Msingi, 2023 na Sheria ya Afya ya Dijitali, 2023, ambayo ilibadilisha Hazina ya Bima ya Hospitali ya Taifa (NHIF) kuwa batili.

Majaji hao, hata hivyo, walisimamisha uamuzi wao kwa siku 45 ili kuruhusu serikali kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Pigo nyingine aliyopata Dkt Ruto kortini ni kufutiliwa mbali kwa tume ya uchunguzi aliyoanzisha kuchunguza vifo vya Shakahola, Kaunti ya Kilifi mnamo Mei mwaka jana.

Jaji Mugambi alikubaliana na Muungano wa Azimio La Umoja One kwamba Rais Ruto hakuwa na mamlaka ya kutwaa.