Ruto, Gachagua kupimana nguvu kuchagua mkuu wa magavana
NAIBU Rais Rigathi Gachagua anatarajiwa kupima nguvu wa ushirikiano wa Rais William Ruto na Kinara wa Azimio Raila Odinga baada ya kumsukuma mwandani wake awanie kiti cha uenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (COG) mwezi ujao.
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, mshirika mkubwa wa Bw Gachagua sasa atawania wadhifa wa COG mnamo Oktoba 7 dhidi ya Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi wa ODM.
Kiti hicho kitasalia wazi kwa kuwa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru atakuwa akiondoka mamlakani baada ya kumaliza muhula wake wa pili.
Muhula wa kudumu kuwa mwenyekiti wa COG, huwa ni mwaka moja lakini anaweza kuongeza mwingine akichaguliwa kwa mara ya pili.
Wawaniaji wa uenyekiti wa baraza hilo la magavana na viti vingine wana hadi Septemba 30 kuwasilisha stakabadhi zao.
“Notisi inatolewa kwa kuzingatia Kanuni ya COG kuwa kutakuwa na mkutano mnamo Jumatatu Oktoba 7, 2024 saa nne asububi. Mkutano huo utafanyika afisi za COG ghorofa ya 11 kwenye chumba cha Ugatuzi,” ikasema notisi hiyo iliyotiwa saini na Bi Waiguru.
“Agenda ya mkutano huo umeambatanishwa. Pia kuna fomu ambapo wawaniaji wenye nia lazima wajaze na kurejesha Septemba 30,” ikaongeza notisi hiyo ya Septemba 16.
Mkutano huo pia utaafikiana kuhusu eneo ambalo litaandaa Kongamano la Tisa la Ugatuzi mnamo 2025.
Kando na uchaguzi wa COG, Magavana pia watawachagua mwenyekiti wa baraza lao, kiranja kisha mwenyekiti na wanachama wa kamati mbalimbali.
Hata hivyo, mapambano hayo sasa yanaonekana kuchukua mwelekeo wa kupimana nguvu kati ya Bw Gachagua kwa upande moja na muungano wa Raila/Ruto upande mwingine.
Bw Kahiga ni mwandani wa Naibu Rais na amekuwa kati ya viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele kumtetea kutokana na kile ambacho amekuwa akirejelea kama kuhangaishwa na serikali.
Naye Bw Abdullahi alichaguliwa kwa tikiti ya ODM, ni mshirika wa karibu wa Raila Odinga ambaye kwa sasa anashirikiana na utawala wa Kenya Kwanza baada ya wandani wake kuteuliwa serikalini.
Japo nafasi ya mwenyekiti wa COG inafaa kupigiwa kura, magavana kwenye chaguzi za hapo awali wamekuwa wakikukumbatia majadiliano na makubaliano kuhusu viongozi wa kushikilia afisi hizo.
Hasa wamekuwa wakizingatia usawa wa jinsia, wa kieneo na miegemeo ya chama.
Waliowahi kuhudumu kama mwenyekiti wa COG ni Isaac Ruto wa Bomet (2013-2015), Peter Munya wa Meru (2015-2017) na Josephat Nanok wa Turkana 2017-2019.
Wengine ni Wycliffe Oparanya wa Kakamega (2019-2021), Martin Wambora wa Embu (2021-2022) na Bi Waiguru (2022-2024).
Gavana wa zamani wa Kwale Salim Mvurya alichaguliwa kama mwenyekiti wa COG mnamo Disemba 2017 lakini hakumaliza muhula wake wa mwaka moja na Bw Nanok akachukua usukani.
Akigusia kura hiyo, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja mnamo Alhamisi alisema bado kuna muda na huenda wawaniaji wengine wakijitokeza kutaka uenyekiti wa COG.
“Bado kuna muda kwa uteuzi. Makataa ni Septemba 30 kwa hivvo bado ni mapema sana kusema ni wawili hao ndio wamejitokeza,” akasema Bw Sakaja.
Duru zinaarifu kuwa Bw Mutahi ambaye kama Bi Waiguru anatoka ukanda wa Mlima Kenya na alichaguliwa kupitia UDA, huenda akawa naibu wa Bw Abdullahi kuhakikisha kuwa kuna usawa wa kieneo na vyama.
“Hakuna Gavana kutoka Kaskazini mwa Kenya ambaye amewahi kushikilia wadhifa huo na huu ndio wakati muafaka. Pia itakuwa haki kwa UDA kuunga mkono chama kingine,” akasema Gavana mmoja kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Bi Waiguru alichaguliwa kupitia njia ya maelewano mnamo 2022 na ndiyo gavana wa kike kuwahi kushikilia wadhifa huo. Bw Abdullahi naye alichagulia kama naibu wake.
Japo Azimio ina magavana wengi kwenye COG waliafikiana kumchagua Bw Waiguru wakati Joseph Ole Lenku wa Kajiado pia alikuwa akigombea kiti hicho kupitia Azimio.