Makala

Ruto: Pigeni sherehe kwa uangalifu msimu wa Krismasi

Na SAMMY WAWERU December 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amewataka Wakenya kusherehekea Krismasi 2024 kwa uangalifu, akiwataka wawajibike.

Akizungumza Jumatano, Desemba 25 katika Kaunti ya Narok ambapo alihudhuria ibada ya Kanisa, Dkt Ruto alihimiza wananchi kuwa waangalifu wakati wa shamrashamra za Krismasi.

“Krismasi ni wakati wa sherehe, lakini pia tufanye yale tunayofanya kwa uangalifu,” Rais alisema.

Huku msimu huu ukihusishwa na matukio mengi, unywaji wa pombe kiholela ukiwemo kwa waraibu, Rais Ruto aliwataka vijana na wananchi kwa jumla kuwa makini.

Aidha, alitaja matumizi ya dawa za kulevya na mihadarati kama visa ambavyo vijana wanapaswa kujiepusha.

Kiongozi wa nchi vilevile amewataka Wakenya kujali maslahi ya familia zao.

“Tulinde familia zetu,” akasisitiza Rais Ruto.

Kauli ya Rais kuhusu pombe inajiri siku chache baada ya naibu rais aliyebanduliwa, Rigathi Gachagua kudai kuwa serikali ya Ruto imefungua milango ya pombe harmau kuelekezwa Mlima Kenya.

Kulingana na Bw Gachagua, serikali imelegeza kamba vita dhidi ya pombe haramu na hatari eneo la Mlima Kenya likilemewa kwa kero hiyo.

Gachagua alikuwa ametwikwa jukumu la kupambana na unywaji wa pombe, hasa Mlima Kenya na eneo la Bonde la Ufa, ambapo aliendesha oparesheni kali akiwa naibu wa Rais Ruto.

Anadai lengo la serikali baada ya kuondolewa mamlakani ni kuona wenyeji wa Mlima Kenya wanakunywa pombe, ili idadi yao ya wapiga kura ipungue kuelekea uchaguzi mkuu 2027.

Ni matamshi ambayo serikali imeyakashifu vikali, Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndnai, Dkt Raymond Omollo akimtaka Gachagua kuandikisha taarifa na idara za uchunguzi kuhusu tetesi hizo.