Makala

UMBEA: Usikilize moyo wako ikiwa unapitia huzuni ya mahaba

August 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SIZARINA HAMISI

HUZUNI ya mahaba hushinda msiba.

Umewahi kusikia maneno hayo ya wahenga?

Kuna watu wamewahi kupagawa, wengine wakakatisha uhai na wengine wakachukia suala zima la uhusiano baada ya kupatwa na huzuni ya mahaba, kukataliwa kimapenzi na kufanyiwa unyama wa moyoni.

Kwa waathirika wa huzuni ya mahaba, huwa sawa na wafiwa waliopoteza wawapendao, hupitia kipindi cha maombolezi sawa na wale waliokuwa kwenye msiba na wapo wanaohitimisha maombelezi hayo, lakini wengine huchukua muda mrefu kufika hitimisho hilo.

Hakuna kipindi kigumu katika uhusiano kama kile unapoachwa ama kuachana na mwenzako kwani unaweza kuhisi kama dunia imefika mwisho. Hasa pale unapoumizwa na yule uliyempenda kwa moyo wako wote.

Kwa kawaida moyo unapopenda kwa dhati, huwa na kawaida ya kujisahau.

Hufikirii kwamba anaweza kukufanyia kitu kibaya, unampa mapenzi kwa moyo wako wote. Unapopenda sana, ndivyo utakavyoumia sana itakapotokea amekubadilikia.

Na ndio maana siku zote unapopenda ni muhimu kubakisha sehemu kidogo katika moyo wake kwa matukio ya kuachwa, kuumizwa ama kukutana na usiyotarajia.

Kwa mtu yeyote ambaye amewahi kupenda kwa dhati na baadaye akaja kuumizwa, atakuwa shahidi kwamba hakuna kitu kinachoumiza moyo kama mapenzi. Kwani kuna baadhi ya watu huwa hawajali kuhusu mioyo ya wenzao, anakufanyia jambo kwa makusudi bila kujua madhara atakayokusababishia.

Wapo ambao kwa sababu ya kushindwa kuyahimili maumivu ya mapenzi, hujikuta wakiyakatisha maisha yao.

Wengine hujikuta wakipoteza kila kitu maishani, sababu ikiwa ni mapenzi. Unakuta mwingine hata kama alikuwa na kazi nzuri, inapotokea amekumbwa na dhoruba ya mapenzi, hawezi tena kufanya kazi kwa ufanisi, muda wote machozi, muda wote anahuzunika, matokeo yake, anashindwa kuendelea na kazi.

Wengine hujikuta wakiingia kwenye ulevi wa kupindukia, ikiwa ni juhudi za kujaribu kutafuta sehemu ya kupunguza machungu. Matokeo yake, wanazalisha matatizo mengine makubwa zaidi na pengine mwisho wao unakuwa ni mauti.

Ni kweli mapenzi yanatesa, lakini inapotokea umeumizwa na mtu uliyempenda kwa moyo wako wote, haimaanishi kwamba huo ndiyo mwisho wa maisha yako. Unaweza kusimama tena, inawezekana kabisa.

Kitu ambacho watu wengi huwa hawakikubali kirahisi, ni ukweli kwamba mapenzi yanatesa. Wengine hujitahidi kuficha maumivu wakijidai kwamba ni jasiri na hawajaumia popote na kujidai wanaendelea na maisha yao, wakati moyoni wanateketea.

Matokeo yake, unalimbikiza tatizo ndani ya moyo wako ambalo litaendelea kukusumbua kwa muda mrefu mpaka utakapotambua namna ya kulishughulikia.

Pale inapotokea kwamba mwenzako unayempenda, ambaye mlikuwa na ndoto nyingi za pamoja, mliyejadili na kupanga mambo mengi pamoja, amekutendea unyama wa moyoni, ameuvunja moyo wako na kukusababishia maumivu makali moyoni, kwanza jipatie muda wa kuwa peke yako kwa muda.

Pale unapopata nafasi ya kuwa peke yako, zungumza na moyo wako, kama unadhani kulia kunaweza kupunguza uchungu moyoni mwako, lia mpaka moyo wako utulie. Jiulize mara kadhaa kuhusu uzito wa kosa alilokufanyia, jiulize mwenyewe, je, baada ya yote hayo unahitaji kuendelea kuwa naye au huwezi tena kuendelea.

Wanachokosea wengi, akishakumbwa na kimbunga cha mapenzi, badala ya kupata muda wa kutosha wa kuwa peke yake, anaanza kuwasimulia marafiki au ndugu akitaka wamshauri nini cha kufanya.

Endapo moyo wako unakwambia kwamba japokuwa amekukosea bado unampenda kwa dhati na unamhitaji, fanya kile moyo unachoona kinafaa. Na endapo moyo wako unaona umefika mwisho kabisa na huwezi kuendelea, usikilize pia moyo wako.

 

[email protected]