TEKNOLOJIA: Mitandao ya kijamii inavyotumika kudunisha demokrasia duniani
NA FAUSTINE NGILA
DUNIANI KOTE, mitandao ya kijamii imewapa watu sauti katika maamuzi ya kisiasa na kuwasukuma maafisa wa serikali kuwajibikia matendo yao.
Mwaka 2011, wakati kampuni za Google, Facebook na Twitter zilitumika kwa mapinduzi ya sera za serikali katika mataifa ya uarabuni almaarufu Arab Spring, mitandao ya kijamii ilisifiwa kwa mchango wake katika kukuza demokrasia.
Lakini kufikia mwaka huu mambo mengi yamebadilika na kugeuza maana halisi ya demokrasia. Kwenye uchaguzi wa urais wa Amerika hapo 2016, mitandao hii ilitumiwa kusambaza habari feki na kueneza uhasama wa kisiasa.
Ni dhana hii ya habari feki iliyomsaidia Rais Donald Trump kupata ushindi dhidi ya mpinzani wake Hillary Clinton.
Utambulisho bandia
Na mwaka uliofuata wa 2017, Afisa Mkuu Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg alifichua kuwa taifa la Urusi lilitumia utambulisho bandia na kulipia matangazo yapatao 3,000 yaliyochapishwa kwa Facebook na yaliyompigia debe Bw Trump kabla na baada ya uchaguzi.
Kwa wastani, kati ya watumizi milioni 146 na milioni 150 walipokea taarifa za matangazo hayo yaliyochapishwa na shirika la serikali ya Urusi, pamoja na watumizi milioni 16 wa mtandao wa Instagram, unaomilikiwa na Facebook.
Kampuni ya Facebook imelaumiwa sana katika mchango wake wa kuua demokrasia duniani. Hapa Kenya, kinara wa upinzani Bw Raila Odinga alijitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 akidai kuwa kampuni hiyo ilishirikiana na Cambridge Analytica kueneza habari za chuki dhidi yake mitandaoni kabla ya uchaguzi.
Hivyo, Facebook imechangia kwa ghasia za baada ya uchaguzi kote duniani kwa uzembe wake wa kuchukua hatua kuhusu masuala haya huku ikiwahadaa watumizi wake kuhusu sera za usiri wa taarifa na juhudi za kupuuza wanaoikosoa.
Facebook, Twitter na Google zimekuwa zikichochea uhasama katika jamii. Lakini zinaelezea matatizo haya kama masuala madogo yasiyo na athari.
Wadukuzi wa Urusi na Brexit
Imebainika kuwa wadukuzi wa taifa la Vladimir Putin waliunda machapisho 80,000 yaliyofikia watu 126 milioni nchini Amerika katika kipindi cha miaka miwili.
Uchanganuzi mmoja wa akaunti sita za wadukuzi wa Urusi uling’amua kuwa machapisho yake yalikuwa yamesambazwa mara 340 millioni!
Na hizo zilikuwa kurasa sita tu kati ya kurasa 470 ambazo Facebook ilitambua akama zilizoundwa kwa njia ya hila kutoka ikulu ya Kremlin.
Posti zenye utambulisho feki pia zilitumika kuchochea ghasia za kisiasa nchini Amerika hasa maandamano dhidi ya uhamiaji na mihadhara ya Kiislamu.
Juhudi sawa zilifanyika kuchochea matokeo ya kura ya Uingereza kujitoa katika Muungano wa Ulaya (EU) almaarufu Brexit, hasa kupitia akaunti feki za Twitter.
Na tangu taifa hilo lipitishe kura hiyo, imekuwa changamoto kwao kupata mkataba unaowafaa baada ya kung’atuka kutoka EU kwa kuwa baadhi ya kampeni mitandaoni kuhusu suala hilo ni za watu wanaojifanya raia wa Uingereza wanaoishi katika mataifa ya nje.
Matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Uholanzi, Ujerumani na Ufaransa pia yalivurugwa na machapisho ya akaunti bandia katika mitandao ya kijamii.
Taifa la Canada kwa sasa lina kila sababu la kuwa na hofu kuhusu jinsi mitandao hii itatumika kubadilisha fikra za wapiga kura katika uchaguzi wa 2019.
Wakati Facebook na Twitter ziliambia wabunge wa Congress nchini Amerika kuwa zingeshirikisha umma katika midahalo baina ya viongozi wa vyama vya kisiasa, watu wengi walishangaa ni asilimia ngapi ya maoni yangechangiwa na akaunti feki za Urusi.
Bw Zuckerberg ameahidi “kurejesha imani katika mchakato wa demokrasia.” Aliahidi kuwa atayataka matangazo yote yafichue ukurasa uliolipia uchapishaji wake, na kuhakikisha kila tangazo linaonekana na kila mtu.
Aliahidi kuzima wadukuzi na wamiliki wote wa akaunti feki kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi wanaoshughulikia masuala ya ulinzi wa data.
Hatua butu
Lakini kama unafiki kuwa hatua hizi zitasuluhisha tatizo la kuvurugwa kwa demokrasia, basi umekosea.
Mwanzo, inahitaji watu wengi zaidi kufuatilia matini kubwa za taarifa, picha na video zinazochapishwa kwa mtandao huo wenye watumizi zaidi ya bilioni mbili.
Na hakuna moja kati ya hatua hizi inabadilisha dhana ya kibiashara ya Facebook ambayo ni kuuzia watangazaji muda na nafasi ya kidijitali kwa kutumia uchanganuzi wa data ya watumizi wa mtandao huo.
Hivyo, matangazo ya kisiasa ni sehemu ya kibiashara ya kampuni hiyo, jinsi yanavyotangazwa kwenye runinga. Mwishowe matangazo haya yataongezeka kote duniani.
Nayo kampuni ya Google imesema itaboresha mfumo wake wa kusaka habari mtandaoni, na kuorodhesha matokeo ya utafutaji yaliyochapishwa katika tovuti za magazeti tajika kwanza.
Lakini mwenye anafikiri hatua hii itazima uenezaji wa habari feki pia amekosea. Kampuni ya Opera Mini, kwa mfano, ina mfumo maalumu unaomletea mwenye simu habari nyingi feki ambazo huvutia wasomaji.
Ukweli
Ukweli ni kwamba, licha ya Facebook, Twitter na Google kuzidi kurudisha imani kwa watumizi wake, mfumo mpya wa siasa umezaliwa duniani.
Sasa kuna aina mbili za wanasiasa duniani: wale wanaojua kutumia mitandao ya kijamii kama chombo cha kampeni na wale wanaobwagwa uchaguzini.
Tofauti kati yao ni wazi. Wanaoibuka washindi wanatambua uwezo na nguvu za mitandao ya kijamii. Trump alimwangusha Bi Clinton kutokana na ufuasi wake mwingi kwenye Facebook na Twitter.
Kampeni ya Brexit ilifaulu Uingereza kutokana na matumizi yake ya matangazo ya Facebook, licha ya Theres May kuwa na wafuasi wachache kwenye mitandao ya kijamii.
Kenya
Nchini Kenya, Rais Uhuru Kenyatta ana wafuasi milioni 3.45 , Naibu Rais William Ruto ana wafuasi 2.12 milioni huku Bw Raila Odinga akiwa na ufuasi wa watu milioni 2.06 kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.
Kwenye Facebook, ukurasa wa Rais Kenyatta una wapenzi milioni 3.6, ukurasa wa Dkt Ruto unapendwa na watu milioni 1.1, huku wa Bw Odinga ukiwa na wafuasi milioni 1.2.
Kwa kupitia taarifa, uchanganuzi na propaganda za kisiasa kwenye mitandao hii miwili, ni wazi kwamba wafuasi wa Bw Odinga na Dkt Ruto wanatoshana, lakini wameachwa mbali na wale wa Rais.
Na ni ithibati hii inayoonyesha kuwa Bw Odinga hakuwa na nafasi ya kumwangusha Bw Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 kwa kuwa ameachwa nyuma katika ufuasi wa mitandaoni, na matangazo mengi yaliegemea kumuunga mkono Rais.
Demokrasia katika enzi hizi za dijitali si demokrasia tena, kwani teknolojia ya kiroboti inatumika kubadilisha mawazo na imani ya wapiga kura kote duniani na kuwachochea kubadilisha maamuzi yao.