SHERIA: Naam, mwanamke anaweza kuozea jela kwa kubaka mwanamume
SHERIA ya makosa ya ngono inataja ubakaji kama kupenya kwa makusudi sehemu za siri za mtu mwingine bila idhini yake.
Kwa kuwa anayebaka huwa hana idhini, huwa anatumia nguvu, vitisho au ushawishi wa aina yoyote ile. Ni muhimu kufahamu kuwa, kisheria, ubakaji unahusishwa na kitendo cha kushiriki ngono kwa mtu mzima bila idhini yake.
Adhabu ya ubakaji n kifungo cha miaka kumi jela au zaidi na inaweza kuongezwa hadi kifungo cha maisha.
Japo watu wengi huchukulia ubakaji kama kosa linalofanywa na mwanamume kwa mwanamke, sheria inatambua kuwa mwanamume anaweza kubakwa na mwanamke kwa kumlazimisha kupenya sehemu zake za siri.
Hivyo basi, ni muhimu kuhakikisha kuwa kabla ya kushirikisha mtu wa jinsia yeyote kwa kitendo cha ngono, unapata idhini yake kwa njia faafu. Sawa na kosa la unajisi, mtu anaweza kuhusishwa na jaribio la kujaribu kubaka.
Katika sheria ya makosa ya ngono, jaribio la kubaka linatajwa kama kujaribu kupenya sehemu za siri za mtu mwingine bila idhini yake, kwa kutumia nguvu au vitisho.
Adhabu ya kujaribu kubaka ni kifungo kisichopungua miaka mitano na inaweza kuongezwa hadi kifungo cha maisha.
Mbali na unajisi, kujaribu kunajisi, kubaka na kujaribu kubaka, mtu anaweza pia kuadhibiwa kwa kosa la kushambulia mwingine kingono.
Kulingana na kifungu cha 5 cha sheria ya makosa ya ngono, haya
ni matumizi ya makusudi ya kitu au sehemu yoyote ya mwili wake (isipokuwa sehemu zao za siri) kupenya sehemu za siri za mtu mwingine bila ruhusa.
Adhabu ya kosa la kushambulia mtu kingono ni kifungo jela cha miaka kumi jela na inaweza kuongezwa hadi kifungo cha maisha.
Kosa hili linajumuisha matukio ambapo vidole, vijiti au chupa hutumiwa kupenya viungo vya ngono kwa kutumia nguvu.
Inafaa kufahamika kuwa kitendo chochote cha kupenya sehemu za siri kwa sababu sahihi na za kitaalamu za usafi au matibabu kunakofanywa na daktari wakati wa uchunguzi wa kimatibabu, kwa ruhusa ya wagonjwa, kwa kutumia vifaa vya matibabu au vidole vyake kunakubaliwa kisheria na hakuwezi kuchukuliwa kama shambulizi la kingono.
Ni muhimu kufahamu tofauti ya ubakaji na unajisi inavyofafanuliwa kisheria.
Unajisi unafafanuliwa kuwa kufanya kitendo cha ngono na mtoto kwa kuwa mtoto hawezi kutoa idhini ya kushiriki kitendo cha ngono.