Makala

TAHARIRI: Tusipochunga madeni yatazamisha Kenya

November 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

Kwa mara nyingine tena, ofisi inayoshughulika na bajeti katika bunge (PBO) imeonya kuwa huenda Kenya ikanyimwa mikopo kutokana na deni kubwa iliyokopa na inayoendelea kukopa nchi tajiri za kigeni na mashirika wafadhili.

Kwenye ripoti yake ya hivi punde, ofisi hiyo inaonya kuwa kasi ya madeni ya serikali ya Jubilee, huenda ikatumbukiza Kenya katika hali ambayo haitaweza kukopa pesa kutoka kwa mashirika ya kimataifa.

Bila shaka hii sio mara ya kwanza ofisi hiyo kutoa onyo kama hilo.Hii ni baada ya kukadiria kuwa deni la Kenya huenda likapita kiwango kilichowekwa na bunge cha Sh9 trilioni katika muda wa miaka mitatu ijayo ikiwa serikali haitakomesha utashi wake wa mikopo.

Inasema kwamba deni la Kenya huenda likawa Sh9.2 trilioni katika muda wa miaka mitatu ijayo.Ripoti hiyo inakubaliana na wataalamu wa uchumi ambao wamekuwa wakionya kuwa pesa zinazokopwa na serikali hazitumiwi kikamilifu kwa miradi inayolengwa.

Kwa lugha rahisi, ni kwamba kumekuwa na ubadhirifu wa pesa zinazonuiwa kufadhili miradi tofauti. Hili linadhihirishwa na madai kwamba pesa zilizopatiwa Kenya na wafadhili kukabiliana na janga la corona ziliporwa.

Uchunguzi kuhusu madai hayo unaendelea. Wasiwasi uliopo ni ripoti hiyo kufichua kwamba Kenya italazimika kukopa ili kujaza pengo katika bajeti hasa kufuatia shughuli za uchumi kuvurugwa na janga hilo.Hii ndio hali inayoshuhudiwa na mataifa mengi yaliyo na uchumi dhaifu kote duniani.

Hata hivyo, inafaa serikali itilie maanani ushauri wa ofisi hiyo na kutumia vyema pesa inazokopa na kwa miradi inayokusudiwa. Deni ni mzigo kwa nchi na iwapo Kenya itanyimwa mikopo kwa sababu ya kutumia vibaya ilizokopa, basi raia wa nchi hii watakuwa wakilipa pesa zilizoingia katika mifuko ya watu wachache.

Muhimu ni kuhakikisha wanapolipa deni kupitia ushuru wanaotozwa, wanafurahia matunda ya mikopo hiyo. Kuendelea kukopa bila mipango maalumu ni hatari kwa nchi na hii ndio onyo la wataalamu.

Wanasiasa hawana budi kuzingatia ushauri huu kwa sababu ni wao wanaochangia kwa njia moja au nyingine kuongezeka kwa deni la nchi.

Tusipokuwa waangalifu, na ikizingatiwa kuwa mabadiliko ya kikatiba yanayopendekezwa yataongeza gharama ya kuendesha serikali, tutazama kwa madeni