Tuliandamana mara moja tu na tuna imani tumesikizwa, Gen Z wa Lamu wasema
VIJANA hasa wale wa umri mchanga, almaarufu Gen Zs, Kaunti ya Lamu Jumanne waliendeleza shughuli zao kama kawaida wakati maandamano yakishuhudiwa kwenye maeneo tofauti tofauti ya nchi.
Kwenye miji mikuu ya Lamu, ikiwemo Mji wa Kale wa Lamu, Mokowe, Hindi, Mpeketoni, Kibaoni, Majembeni, Witu, Faza, Pate, Mkokoni, Kiwayu na Kiunga mpakani mwa Kenya na Somalia, shughuli ziliendelea kama kawaida kana kwamba hakuna chochote kilikuwa kikiendelea nchini.
Kinyume na maeneo mengine ya nchi ambako Biashara na usafiri ulitatizwa, miji ya Lamu ilishuhudia maduka yakifunguliwa ilhali usafiri ukiendelea bila tatizo.
Baadhi ya vijana waliohojiwa walisema wao tayari wameshiriki maandamano wiki jana na kwamba hatua hiyo inadhihirisha wazi kuchoshwa kwao na utawala wa serikali ya Rais William Ruto.
Wanasema licha ya kukosa kushiriki maandamano ya Jumanne wiki hii, msimamo wao bado ni ule ule kama wa wenzao wengine nchini kwamba mageuzi yafanyike nchini.
Kiongozi wa vijana hao kisiwani Lamu, Bw Mohamed Omar alisema wanaunga mkono Rais Ruto kujiuzulu.
“Hapa Lamu tayari tumeandamana kwa mara ya kwanza juma lililopita. Hata tukakosa kurudiarudia haya maandamano tunaamini kilio chetu bado kilisikika. Tunaunga mkono mageuzi yafanyike nchini, ikiwemo huyu Zakayo (Rais Ruto) ashuke, yaani ajiuzulu. Msimamo wetu tuliutangaza wiki jana wakati tuliposhiriki maandamano. Haina haja ya kujirudiarudia,” akasema Bw Omar.
Simon Mbuthia, kijana wa Mpeketoni, alisema hawangeshiriki maandamano ya Jumanne kwani wamepanga kufanya hivyo siku ya Alhamisi hii (leo).
“Tumepewa notisi yetu kufanya maandamano Alhamisi wiki hii. Kwa hivyo tunaunga mkono vijana wenzetu kote nchini. Lazima Rais Ruto abanduke mamlakani,” akasema Bw Mbuthia.
Naye Bi Brenda Mwangi aliwarai polisi kutotumia nguvu kupita kiasi kwa waandamanaji.