Makala

TAHARIRI: IEBC inahitaji kupigwa darubini upya

December 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

Kwa mara nyingine, Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeonyesha kuwa udhaifu unaoikumba taasisi hiyo muhimu hauwezi kumalizwa kwa urahisi. Hivyo basi, panahitajika njia mwafaka na ya kudumu ya kusuluhisha tatizo hilo la kila mara.

Kwa kujikumbusha tu, udhaifu huu umejitokeza kuanzia siku za aliyekuwa mwenyekiti wa ECK marehemu Samuel Kivuitu, ukarudi tena katika enzi ya Isaak Hassan (2013) na kisha katika utawala wa Wafula Chebukati (2017).

Mbali na madai ya kujiendesha katika njia inayoshukiwa na baadhi ya viongozi kama yenye hila katika uchaguzi, kwa sasa IEBC imekumbwa na mizozo tele yakiwemo madai ya matumizi mabaya ya afisi na ufujaji wa pesa pamoja na ufisadi miongoni mwa maafisa wake katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita.

Udhaifu huu unaibua maswali mengi kuhusu ni vipi tume hii inavyoendelea kuandamwa na mambo ambayo yanawavunja moyo Wakenya wanaoitegemea kupata viongozi wanaostahili?

Aidha, swali kuhusu ufaafu wa maafisa wanaoteuliwa kuwa viongozi wa tume hiyo, linaibuka.

Taifa hili linastahili kuangalia ni vipi litaweza kuboresha utendakazi wa tume hiyo ili kuhakikisha inatimiza matarajio ya Wakenya kwa uwazi bila kuibua tashwishi kama ilivyo kwa sasa.

Je, ni vipi tunavyoweza kuangamiza zimwi linalotawala shughuli za tume ya uchaguzi kila mara?

Huenda jibu limo kwenye marekebisho ya katiba. Ni muhimu, kwa hivyo, Wakenya wanapowazia suala la marekebisho ya katiba, kutilia maanani tume hii na jinsi inavyoundwa.

Inasikitisha kuwa kwa kipindi kirefu tume ya uchaguzi imezingirwa na madai mbalimbali ambayo yanaathiri majukumu yake na kufanya wananchi kukosa imani kwake.

Kadhalika, kwa kukosa uadilifu na uwazi hasa kuhusiana na uchaguzi wa urais, uhasama, ghasia na hata vita huzuka miongoni mwa wananchi na hivyo basi kukwamiza shughuli nyingi zenye umuhimu kwa taifa kama vile uchumi na mshikamano wa kijamii.

Twatumai katika kutimiza kauli ya Rais Uhuru Kenyatta kuwa ipo mikakati itakayohakikisha kuwa ghasia hazizuki tena kutokana na uchaguzi wa urais, suala la muundo wa IEBC lizingatiwe kama mojawapo ya njia nzuri za kutimiza azimio lake hilo.