TAHARIRI: Wauzao bidhaa feki ni wauaji, wanyongwe!
Na MHARIRI
NI jambo la kusikitisha sana kuwa tamaa ya utajiri wa haraka imewafanya baadhi ya Wakenya kuingiwa na ushetani kiasi cha kuweka afya na maisha ya wananchi katika hatari kubwa.
Imeibuka kuwa wakora hawa, baadhi yao wenye vyeo serikalini na wanasiasa, wamekuwa wakishiriki biashara ya bidhaa za magendo, ambazo cha kutia wasiwasi ni kuwa zina sumu hatari kwa wanaotumia bidhaa hizo. Bidhaa hizi ni nyingi na zinatumiwa kila siku na mamilioni ya Wakenya.
Kinachoudhi zaidi ni kuwa waliopewa kazi ya kuhakikisha bidhaa zinazotumika nchini ni salama na zimefikia viwango vilivyowekwa, wameambukizwa ulafi huu, nao pia wameacha kulinda maisha ya Wakenya na badala yake wanahusika katika biashara ya kuwadhuru raia wasio na hatia.
Ni kutokana na ushetani wa wafanyabishara wachache, wanaosaidiwa na wanasiasa waliopotoka na maafisa wa serikali, ambapo magonjwa hatari kama saratani yameongezeka kutokana na vyakula vyenye sumu na dawa mbaya zilizopitwa na wakati.
Mijengo nayo inaendelea kuporomoka na kuua wengi kutokana na matumizi ya vifaa ghushi huku ajali za barabarani zikiongezeka baada ya vipuri feki kumwagwa nchini.
Mbali na madhara ya kiafya, uchumi pia umepata pigo kutokana na biashara hii kwa sababu wauzaji wa bidhaa feki wanaiga zile halali, na hivyo kuharibu soko ya bidhaa zinazotengezwa nchini. Matokeo yake ni kudorora kwa uchumi, uhaba wa ajira na ongezeko la umaskini.
Madhara ya bidhaa hizi ni makubwa hivi kwamba wanaohusika hawapaswi kuonewa huruma hata kidogo.
Kama kweli Serikali inajali maisha ya raia wake, inapasa kuonyesha kwa vitendo kwa kuwakabili wahusika kikamilifu bila huruma wala kujali vyeo vyao.
Hawa ni wauaji ambao adhabu yao inafaa kuwa kifo ama kifungo cha maisha gerezani na mali yao kutwaliwa ili wanaofikiria kufuata mkondo wao wafikirie tena na tena kabla ya kujiingiza katika shughuli hizi hatari.