Makala

TAHARIRI: Jambo lifanywe kuhusu mishahara

April 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

JUMATANO hii ulimwengu unaposherehekea sikukuu ya Lebadei, Kenya kwa inahitaji kujali maslahi ya wafanyakazi wake hasa wakati huu wa gharama ya juu ya maisha pamoja na mfumko wa bei.

Mishahara na ujira wa Wakenya wengi hasa wenye malipo ya chini imekuwa ikidumaa huku mingine ikiongezeka kwa mwendo wa kobe ilhali maisha yanaruka kwa kasi ya swara.

Tusipokuwa waangalifu kama taifa na hasa viongozi wa serikali walio katika nafasi nzuri ya kuunda sera, tutagutuka kama watu wetu wameangamia.

Wazazi wengi kwa sasa hawajui watakakotoa karo ya shule wakati huu wa kufunguliwa kwa shule. Wengine wengi hawana kodi ya nyumba na hata bado wapo wale wasiokuwa na chakula.

Sharti mikakati mipya iwekwe ya kuwaauni Wakenya. Mojawapo wa mikakati faafu kwa wananchi hawa ni kuwapa nyongeza nzuri ya mishahara na kuhakikisha kila mwajiri ametekeleza amri ya kuongeza asilimia inayofaa.

Katibu wa chama cha wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli amependekeza asilimia 15 kama nyongeza ya mwaka huu.

Ametoa pendekezo hilo kama sharti la kuunga mkono Azimio la Makazi Nafuu la Rais Uhuru Kenyatta.

Azimio hilo linapangwa kutekelezwa kwa kuwakata wafanyakazi wote na waajiri wao asilimia moja na nusu ya mshahara wao.

Naam huenda asilimia hiyo ya COTU ni kubwa kwa serikali kumudu lakini ni aula nyongeza ya mwaka huu iwe ya maana wala lengo la nyongeza hiyo lisiwe tu ada ya makazi nafuu bali dhamira iwe kuboresha maisha ya Wakenya.

Mbali na mkakati wa kuongeza mishahara, itakuwa bora serikali ianze kutafuta njia za kuwapunguzia wananchi gharama ya maisha.

Kutokana na kupungua kwa thamani ya mishahara, hatua itakayowakinga Wakenya hasa wa tabaka la chini ni kuwapunguzia gharama ya maisha hususan bei za bidhaa muhimu za kimsingi kama vile unga na mafuta na hata ikiwezekana kuweka viwango vya nauli.

Jambo jingine linalowaumiza Wakenya zaidi ni mzigo wa karo ya shule. Japo serikali iliahidi kuhakikisha kuwa wanafunzi wa sekandari wanaosoma kwa kurejea nyumbani hawatozwi pesa zozote hakuna shule ambayo haiwatozi wanafunzi ada za masomo.

Wazazi wengi, kadhalika, wanatatizika na karo za juu za masomo ya vyuo vya kadri na vyuo vikuu. Sharti jambo lifanyike.