RAMADHANI: Mambo yanayoweza kuharibu saumu
Na MOHAMED KHAMIS
TUNAPOINGIA siku ya sita katika ibada ya saum mwezi huu wa Ramadhan, inawezekana kuna baadhi yetu ambao wanajiunga tu na wengine kwenye ibada bila ya kufahamu mambo muhimu ya kuzingattiwa.
Saumu, sawa na ibada nyingine, ina masharti yanayostahili kuzingatiwa, ambapo bila hivyo, ibada ya kufunga huharibika.
1. Kula au kunywa kimakusudi.
Hakuna tafauti ikiwa kitu kile kinaliwa kama mkate au maji, au hakiliwi kama udongo au mafuta ya taa. Pia haijalishi kama unakula au kunywa kwa mdomo kama desturi au kwa pua, au kwa njia ya kudungwa sindano.
Lakini kupenyeza dawa kwa njia ya sindano katika mikono au paja au mahala popote pa kiwiliwili haitadhuru saumu. Mtu aliyefunga akila au kunywa kwa kusahau saum yake haiharibiki.
Hata hivyo, inampasa awache punde tu akigundua kuwa yuko kwenye saum. Kutafuna chakula kwa ajili ya watoto au ndege, na kuonja chakula (kwa wapishi) ambao kwa desturi hakifiki kooni hakuna makosa.
2. Kuingiliwa mtu na utupu
Kufanya tendo la ndoa hufanya wote wawili kuwa hawajafunga, hata kama hawakutoa manii (shahawa). Ikiwa mtu katika hali ya saumu amelala akaota usingizini na akatokwa na manii, saum yake hubaki pale pale. Muhimu ni kuwa itampasa kuoga janaba anapotaka kusali.
3. Kuzamisha kichwa chote katika maji makusudi
Hakuna tofauti ikiwa kiwiliwili kipo ndani au nje ya maji. Ikiwa umepiga mbizi kwa kusahau tu, haitabatilika saumu. Iwapo aliyefunga atataka kuingia kwenye kidimbwi cha maji, itakuwa vyema kama atajiepusha na kupiga mbizi kwa kuingiza kichwa chote ndani ya maji.
Kukaa na janaba hadi alfajiri makusudi hukuoga ni haramu.
Ikiwa mtu amelala kwa dhamiri ya kuoga kabla ya alfajiri na usingizi ukamchukua mpaka asubuhi, saumu yake haibatiliki.
Mambo yavunjao saumu ni mengi tu yafaa tuhudhurie darsa (hotuba) misikitini ili tujifunze mengi. Mwenyezi Mungu atuongoze na atukubalie funga zetu.