Makala

SIHA NA LISHE: Njia mbalimbali za kupunguza uzani bila kujinyima chakula

January 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

BAADA ya shamrashamra za Krismasi na Mwaka Mpya ni dhahiri kwamba wengi wamefurahia mapochopocho tofauti; na sasa baadhi wanajiuliza ni vipi wanavyoweza kupunguza uzani bila ya kufanya mazoezi na kujinyima vyakula.

Kuna njia rahisi kama unaweza kujizoesha kufanya basi unaweza kupunguza uzani lakini pia kuwa na afya kipindi chote.

Maji mengi

Washauri wengi wa mambo na masuala yanayohusu afya wanashauri kunywa maji lita zaidi ya mbili kwa siku kama mtu angependa kuwa na afya nzuri huku pia akilenga kupunguza uzani.

Unapoyaywa maji mara kwa mara unahisi umeshiba na hata ni hali inayoweza kukufanya kutotaka kula sana.

Chai ya kijani yaani ‘green tea’

Wachina wamekuwa wakizingatia kunywa chai ya kijani kwa miaka mingi.

Wanaiamini na kuithamini kwa sababu ina uwezo wa kusafisha mwili kutokana na sumu yoyote kwa kuwa inaaminika kuwa na anti-oxidant nyingi.

Zaidi ya hayo, kunywa kikombe cha chai ya kijani baada au wakati wa mlo husaidia kuondokana na tamaa ya kunywa vinywaji vingine visivyo na afya kama soda au mvinyo.

Kula chakula cha usiku kabla ya saa mbili usiku

Watu wengi huwa na mazoea ya kulala kuanzia saa tatu mpaka saa nne.

Ukila chakula baada ya saa mbili usiku inamaanisha chakula hakipati muda mzuri wa kumemenyeka kabla hujalala, unashauriwa kula chajio kuanzia saa kumi na mbili na nusu jioni mpaka saa mbili usiku hii hufanya chakula chao kimemenyeke vyema kabla ya kwenda kulala.

Chagua vyakula vya kuoka na supu zaidi kuliko vya kukaanga

Mafuta si mazuri mwilini, kwa kuwa mafuta huganda mwilini.

Kutumia vyombo vidogo

Unapaswa kutumia vyombo vidogo, iwe sahani, bakuli au kikombe. Hii ni kutaka kutokupakua vyakula vingi. Kuna msemo usemao “smaller bowls = smaller portion” lakini pia kama una vyombo vikubwa basi jitahidi kujikadiria chakula cha wastani na sio kutaka kujaza chakula kutokana na ukubwa wa chombo chako.

Matunda na mbogamboga

Kuzoea kula mbogamboga na matunda kunasaidia pia kufanya mwili upungue na uwe na afya nzuri. Unaweza kula mbogamboga kama main dish na kula matunda unapojisikia hamu ya kula kitu kingine baada ya kula chakula kikuu. Hii husaidia kutokula vitu visivyo na afya kama chokoleti na biskuti.