Makala

Ruto, Raila wapuuza matakwa ya Gen Z wakiungana serikalini

Na BENSON MATHEKA, WINNIE ONYANDO July 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamepuuza matakwa ya vijana wanaoandamana huku vyama vyao vikionekana kuungana kuunda serikali.

Hii ilidhihirika jana Rais Ruto alipotangaza orodha ya pili ya mawaziri wateule katika Ikulu ya Nairobi.

Licha ya vijana wa Gen Z kupigania haki zao barabarani na mtandaoni, na hatakujeruhiwa na makumi ya watu wakitekwa nyara, kuteswa na kuuawa, Rais na Odinga walionekana kuwapuuza na kuwafurahisha wafuasi na wandani wao.

Kwenye orodha hiyo, Dkt Ruto alikosa kabisa kusikiza malalamishi ya vijana wa Gen Z kwa kuwa walioteuliwa ni walewale waliotimuliwa na wandani wa Bw Odinga.

Vijana wamekuwa wakitaka mawaziri waliofutwa kazi wasirejeshwe kazini, ufisadi ukomeshwe na serikali kupunguza matumizi.

Vijana hao wamekuwa wakitaka sheria ya kuunda Mamlaka ya Afya ya Jamii iondolewe na serikali isitishe ushuru wa nyumba nafuu miongoni mwa maswala mengine ya utawala mbaya.

Hata hivyo, katika hotuba yake jana, kiongozi wa nchi aliwarejesha kazini baadhi ya mawaziri aliofuta kazi kufuatia shinikizo za vijana na kutangaza kuwa serikali yake itaendelea mbele na mpango wake wa afya kwa wote na wa nyumba nafuu.

Baadhi ya mawaziri aliorudisha kazini ni Kipchumba Murkomen ambaye sasa atasimamia wizara ya vijana ambao wamekuwa wakishinikiza asirudishwe katika baraza la mawaziri na Kithure Kindiki ambaye akiidhinishwa na bunge, ataendelea kusimamia Wizara ya Usalama wa Ndani.

Wiki jana, vijana hao walikataa wito wa Rais Ruto wa serikali umoja wa kitaifa ilipobainika kuwa Bw Odinga alikuwa akiongoza chama chake kujiunga na serikali.

Katika taarifa kali Jumanne wiki iliyopita, vijana hao walimshutumu waziri Mkuu huyo wa zamani kwa kujaribu kuteka mapambano yao kuungana na serikali inayowakandamiza.